Mbunge: Sikukimbia mafunzo JKT



Mbunge wa Jimbo la Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine ameibuka na kukanusha taarifa kwamba alikimbia mafunzo maalum ya wiki tatu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yaliyowashirikisha wabunge 47.

Mbunge huyo awali alipangiwa kambi ya Mlale iliyopo Songea, kabla ya kubadilisha na kuhamishiwa kambi ya JKT Ruvu, alitoweka ikiwa imebaki wiki moja ahitimu mafunzo hayo yaliyofanyika katika vikosi mbalimbali nchini, wabunge 23 tu ndio waliofanikiwa kuhitimu.

Mafunzo hayo ya awali kwa wabunge yalifungwa na Rais Jakaya Kikwete Machi 26 mwaka huu, ambapo pia alizindua mafunzo ya miezi mitatu ya Jeshi hilo kwa vijana 4,710 nchi nzima kwa mujibu wa sheria.

Baadhi ya waliohitimu mafunzo hayo Ester Bulaya, Halima Mdee, Neema Hamid, David Silinde, Murtaza Mangungu, Livingston Lusinde, Yusuph Khamis, Said Mtanda na Mendrad Kigola.

Akizungumza Dar es Salaam jana,Nyangwine alisema alishiriki mafunzo mbalimbali, lakini ilipofikia wakati wa kufanya mafunzo msituni aliugua.

“Sikwenda katika zoezi la msituni kwa sababu daktari alinipima na kugundua kuwa nilikuwa na tatizo la shinikizo la damu(BP), kutokana na presha yangu kupanda bila sababu za msingi nilitakiwa kupumzika” alisema Nyangwine.

Alisema licha ya kupumzika bado hali yake ilikuwa mbaya, hivyo kulazimika kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambapo alitakiwa kupumizia kwa zaidi ya siku mbili.

“Kule kambini walinipa ruhusa ambayo haikueleza siku ambayo natakiwa kurudi. Baada ya kupata nafuu wenzangu walikuwa wameshamaliza, lakini cheti changu cha JKT kipo na muda wowote naweza kwenda kukichukua” alisema

Alisema alishindwa kuhudhuria sherehe za kutunukiwa vyeti kwa kuwa alikwenda Mwanza kushiriki mkutano wa wabunge ambao majimbo yao yamezungukwa na hifadhi za wanyamapori.

Mafunzo ya JKT yalianza tena baada ya kufutwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kutokana na kuyumba kwa uchumi, lakini kutokana na umuhimu, Serikali sasa imeamua kuyarudisha ingawa bado yanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na fedha.

Tuhuma nzito: Chadema yamtuhumu Kinana kuhusika na biashara ya pembe za ndovu

Abdulrahman Kinana 

Dodoma. Kambi ya Upinzani Bungeni imetoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ikidai kuwa anajihusisha na mtandao wa ujangili nchini.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amejibu tuhuma hiyo akisema ni za uongo huku akiituhumu kambi hiyo kuwa imedanganya wakati inajua ukweli kuhusu tuhuma dhidi ya Kinana.
Akiwasilisha maoni ya upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013/14, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Maliasili, Mchungaji Peter Msigwa alisema vitendo vya ujangili vimekuwa vikilitia doa taifa kwenye jumuiya za kimataifa.
“Kwa bahati mbaya ni kwamba wahusika wengi ambao wanatajwa kwa ushahidi ni makada maarufu na wengine ni viongozi waandamizi wa CCM,” alisema Mchungaji Msigwa.
“Tumeshuhudia watuhumiwa wengine wa ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi kubwa za uongozi wa taifa hili, licha ya kutajwa kwenye ripoti ya uchunguzi kuhusiana na ujangili.”
Alisema mwaka 2009, meli ya Kampuni ya Wakala wa Meli ya Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa China ikiwa na makontena yenye nyara za Serikali ikiyasafirisha kwenda Hong Kong.
“Nyaraka zilizopo Ofisi za Wakala wa Usajili wa Kampuni na Biashara (Brela), zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Kinana ilisajiliwa Oktoba 2003 na kupewa hati na. 47221.
“Nyaraka zinaonyesha kuwa Kinana anamiliki hisa 7,500 kati ya 10,000 za kampuni hiyo iliyosajiliwa Dar es Salaam. Mshirika mwenzake katika kampuni hiyo, Rahma Hussein ambaye ni mke wake anamiliki hisa 2,500,” alisema Msigwa.

