Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi
Dar es Salaam. Wamiliki wa vituo vya utangazaji
vya televisheni nchini, wamesema watasitisha kurusha matangazo ndani ya
mwezi mmoja kuanzia sasa kutokana na kushindwa kumudu gharama za
uendeshaji.
Hatua hiyo inatokana na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) kuzima mitambo ya analojia na kuhamia dijitali Desemba
31, mwaka jana kitendo walichodai kimepunguza mapato yanayotokana na
matangazo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya
Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi alisema hakuna haja ya kurusha
matangazo kwa hasara.
Mengi alisema kutokana na kuanza kwa mfumo wa
dijitali, watangazaji wamesitisha kutoa matangazo kwa sababu wananchi
wengi hawana ving’amuzi.
“Kama mamlaka itashindwa kurudisha ule mfumo
wa analojia kuwa sambamba na dijitali hadi wananchi watakapokuwa na
ving’amuzi, tutazima televisheni zetu ndani ya mwezi mmoja ujao,”
alisema Mengi.
“Ibara ya 18 ya Katiba imekiukwa kutokana na
wananchi kunyimwa fursa ya kupata habari, hivyo hali hii hatutaki
iendelee,” alisema Mengi.
Mengi ambaye pia ni mmiliki wa vituo vya
televisheni vya ITV, EATV na Capital TV, alisema licha ya nchi za
Afrika, Tanzania imekuwa ya kwanza kuzima mitambo ilhali wananchi
hawakuwezeshwa kumudu gharama za ving’amuzi.
“Nchi ambazo zimeendelea kwa kila kitu kama
Uingereza, Marekani, Japan na kwingineko kuzima mitambo ya analojia
walitumia zaidi ya miaka minane kwa nini sisi tumewahi hivi wakati
hatujajipanga?” alihoji Mengi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Sahara Media Group na
mmiliki wa Kituo cha Star Tv, Samwel Nyalla alisema hivi sasa
wanaendesha biashara hiyo kwa hasara.
Nyalla alisema hadi mwaka 2015, hali itakuwa mbaya kutokana na kukosa ving’amuzi.
Mkurugenzi
wa Utangazaji wa TCRA, Habby Gunze alisema wao hawakualikwa katika
mkutano huo hivyo hawajui chochote. Gunze alimtaka mwandishi kwenda
ofisini leo.
“Sisi hatujui chochote na kama unataka maelezo
mengine njoo kesho (leo) ofisini kwetu uonane na Mkurugenzi Mkuu
(Profesa John Nkoma), ili tuzungumze kwa ‘fact’ (kwa ushahidi) kipi
kinachoendelea,” alisema Gunze.
Nukuu
“Kama mamlaka itashindwa
kurudisha ule mfumo wa analojia kuwa sambamba na dijitali hadi pale
wananchi watakapokuwa na ving’amuzi tutazima televisheni zetu ndani ya
mwezi mmoja ujao labda TBC ndiyo itakayobaki”.
No comments:
Post a Comment