JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamsaka Richard
Jecap (30) mkazi wa kitongoji cha Matai A kwa tuhuma za kumuua baba yake
kwa kumpiga mpini kichwani akimtuhumu kuwa ni mshirikina.
Tukio hilo lilitokea Aprili 18 saa 4.50 asubuhi wakati baba huyo akiwa amekaa nyumbani kwake akiota jua.
Akizungumza na gazeti hili, mwenyekiti wa kijiji
hicho, Emmanuel Mwakibinga alisema kuwa mtuhumiwa alifanya mauaji hayo
baada ya watoto wake kufariki ambapo mtoto wa kwanza mwenye umri wa
miaka minne alifariki Januari mwaka huu na alikuwa akidai baba yake huyo
ndiye aliyemloga.
Alisema kuwa Aprili 16 mtoto wake wa pili mwenye
umri wa miaka miwili alifariki na alidai kuwa baba yake ndiye aliyemloga
kwani amekuwa akiloga watoto wake hao na siku ya mazishi aliahidi
kumfanyia kitu kibaya baba yake huyo licha ya kuwa hakueleza ni kitu
gani.
Mwenyekiti huyo alisema siku ya tukio hilo alikuwa
akipita karibu na nyumba hiyo akasikia kishindo kikubwa kutoka eneo la
nyumba hiyo na kisha kufuatia vilio vya watu na aliposogea alikuta
mtuhumiwa huyo amekwishampiga mpini kichwani baba yake huyo na kisha
kuanguka na kupoteza fahamu.
Baada ya kuona hivyo, walisaidiana pamoja na
wanafamilia wengine kumwahisha hospitali na alitundikiwa maji sambamba
na kushonwa katika jeraha kubwa alilolipata kichwani na usoni na kisha
kulazwa ili kuendelea kupata matibabu.
Mwakibinga alisema kuwa wakati akiendelea kupatiwa
matibabu alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi na maumivu
makali aliyokuwa nayo katika jeraha alilolipata baada ya kupigwa na
mpini wa shoka kichwani.
No comments:
Post a Comment