Dk Nchimbi ajibu mapigo
Akijibu tuhuma hizo, Waziri Nchimbi alisema: “Ukiona mtu anasimama na kuamua kusema kuwa hakuna kinachofanywa na wizara kuhusu masuala ya ujangili, ni wazi uelewa wake unakuwa na utata mkubwa.”
Alisema hoja zilizojengwa dhidi ya Kinana ni uongo mtupu... “Nimejaribu kufuatilia kwa makini alichokisema alikimaanisha, alikielewa, alikitafakari au aliandikiwa tu akaenda kusoma? Baada ya kutafakari kwa kina nikagundua hakuwa na nia mbaya, aliandikiwa tu na ameenda kusoma,” alisema Dk Nchimbi.
Alisema ukweli wa jambo hilo ni kwamba ipo tofauti ya majukumu ya kampuni za Wakala wa Meli na shughuli za kupakia mizigo bandarini huku akituhumu kambi ya upinzani kuwa inajua ukweli lakini imeamua kupotosha umma.
Dk Nchimbi ambaye alikuwa mchangiaji wa kwanza, alisema wakala hawezi kuwa mmiliki wa meli, bali anamwakilisha mwenye meli kwenye shughuli ndogondogo zinazofanyika inapofika nchi fulani kama kuhudumia watumishi wa meli, mahitaji muhimu na kufanya usafi.
“Lakini kuna watu wanaitwa ‘clearing and forwarding (Kupakua na kupeleka mizigo). Napenda kukwambia Mchungaji Msigwa kuwa kazi yao ni kupeleka na kutoa mizigo bandarini,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza;
“Kule ndiko kuna utaratibu wa upekuzi, katika utaratibu wa upekuzi mtu wa ‘shipping agency’ (wakala wa meli) hahusiki, sina shaka hata kidogo Mchungaji Msigwa analijua hili ninalolisema, ila amelifumbia macho kwa makusudi kwa masilahi yasiyokubalika katika taifa.”
Alisema kumekuwa na uvumi ambao umekuwa ukifanywa kwa makusudi kuwa Kinana anahusika na meli iliyohusika kusafirisha pembe zile.
“Uvumi huu ni uzushi, meli iliyobeba mizigo ile inaitwa Delmas Nakadha, mmiliki wake anaitwa Bus Herman Ledley jambo hili Kambi ya Upinzani Bungeni inalijua, ila kwa masilahi yasiyokubalika katika taifa wameamua kupotosha Bunge lako,” alisema.
Alisema baada ya uchunguzi wa kutosha, wahusika walibainika na ikafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 3 na 4 ya mwaka 2009 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
“Hawa (anawataja) ndiyo waliopelekwa kortini, uchunguzi ulijidhihirisha kuwa ndiyo watuhumiwa wa jambo hili, Kambi ya Upinzani Bungeni inalijua,” alisema.

