Abdulrahman Kinana
Dodoma. Kambi ya Upinzani
Bungeni imetoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
ikidai kuwa anajihusisha na mtandao wa ujangili nchini.
Hata hivyo,
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amejibu tuhuma hiyo
akisema ni za uongo huku akiituhumu kambi hiyo kuwa imedanganya wakati
inajua ukweli kuhusu tuhuma dhidi ya Kinana.
Akiwasilisha maoni ya
upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili
na Utalii mwaka 2013/14, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Maliasili,
Mchungaji Peter Msigwa alisema vitendo vya ujangili vimekuwa vikilitia
doa taifa kwenye jumuiya za kimataifa.
“Kwa bahati mbaya ni kwamba
wahusika wengi ambao wanatajwa kwa ushahidi ni makada maarufu na wengine
ni viongozi waandamizi wa CCM,” alisema Mchungaji Msigwa.
“Tumeshuhudia
watuhumiwa wengine wa ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi
kubwa za uongozi wa taifa hili, licha ya kutajwa kwenye ripoti ya
uchunguzi kuhusiana na ujangili.”
Alisema mwaka 2009, meli ya Kampuni
ya Wakala wa Meli ya Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa
China ikiwa na makontena yenye nyara za Serikali ikiyasafirisha kwenda
Hong Kong.
“Nyaraka zilizopo Ofisi za Wakala wa Usajili wa Kampuni na
Biashara (Brela), zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Kinana ilisajiliwa
Oktoba 2003 na kupewa hati na. 47221.
“Nyaraka zinaonyesha kuwa
Kinana anamiliki hisa 7,500 kati ya 10,000 za kampuni hiyo iliyosajiliwa
Dar es Salaam. Mshirika mwenzake katika kampuni hiyo, Rahma Hussein
ambaye ni mke wake anamiliki hisa 2,500,” alisema Msigwa.
Dk Nchimbi ajibu mapigo
Akijibu
tuhuma hizo, Waziri Nchimbi alisema: “Ukiona mtu anasimama na kuamua
kusema kuwa hakuna kinachofanywa na wizara kuhusu masuala ya ujangili,
ni wazi uelewa wake unakuwa na utata mkubwa.”
Alisema hoja
zilizojengwa dhidi ya Kinana ni uongo mtupu... “Nimejaribu kufuatilia
kwa makini alichokisema alikimaanisha, alikielewa, alikitafakari au
aliandikiwa tu akaenda kusoma? Baada ya kutafakari kwa kina nikagundua
hakuwa na nia mbaya, aliandikiwa tu na ameenda kusoma,” alisema Dk
Nchimbi.
Alisema ukweli wa jambo hilo ni kwamba ipo tofauti ya
majukumu ya kampuni za Wakala wa Meli na shughuli za kupakia mizigo
bandarini huku akituhumu kambi ya upinzani kuwa inajua ukweli lakini
imeamua kupotosha umma.
Dk Nchimbi ambaye alikuwa mchangiaji wa
kwanza, alisema wakala hawezi kuwa mmiliki wa meli, bali anamwakilisha
mwenye meli kwenye shughuli ndogondogo zinazofanyika inapofika nchi
fulani kama kuhudumia watumishi wa meli, mahitaji muhimu na kufanya
usafi.
“Lakini kuna watu wanaitwa ‘clearing and forwarding (Kupakua
na kupeleka mizigo). Napenda kukwambia Mchungaji Msigwa kuwa kazi yao ni
kupeleka na kutoa mizigo bandarini,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza;
“Kule
ndiko kuna utaratibu wa upekuzi, katika utaratibu wa upekuzi mtu wa
‘shipping agency’ (wakala wa meli) hahusiki, sina shaka hata kidogo
Mchungaji Msigwa analijua hili ninalolisema, ila amelifumbia macho kwa
makusudi kwa masilahi yasiyokubalika katika taifa.”
Alisema kumekuwa na uvumi ambao umekuwa ukifanywa kwa makusudi kuwa Kinana anahusika na meli iliyohusika kusafirisha pembe zile.
“Uvumi
huu ni uzushi, meli iliyobeba mizigo ile inaitwa Delmas Nakadha,
mmiliki wake anaitwa Bus Herman Ledley jambo hili Kambi ya Upinzani
Bungeni inalijua, ila kwa masilahi yasiyokubalika katika taifa wameamua
kupotosha Bunge lako,” alisema.
Alisema baada ya uchunguzi wa
kutosha, wahusika walibainika na ikafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi
namba 3 na 4 ya mwaka 2009 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam.
“Hawa (anawataja) ndiyo waliopelekwa kortini, uchunguzi
ulijidhihirisha kuwa ndiyo watuhumiwa wa jambo hili, Kambi ya Upinzani
Bungeni inalijua,” alisema.
No comments:
Post a Comment