Ni kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa
mamilioni ya fedha za manispaa hiyo kama zilivyoibuliwa na Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Tabora. Halmashauri ya Manispaa
ya Tabora, imewafukuza kazi Mchumi, Mhasibu na Mhandisi wa Ujenzi wa
Manispaa hiyo.Orodha hiyo inamjumuisha pia Ofisa Utawala wa Manispaa.
Hatua
hiyo imekuja siku kadhaa baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali, kubaini ufisadi wa kutisha katika Manispaa ya Tabora.
Watumishi hao wamefukuzwa kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha wakati wakiwa kazini.
Habari
za ndani ya Manispaa ya Tabora, zinasema watumishi hao sasa wanasubiri
kupewa barua zao za kuachishwa kazi. Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Meya wa Manispaa ya Tabora, Gullamhusein Dewji, alisema watumishi
hao, wamefukuzwa kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo
ubadhilifu wa mamilioni ya fedha.
Hivi karibuni katika taarifa yake kwa vyombo vya
habari, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, alibaini ufisadi
wa zaidi Sh2 blioni katika Manispaa ya Tabora.
Hali hiyo imeisababishia manispaa hiyo kupata
hati chafu, huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia akitangaza kuipunguza ruzuku ya fedha za
maendeleo kutoka asilimia 100 hadi 50 katika mwaka huu wa fedha.
Mwaka jana aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya
Tabora ambaye alihamishiwa Wilaya ya Uyui, Hadija Makuwani,
aliwasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za
ubadhilifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka.
No comments:
Post a Comment