Mbunge: Sikukimbia mafunzo JKT



Mbunge wa Jimbo la Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine ameibuka na kukanusha taarifa kwamba alikimbia mafunzo maalum ya wiki tatu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yaliyowashirikisha wabunge 47.

Mbunge huyo awali alipangiwa kambi ya Mlale iliyopo Songea, kabla ya kubadilisha na kuhamishiwa kambi ya JKT Ruvu, alitoweka ikiwa imebaki wiki moja ahitimu mafunzo hayo yaliyofanyika katika vikosi mbalimbali nchini, wabunge 23 tu ndio waliofanikiwa kuhitimu.

Mafunzo hayo ya awali kwa wabunge yalifungwa na Rais Jakaya Kikwete Machi 26 mwaka huu, ambapo pia alizindua mafunzo ya miezi mitatu ya Jeshi hilo kwa vijana 4,710 nchi nzima kwa mujibu wa sheria.

Baadhi ya waliohitimu mafunzo hayo Ester Bulaya, Halima Mdee, Neema Hamid, David Silinde, Murtaza Mangungu, Livingston Lusinde, Yusuph Khamis, Said Mtanda na Mendrad Kigola.

Akizungumza Dar es Salaam jana,Nyangwine alisema alishiriki mafunzo mbalimbali, lakini ilipofikia wakati wa kufanya mafunzo msituni aliugua.

“Sikwenda katika zoezi la msituni kwa sababu daktari alinipima na kugundua kuwa nilikuwa na tatizo la shinikizo la damu(BP), kutokana na presha yangu kupanda bila sababu za msingi nilitakiwa kupumzika” alisema Nyangwine.

Alisema licha ya kupumzika bado hali yake ilikuwa mbaya, hivyo kulazimika kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ambapo alitakiwa kupumizia kwa zaidi ya siku mbili.

“Kule kambini walinipa ruhusa ambayo haikueleza siku ambayo natakiwa kurudi. Baada ya kupata nafuu wenzangu walikuwa wameshamaliza, lakini cheti changu cha JKT kipo na muda wowote naweza kwenda kukichukua” alisema

Alisema alishindwa kuhudhuria sherehe za kutunukiwa vyeti kwa kuwa alikwenda Mwanza kushiriki mkutano wa wabunge ambao majimbo yao yamezungukwa na hifadhi za wanyamapori.

Mafunzo ya JKT yalianza tena baada ya kufutwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kutokana na kuyumba kwa uchumi, lakini kutokana na umuhimu, Serikali sasa imeamua kuyarudisha ingawa bado yanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na fedha.

No comments:

Post a Comment