Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Wilaya ya Arumeru, Ester Malleko.
TANZANIA inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa Rais
wa awamu ya tano mwaka 2015. Uchaguzi huo pia utahusisha nafasi za
ubunge na udiwani ukitanguliwa na ule wa serikali za mitaa mwakani.
Mengi yanazungumzwa kuhusu chaguzi hizo, ikiwemo
uwezekano kuwa na Rais, Makamu wake au Waziri Mkuu mwanamke kutokana na
uwezo wa kiuongozi unaoonyeshwa na wanawake waliopata fursa za uongozi.
Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), wilaya ya Arumeru, Ester
Malleko anazungumzia nafasi na uwezekano huo kama alivyozungumza na
Mwandishi Wetu, Peter Saramba.
Swali: Nini kilikusukuma kuingia kwenye siasa na nini malengo yako ya baadaye?
Jibu:
Nimeingia kwenye siasa kuwatumikia wananchi na kuthibitisha kuwa
wanawake tunaweza. Nimekuwa mwenyekiti wa UVCCM wilaya na sasa
ninaongoza wanawake.
Nafasi ya mwanamke kwenye jamii siyo kuzaa na
kutunza familia pekee. Tunapaswa na hakika tuna haki ya kushiriki katika
ujenzi wa taifa sawasawa na wanaume kwa kila mmoja kutekeleza na
kutimiza wajibu wake pale alipo.
Swali: Wewe ni mwanachama na
kiongozi wa CCM. Kuna madai kwamba chama chako kimepoteza haiba mbele ya
umma kutokana na ninyi viongozi kuacha misingi iliyoasisi chama hicho.
Nini maoni yako?
Jibu: CCM kama taasisi haina tatizo
na haijapoteza haiba. Bado ipo na itaendelea kudumu katika misingi yake
ile ile iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili ambayo ni amani, upendo,
udugu na mshikamano bila kujali tofauti zetu za kikabila, kidini wala
maeneo mtu anakotoka.
Chama hiki bado kinaaminiwa na umma. Hilo
linathibitishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo CCM ilipewa ridhaa ya
kuunda Serikali baada ya kushinda kiti cha urais na kupata wabunge na
madiwani wengi.
Hata hivyo, ni kweli kuna kosoro ndogo ndogo
zinajitokeza kutokana na makosa ya watu binafsi ambazo zinashughulikiwa
kupitia vikao, katiba, kanuni na taratibu za chama.
Swali: Mwaka
2015 tunaingia kwenye uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, kuna
maneno kuwa wanawake waliopata fursa wameonyesha uwezo mkubwa
kiuongozi. Unadhani muda umefika wa kuwa na Rais, Makamu au Waziri Mkuu
mwanamke?
Jibu: Muda umefika, tena unapita. Ninaamini Taifa hili linaweza
kuongozwa na mwanamke kwa sababu viongozi wanawake waliopata fursa za kuongoza wameonyesha kuwa wanaweza.
Wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na kutoa uamuzi wa haraka wenye faida na maslahi kwa umma.
Wanawake viongozi wamethibitisha kuwa hawapigi dili kama ambavyo mama nyumbani asivyoweza kuisaliti familia.
Swali: Unaweza kutaja kwa uchache majina ya wanawake unaodhani wana uwezo wa kuwa Rais wa taifa hili?
Jibu:
Wapo wanawake wengi wanaonivutia katika uongozi wao. Baadhi wapo kwenye
nafasi zao uongizi hadi sasa katika medani mbalimbali ikiwemo uongozi
wa kisiasa, kijamii na harakati mbalimbali.
Ingawa wako wengi ambao
siwezi kuwataja wote, lakini kwa uchache wapo Dk Asha Rose Migiro, Dk
Hellen Kijo-Bisimba, Profesa Anna Tibaijuka, Ananilea Nkya, Mama Anna
Abdalah, Mama Gertrude Mongella na Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano, Anne Makinda.
Swali: Kuna msemo kwamba mwanamke anaweza akiwezeshwa. tupe maoni yako?
Jibu: Binafsi sikubaliani na msemo huo, kwani unafifisha uwezo wa
kijiamini kwa wanawake ambao hukaa kutegemea kuwezeshwa ndipo wafanye jambo.
Siyo
kweli kwamba ili mwanamke afanikiwe au kuweza jambo lazima awezeshwe.
Nadhani kauli hii iliyotumika huko nyuma kuwahamasisha na kuwatia moyo
wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi sasa imepitwa na wakati.
Mimi
naamini uwezo wa mwanamke upo dhahiri ndiyo maana nyuma ya kila
mwanaume shupavu na mwenye mafanikio, yupo mwanamke shupavu na jasiri.
Na huu unathibitishwa na usemi kuwa “Kila mwanaume aliyefanikiwa,nyuma
yake kuna mwanamke”
Kifamilia, mshauri mkuu wa baba ni mama. Sasa
tutakubali vipi kwamba ili mwanamke afanikiwe lazima awezeshwe?
Awezeshwe na nani? Huyo huyo mwanaume ambaye yeye anamshauri?
Hata
hivyo, pamoja na ukweli huo, lazima tukubali kwamba adui wa mwanamke ni
mwanamke mwenyewe. Wanawake hatujiamini. Lakini hata anapotokea mwenzetu
kujiamini na kujitokeza, hatumuungi mkono, pengine kwa ile
ile dhana kuwa hatuwezi au wivu tu wa kike.
Swali:
Jiji la Arusha ni miongoni mwa halmashauri zenye chaguzi ndogo za
madiwani kujaza nafasi zilizo wazi. Unatarajia chama chako kitamudu
kurejesha kata hizo nne zilizonyakuliwa na upinzani uchaguzi uliopita?
Jibu:
Yeyote anayeingia kwenye mashindano, lengo lake ni kushinda. CCM tuna
matumaini makubwa ya kushinda baada ya kugundua na kurekebisha makosa
madogo madogo yaliyosababisha tupoteze kata hizo.
Tumesimamisha
wagombea wanaokubalika na tumejiandaa kuwanadi kukamilifu kupitia sera
za chama. Hatutatukana wala kuzungumzia watu binafsi kama wenzetu
wanavyofanya. Tutanadi sera ili kutoa fursa kwa wananchi kuzilinganisha
na za wenzetu.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaasa watu wa Arusha tusikubali
kutenganishwa
wala kufarakanishwa kutokana na chaguzi hizi. Ni kweli kila mtu ana
haki ya kufuata na kuamini itikadi aipendayo kisiasa, tufanye hivyo bila
kubezana, kufarakana wala kusababisha ufa kwenye uhusiano wetu.
Baada
ya uchaguzi huu na zingine zijazo, Arusha inapaswa kuendelea kuwa
sehemu salama kwa maisha na mali zetu. Wananchi tunataka ufumbuzi wa
matatizo yanayotukabili kwa pamoja bila kujali tofauti zetu kisiasa,
kidini wala kibabila.
No comments:
Post a Comment