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI MAY 1

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

ALIYEZIKWA AKIWA HAI AFUKULIWA NA KUKUTWA AMEKUFA CHUNYA MBEYA


KWANZA KABISA WANAANZA TOA JENEZA LA ALIEKUFA KWA UGONJWA NA KUZANIWA AMEROGWA NA ALIYEZIKWA AKIWA HAI MAANA KATIKA KABURI HILO WALIZIWA WATU WAWILI KATIKA KABURI MOJA  ALIE HAI NA MFU
JENEZA LA ALIEKUFA KWA UGONJWA TAYARI LIMETOLEWA HILO PEMBENI SASA ANAFUKULIWAALIEZIKWA HAI
MWILI WA ALIEZIKWA AKIWA HAI SASA UNATOLEWA KABURINI
HII MITI NDIYO ILIYOTENGANISHA JENEZA NA ALIEZIKWA AKIWA HAI KWANZA ALIANZA ALIE HAI KUZIKWA IKAFUATIA MITI HIYO NDIYO LIKAFUATA JENEZA LA ALIEKUFA KWA UGONJWA
MWILI WA ALIEZIKWA AKIWA HAI BAADA YA KUTOLEWA KABURINI
MDOGO WA MAREHEMU ALIEZIKWA AKIWA HAI

WANANCHI HAO HAIKUTOSHA BAADA YA KUMZIKA MWENZAO AKIWA HAI WALIKWENDA KUCHOMA NYUMBA YAKE
NA KUHARIBU MAZAO YAKE SHAMBANI




KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa kijiji na kata ya Mkwajuni Wilaya ya Chunya Mkoani hapa wamemzika Mwanakijiji mwenzao akiwa hai wakimtuhumu kusababisha kifo cha Mkazi mmoja kijijini hapo.

  

Tukio hilo la kusikitisha limetokea Apri 26 mwaka huu  majira ya Saa Nane Mchana katika Kitongoji cha Maweni Makaburini baada ya Mhanga aliyefahamika kwa jina la Victory Mwachirui(68) kuhudhuria mazishi ya Pita Barton(28)aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Thobias Ismail amesema marehemu alipatwa na umauti akiwa anapatiwa matibabu kwa mganga wa jadi ambaye jina lake halikuweza kujulikana maramoja.

Amesema wakati taratibu za mazishi zikiendelea Ndugu wa marehemu walidai kuwa kifo cha Marehemu kilisababishwa na Mwachirui ambaye ni Katekista mstaafu kwa imani za kishirikina.

Ameongeza kuwa wakati kaburi likichimbwa kwa ajili ya kumzika  marehemu ndipo vijana waliokuwa wakichimba waliagiza Wazee wa Mila wafike makaburini kwa ajili ya kuangalia utaratibu wa mazishi na kukagua ukubwa wa Kaburi ambalo lilikuwa limekwisha chimbwa.

  

Kutokana na mwito huo walifika wazee wanne akiwemo Mzee Mwachirui ambaye walimsisitiza kusogea jirani na kaburi ambapo baada ya kusogea alipigwa na Sururu kichwani na kuangukia kaburini huku akisindikizwa na marungu.

  

Baada ya Mzee huyo  kupoteza fahamu Vijana hao walianza kutandika fito ndani ya kaburi kisha kufukia kwa udongo kiasi kwa lengo la kutenganisha na Mwili wa Marehemu Pita uliokuwa kwenye jeneza baada ya kuwazika kwenye kaburi moja.

  

Baada ya kukamilika kwa zoezi la mazishi kundi la vijana lilielekea hadi nyumbani kwa Mzee aliyezikwa akiwa hai na kuiteketeza nyumba yake huku wakiapa kutotoa siri wakidai Siri ya Jeshi.

  

Hata hivyo baadhi ya wananchi walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Credo Kayanza ambaye pia alitoa taarifa kwa Diwani wa Kata hiyo Chesco Ngairo ambao kwa pamoja walitoa taarifa Jeshi la Polisi ambao baada ya taarifa hiyo walifika eneo la tukio huku wakidhani lililotokea ni kuchomwa kwa nyumba pekee.

  

Jeshi la Polisi baada ya kufanya upelelezi na kubaini kitendo hicho waliwaamuru baadhi ya Vijana kufukua kaburi hilo zoezi ambalo lilifanyika baada ya Vijana hao kulipwa.

  

Baada ya kufukuliwa kwa kaburi hilo Mwili wa Marehemu Mzee Mwachirui ulichukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Misheni ya Mkwajuni kwa ajili ya Uchunguzi huku Mwili wa Pita ukizikwa upya palepale.

  

Baada ya kukamilika kwa uchunguzi mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi ambapo Marehemu alizikwa katika eneo tofauti na alipokuwa amefukiwa awali.

  

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo pia ametoa wito na kuwaasa  wananchi na jamii kuacha tabia  ya kuamini mambo ya ushirikina na uchawi kwa madai kuwa hauna faida kwao bali huchochea migogoro katika jamii zao.

Aidha ameongeza kuwa wakumbuke kitendo cha kujichukulia sheria mkononi ni kosa kisheria ambapo pia  amewaomba wenye taarifa za walipo waliohusika na mauaji hayo kuzifikisha polisi haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ingawa hakuna aliyekamatwa kuhusika na tukio hilo.

NJAA CHAMWINO

Na John Banda, Chamwino

VIJIJI  vyote 77  vya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma vimekumbwa na baa la njaa   kutokana na ukame mkali uliodumu kwa miezi miwili mfurulizo.

Ukame huo ulio ulioanza mwanzoni mwa mwezi wa kwanza mpaka mwishoni mwa  mwezi wa pili umefanya hali ya chakula kuwa mbaya Wilayani humo hali inayozidi kutishia maisha ya watu.

Akitoa taarifa ya hali ya chakula Afsa kilimo wa Wilaya ya Chamwino kwenye Baraza la Madiwani lililofanyika jana  Gofrey  Mnyamale  alisema kutonyesha Mvua kwa kipindi hicho kumesababisha  hata zao la Mtama ambalo huwa linastahimili ukame kukauka.

Alisema  katika msimu wa kilimo wa Mwaka 2012/13 wilaya ilijiwekea malengo ya kulima Hekta 118, 071 za mazao ya chakula na kutarajia kuvuna tani 105, 040 kama Mtama,  Mahindi na uwele  lakini malengo hayo yamepotea.

Aliongeza kuwa Mvua nyingi zililizonyesha katika mtiririko usioridhisha hasa Mwezi Desemba na kufuatia na ukame mkali katika miezi hiyo miwili kuliwapoteza watu waliozoea kupanda mapema kutokana na hali ya hewa ya mkoa wenyewe.

Mnyamale alitanabaisha kuwa waliamua kuwaagiza wananchi kutunza chakula kidogo walichonacho, wenye mifugo kuuza ili kununua chakula, kuzuia wafanyabiashara wasitoe nje chakula na kufanya tasmini ya kina ili taarifa ipelekwe kwa Waziri mkuu mapema iwezekanavyo.

‘’Tunataka baada ya kukamilisha Tathimini hii Taarifa itapelekwa haraka kwa Waziri Mkuu ili hatua za haraka za kunusuru watu dhidi ya janga la njaa zichukuliwe  mapema mapema iwezekanavyo ambapo tunatarajia kabla  Mei 10 mwaka huu kuwa imekamilika’’, alisema

Kwa upande wake Mjumbe wa Nec ya CCM Samwel Malecela aliitaka Selekari kuchukua hatua za Halaka ili kunusuru hali ya njaa katika Wilaya nyingi kutokana na upungufu wa chakula kuwa kila sehemu.

‘’ Janga hili ni kubwa  na Mala nyingi Selekari imekuwa ikisema inafanya upembuzi yakinifu na inatumia muda mwingi kupembua katika hili nawaambia wafanye haraka kwani hali ni mbaya mno bora kitu kingine kuliko njaa’’, alisema

Malecela Aliongeza kuwa yeye kwa nafasi yake anatembea kila wilaya na amebakiza chache ili amalize na sehemu kubwa inatatizo la kukosa chakula hivyo serekali ihakikishe inatoa kipaumbele kuanzia na wilaya zilizoathirika sana kama hiyo ya Chamwino anakotokea.

MWISHO  

Mbowe amtwisha mzigo mzito Zitto

 

Tabora. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemwagiza Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe kuhakikisha chama kinapata ushindi katika majimbo mengi kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mbowe alisema chama chake kitahakikisha kinachukua majimbo ya Samwel Sitta, (Urambo Mashariki), Ismail Aden Rage (Tabora mjini) na Jimbo la Kaliua la Profesa Juma Kapuya, katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mbowe alimwagiza mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kuhakikisha kwamba majimbo hayo yanachukuliwa na Chadema katika uchaguzi mkuu ujao.

Alimtaka kufanya kampeni za mtaa kwa mtaa, nyumba kwa
hadi nyumba na mtu kwa mtu ili kuhakikisha kwamba wabunge hao wa sasa katika majimbo hayo hawachaguliwi tena na wananchi katika uchaguzi huo.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Town School mjini Tabora, pamoja na mambo mengine alisema anazindua kampeni hiyo kwa ajili ya mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi ambapo Zito Kbwe alikabidhiwa jukumu la kuisimamia  kanda hiyo.

Aliwageukia polisi na kuwataka kukiunga mkono chama hicho ili kikifanikiwa kuingia madarakani kiweze kuwaboreshea mishahara yao kuliko ilivyo sasa akidai wanalipwa mishahara kiduchu ikilinganishwa na ugumu wa kazi yao.

“Nyie makamanda nanyi mmepigika kama sisi, sasa ninachowaomba tuungeni mkono kupambana na hawa CCM ili tuwakomboe wanyonge,” alisema Mbowe.

Awali Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe alisema Kanda ya Magharibi ina historia katika nchi kwa Mkoa wa Tabora kuwa kitovu cha mapambano ya uhuru wa nchi na Kigoma kuwa kitovu cha mapambano ya mageuzi.

Lema kizimbani Arusha leo

Mbunge wa Arusha Mjini,Godbless Lema. 

Dar/mikoani. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema anafikishwa mahakamani leo kwa madai ya kuchochea vurugu katika Chuo cha Uhasibu Arusha,(IAA) huku ikielezwa kwamba jiji hilo litakuwa katika ulinzi mkali.
Ulinzi umeimarishwa maradufu katika mitaa yote jijini Arusha na Kituo Kikuu cha Polisi anakoshikiliwa mbunge huyo tangu usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita.

Lema anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo akidaiwa kuchochea vurugu katika chuo hicho baada ya wanafunzi kuchachamaa kutokana na mauaji ya mwenzao, Henry Kago aliyeuawa kwa kisu karibu na chuo hicho, Jumanne iliyopita.

Ingawa Jeshi la Polisi linadai ulinzi huo ni jukumu lao la kawaida la kila siku, lakini wingi wa askari mitaani umechagizwa na tukio la kukamatwa na kufikishwa mahakamani leo kwa Lema suala linalotokana na rekodi ya wafuasi wa Chadema hasa kukiwa na jambo linalomhusisha mbunge wao na polisi.

Tangu baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2010, wafuasi, wapenzi na viongozi wa Chadema Arusha na kitaifa wamekabiliana mara kadhaa na Polisi mkoani hapa na moja ya matukio yanayokumbukwa ni lile la maandamano ya Januari 5, 2011 lililoishia kwa mauaji ya watu wawili huku viongozi kadhaa wa chama hicho wakifunguliwa kesi ya kusanyiko lisilo halali.

Viongozi wa Chadema wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa, Lema, wabunge kadhaa na viongozi wa ngazi ya wilaya na mikoa. Polisi kutoka wilaya jirani na Arusha za Arumeru, Monduli, Karatu na Longido wanahusika katika ulinzi huo ulioimarishwa tangu juzi.

Wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani wamekuwa na desturi ya kujaa mahakamani pale viongozi wao wanaposhtakiwa kwa kosa lolote na hutoka kwa maandamano yasiyo rasmi kila kesi inapoahirishwa, jambo ambalo limekuwa likizua mvutano kati yao na polisi na aghalabu kuishia kuwatawanya kwa mabomu ya machozi na baadhi kutiwa mbaroni.

Ulinzi mkali ‘selo’ ya Lema
Polisi wameimarisha ulinzi katika eneo lote la Kituo Kikuu anakoshikiliwa mbunge huyo tangu Ijumaa iliyopita na tangu siku hiyo, watu ambao wamekuwa wakifika hapo kwa sababu mbalimbali wamelazimika kujieleza kwanza kwa askari wa doria kabla ya kuruhusiwa kukaribia lango la kituo hicho.

Katika mitaa mbalimbali nako kuna askari wenye silaha wanaotembea kwa miguu wakiwa wawiliwawili hadi watatu pamoja wale wa pikipiki na wa kikosi cha mbwa na farasi.

Kesi nyingine kubwa za leo
Mbali na kesi hiyo, huenda leo Mahakama Kuu ikatoa uamuzi wa maombi ya Jamhuri katika rufani ya kesi ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Jerry Murro na wenzake wawili.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa uamuzi wa kama Muro na wenzake wawili, Edmund Kapama maarufu kama ‘Dokta’ na Deogratius Mugassa wapandishwe kizimbani tena na kuanza kusikiliza upya kesi ya rushwa iliyokuwa ikiwakabili au la.

Kesi nyingine ni ya anayedaiwa kumuua Padre Evaristus Mushi ambaye atapandishwa kizimbani kwa mara ya tatu.

Mtuhumiwa huyo, Omar Yusufu Makame, mkazi wa Mwanakwerekwe, Unguja alikamatwa Machi 29, mwaka huu baada ya uchunguzi uliofanywa na wapelelezi wa Tanzania walioshirikiana na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI). Pia leo kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) Ltd, Iddi Simba na wenzake na inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 

Mara ya mwisho kesi hiyo iliahirishwa, kwa sababu Hakimu Mkuu Mfawidhi, IIvin Mugeta anayeisikiliza alikuwa na shughuli nyingine za kiofisi. Mbali na Simba, washtakiwa wengine ni Meneja wake, Victor Milanzi na Mkurugenzi wa Shirika, Salim Mwaking’ida.

Katika Mahakama ya Kinondoni, dereva aliyemgonga Askari wa Usalama Barabarani, WP 2492 CPL-Elikiza na kusababisha kifo chake, Jackson Fimbo atafikishwa mahakamani leo.
Dereva huyo alimgonga askari huyo wakati msafara wa Rais Jakaya Kikwete ukipita katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Kesi nyingine itakuwa huko Liwale ambako watu 31 akiwamo Diwani wa Kata ya Liwale B, Mohamedi Mtesa (CUF), wanatarajiwa kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Liwale leo wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kuharibu mali na kuchoma nyumba za mbunge, viongozi wa  vyama vya ushirika vya msingi na Mwenyekiti wa halmashauri.

Idadi hiyo ya watuhumiwa itafanya watu 68 kupandishwa kizimbani baada awali, watu 37 kufikishwa mahakamani Alhamisi iliyopita.

Mjini Sumbawanga, Rukwa, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Samweli Kisabwiti na Diwani wa Kata ya Katandala (CCM), leo anafikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Sumbawanga kwa tuhuma za kutishia kujeruhi kwa panga.

Imeandikwa na James Magai (Dar), Juddy Ngonyani (Sumbawanga), Christopher Lilai (Lindi), Mussa Juma na Peter Saramba (Arusha) na Masoud Sanani (Zanzibar).

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI APRIL 29

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.