Uhuru kuapa kama Obama


Uhuru Kenyatta 


Mke wake ndiye atamshikia Biblia na yeye atakuwa anaishika kwa kuweka mkono kama  alivyofanya Rais Obama wa Marekani

Nairobi. Rais Mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema kwamba wakati wa kuapishwa hataapa kwa kuinua Biblia bali atasaidiwa na mkewe kama alivyoapishwa Rais Obama wa Marekani.
Mkuu wa Majeshi ya Kenya (KDF), Jenerali Julius Karangi alisema jana kuwa Kenyatta aliomba  mkewe Margaret Kenyatta amshikie Biblia atakapokuwa akiapishwa.

“Hili ni ombi la rais mteule na itakuwa vyema tukubali ombi lake katika siku hii ya kihistoria,” alisema Jenerali Karangi.
“Mke wangu atanishikia biblia kisha nitaweka mkono kama alivyofanya Omaba,hakuna Rais wa Kenya aliefanya hivyo” alisema

Kenyatta ataweka  tu mkono wake wa kushoto juu ya Biblia ikishikiliwa na mkewe, katika kile anachotaja hatua ya kuachana na mtindo wa awali wa kuapisha marais wa Kenya wakiinua Biblia.

Kenyatta ataiga mfano wa Rais Barack Obama wa Amerika, alipoapishwa hadharani mjini Washington DC mnamo Januari 21, 2013, ambapo aliomba mkewe Michelle Obama amshikie Biblia.

Siku hiyo Rais Mwai Kibaki atamkabidhi katiba mpya Kenyatta, ambayo ilianza kutumika mnamo Agosti 2010. Mtindo huu utakuwa wa kwanza tangu nchi hiyo kupata Uhuru. Sherehe hiyo itafanywa katika Uwanja wa Michezo wa Moi Kasarani, ambapo pia Naibu wa Rais William Ruto ataapishwa.
Shughuli hiyo inatarajiwa kumalizika saa 7.45. Kamati ya Mamlaka ya Ofisi ya Rais tayari ina ratiba ya mpangilio wa shughuli hiyo.
Ratiba hiyo ina picha ya rais anayeondoka katika ukurasa wa pili na ya  Kenyatta katika ukurasa wa tatu. Kamati hiyo imeteua Rais Yoweri Museveni kuzungumza kwa niaba ya wageni wote waalikwa siku hiyo.

Hapo jana asubuhi, kamati hiyo inayoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Francis Kimemia, ilisema kwamba shughuli itaanza rasmi 5:45 asubuhi Rais Kibaki atakapowasili uwanjani.

Kulingana na mpangilio uliopo, wageni watahitajika kusimama Rais Kibaki akiwasili, wakati wa sherehe ya kuapishwa, saluti ya mizinga 21 itakapopigwa nje ya uwanja na wimbo wa taifa utakapoimbwa kabla ya Rais Kibaki na rais mpya kuondoka uwanjani.

Siku hiyo,  Kenyatta atapambwa kwa vifaa vya mamlaka ambavyo ni pamoja na Mkuu wa Nakshi (CGH), pia atapokea mkuki, ngao na katiba.

Zana hizo zinaashiria mamlaka; kwa mfano Katiba inasimamia Kenya na watu wake, mkuki unasimamia Amiri Jeshi Mkuu ilhali CGH ni heshima kubwa zaidi Kenya.

No comments:

Post a Comment