'Mafisadi wanamtisha Mkurugenzi Mkuu wa NHC'

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu

Serikali imeombwa kumwekea ulinzi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu, kutokana na vitisho ambavyo ameanza kupata kutoka kwa mtandao wa mafisadi waliojimilikisha nyumba za shirika hilo baada ya mirija yao ya wizi kukatwa na mkurugenzi huyo.

Ombi hilo lilitolewa jana bungeni mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Magdalena Sakaya, wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Sakaya alisema Mchechu  amekuwa akifanya kazi nzuri tangu aingie NHC, lakini mafisadi wachache ambao walikuwa na mirija ya kufanya ufisadi ndani ya shirika hilo wamekuwa wakimwandama na wakati mwingine wakimtumia ujumbe wakumtisha ili kumkatisha tamaa asiendelee na jitihada zake za kupambana na ufisadi uliokuwapo.

“Mheshimiwa Spika, wale mafisadi baada ya kuona mirija yao imekatwa wanamtumia ujumbe wa vitisho wakimwambia kuwa kijana  umekuja na utaondoka... naomba serikali imlinde, Mkurugenzi huyu ni  kijana mdogo, lakini mzalendo wa kweli na amefanyakazi kubwa sana,” alisema Sakaya.

Akizungumza na NIPASHE nje ya ukumbi wa Bunge, Sakaya alisema kuna watu ambao walikuwa wamehodhi nyumba nyingi za NHC na kuzikodisha kwa watu kwa bei kubwa huku wakilipa fedha ndogo kwa shirika hilo.

Sakaya alisema kuna watu ambao walikuwa wanaingiza hadi Sh. 7, 000, 000 kwa mwezi kwa kupangisha nyumba za NHC, hivyo ujio wa Mchechu umekuwa balaa kwao kwani mirija mingi imefungwa.

Alisema kuna watu walikuwa wanamiliki hadi nyumba nne za NHC na kuzikodisha kwa bei kubwa kwa watu mbalimbali, hivyo baada ya kuona mirija hiyo imekatwa wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ikiwamo kumtisha Mchechu.

“Mimi nimekuwa mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa zaidi ya miaka saba, ningekuwa na tamaa ya mali ningekuwa na hata ghorofa namiliki sasa, lakini siko hivyo, mimi nataka NHC iwe mali ya Watanzania na iwanaufaishe Watanzania, hakuna ndugu yangu hata mmoja anayeishi NHC ingawa ningetaka wangepata,” alisema Sakaya na kuongeza:

“Nimefuatwa mara nyingi na wafanyabiashara wakiniuliza ninataka Shilingi ngapi ili niwatetee bungeni wauziwe nyumba, lakini nimekataa kwa sababu mimi ni mzalendo na sitaki ufisadi kabisa, ningetaka utajiri ningeshaupata kupitia NHC.”

Mbunge huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia hadi baadhi ya wabunge kuwatetea bungeni wengine wakitaka Mchechu aondolewe kwenye nafasi hiyo ili waendelee kula.

Alisema kabla ya Mchechu kuingia NHC, kulikuwa na mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wanaohodhi nyumba hizo za shirika hilo na ndio wanaohangaika hadi kuwatumia baadhi ya wabunge wakitaka serikali iwauzie zile nyumba na isiwaongezee kodi wapangaji na wengine wakiishauri serikali imwondoe Mchechu.

“Usione kila anayefoka kuhusu NHC ukadhani ana uchungu na Watanzania wanyonge, wengine wametumwa na wafanyabiashara hao hao ambao wana mtandao unaomiliki nyumba za NHC, hakuna mlalahoi wanayemtetea, wanataka wauziwe zile nyumba ili wazilangue kwa bei kubwa,” alisema Sakaya na kuongeza:

“Alichofanya Mchechu kimewaathiri mafisadi wengi sana waliokuwa wanalinyonya shirika, unakuta mfanyabiashara amempangisha mtu nyumba moja ya  NHC na analipwa Shilingi 1,000,000 kwa mwezi wakati NHC anakwenda kulipa 400,000, sasa kilichofanyika NHC imewafuata wale waliopangishwa na wafanyabiashara na kuwapa mikataba yenyewe ili wailipe NHC badala ya wale walanguzi hapo ndipo wanahangaika.”

Sakaya aliishauri pia serikali iondole Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa vifaa vya ujenzi  kwa NHC ili wajenge nyumba bora na za bei nafuu ambazo Watanzania wa hali ya chini watamudu kuzinunua.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Kiwelu, alisema ni aibu kwa serikali kushindwa kulipa madeni inayodaiwa na NHC wakati kila mwaka bajeti imekuwa ikitengwa kwa ajili ya kulipia pango.

Alisema kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ambayo yeye ni mjumbe inamuunga mkono Mkurugenzi wa NHC, lakini amekuwa akikwamishwa na serikali ambayo inashindwa kulipa madeni ya muda mrefu, hivyo kushindwa kujenga nyumba mpya.

“Bajeti tunapitisha kila mwaka hapa, lakini hamlipi pango la NHC, Waziri tunaomba utueleze hizo fedha huwa mnazipeleka wapi?” alihojiu na kuongeza:  “Tunaomba katika bajeti hii Wizara inayodaiwa deni lake lipelekwe Hazina ikatwe huko huko wapewe NHC.”

Alishauri NHC ikipata fedha za kutosha ijenga nyumba za matabaka ya wenye nazo na nyumba ambazo watu wa tabaka la chini kabisa watamudu kuzinunua kwa kuwa za sasa hakuna mlalahoi atakayezimudu.

Kiwelu alisema inasikitisha kuona kuwa Tume nyingi zimeundwa kuchunguza mambo zikitumia fedha zinazotokana na kodi wanazolipa walalahoi, lakini ripoti hizo huwa haziwekwi hadharani.

Alitoa mfano wa Tume ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuchunguza majengo 100 jijini Dar es Salaam, lakini kwa mshangao mkubwa kamati yake imeitafuta kwa muda mrefu na haijulikani iliko.

“Tumeitafuta ripoti ya Tume ya Lowassa, lakini tumeikosa na hadi sasa ripoti hiyo haijulikani iliko, sasa naomba Waziri atueleze iliko ili isomwe na ifanyiwe kazi kwa kuwa kuna majengo zaidi ya 100 ambayo ilisemekana ni mabovu na yanapaswa kubomolewa,” alisema.

Herbert Mtango (Lushoto-CCM), alisema kuna wawekezaji ambao wamejilimbikizia mashamba makubwa miaka 40 iliyopita bila kuyaendeleza, lakini bado wanamiliki hatimiliki za mashamba hayo.

Alisema licha ya mashamba hayo kugeuka mapori kwa miaka yote hiyo huku wawekezaji hao wakiwa nje ya nchi, serikali imeshindwa kuzifuta hati hizo na kusababisha wananchi wengi wa Muheza kukosa sehemu za kuendesha shughuli za kilimo.

“Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa sana, mwekezaji anapewa hati ya kumiliki shamba kwa miaka 99 na sasa kwa zaidi yamiaka  40 iliyopita ameshindwa kuendeleza shamba, lakini anaendelea kumiliki ardhi wakati wazawa hawana ardhi,” alisema.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment