Iringa. Wabunge wawili
machachari wa CCM, Deo Filikunjombe (Ludewa) na Kangi Ligola (Mwibara)
wamemfagilia Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa wakimwelezea kuwa ni
kiongozi mchapakazi.
Filikunjombe na Ligola walikaribishwa kuzungumza
wakati wa Lowassa alipokabidhiwa tuzo maalumu na Kanisa la Overcomers
Power Centre (OPC) Mjini Iringa jana na kumtaka asikate tamaa licha ya
madhila ya kisiasa yaliyomkuta, bali aendelee kusaidia jamii.
Wabunge hao wanajulikana kutokana na ujasiri wao wa kutoa hoja kali bungeni na hata kuikosoa Serikali bila woga.
Hivi karibuni, ndiyo wao pekee kutoka CCM waliopinga hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ligola alimwagia
sifa Lowassa akisema licha ya maneno mengi yanayosemwa juu yake na
matukio yaliyomkuta, lakini bado anaendelea kuitumikia jamii kwa bidii
kupitia siasa na kazi za kanisa.
Alisema kama ilivyokuwa kwa Yesu ambaye alipigwa
na kunyanyaswa na kuyaacha yote kwa Mwenyezi Mungu, Lowassa naye
aliandamwa na watu waliomzushia kesi kama Yesu kiasi cha kuamua
kujiuzulu uwaziri mkuu.
“Mnakumbuka kuwa waliomchukia Yesu walimfungulia mashtaka ya uongo wakamfikisha mbele ya Pilato.
Walipoambiwa watoe ushahidi wakashindwa, lakini
wakapiga kelele asulubiwe. Yesu alipigwa, akatemewa mate lakini yeye
akasema, “Ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke, lakini si kama nitakavyo
mimi bali mapenzi ya Mungu yatimizwe.”
“Vivyo hivyo Edward, aliposakamwa sana aliamua
hata kujiuzulu uwaziri mkuu. Lakini tunajua kuwa Yesu baada ya kuuawa,
alifufuka na kuinuliwa. Naomba Kanisa liendelee kumwombea Lowassa ili
naye ainuliwe juu katika nchi yetu ya Tanzania,” alisema Lugola katika
shughuli hiyo, ambayo ilihudhuriwa pia na wabunge Ritha Kabati (Viti
Maalumu – CCM) na Menrad Kigola (Mufindi Kusini – CCM).
Filikunjombe kwa upande wake, naye alimwaga sifa
akimtaka kutokatishwa tamaa na maneno yanayosemwa na watu: ... “Siku
zote mti wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe.”
“Hii Tuzo ya Ramani ya
Tanzania ambayo Lowassa umetunukiwa leo ina maana kubwa sana... Baba
Askofu hukumpa ramani ya Monduli, au ramani ya Iringa, au Ludewa, amempa
ramani ya Tanzania, ina maana kubwa sana,” alisema Filikunjombe.
Pia hafla hiyo ilihusisha uchangiaji wa kusaidia ujenzi wa Kanisa la OPC na kituo cha redio.
Lowassa alilazimika kujiuzulu wadhifa wa Waziri
Mkuu mwaka 2008 baada ya Serikali kukumbwa na kashfa ya kutoa zabuni ya
kuzalisha umeme kwa Kampuni ya Richmond wakati ikiwa haina uwezo.
Kitendo hicho cha Lowassa kuungwa mkono na wabunge
hao kinaonekana kama kumjengea mazingira mazuri katika mbio za kuwania
urais kupitia CCM mwaka 2015 kwani amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa
makada wa chama hicho wanaotaka kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lowassa, ambaye pia ni Mbunge wa
Monduli (CCM), alivitaka vyombo vya habari kuhakikisha kuwa vinafanya
kazi zake kwa uadilifu mkubwa ili kutunza amani ambayo ndiyo tunu kubwa
ya nchi.
Alisema uzoefu unaonyesha kuwa vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika kutunza au kuvuruga amani.
Alisema vyombo hivyo vinapaswa kuwa makini katika
kuchapisha na kutangaza habari za matukio mbalimbali ili kuepuka
kulitumbukiza taifa pabaya.
No comments:
Post a Comment