Serikali inavyoulea mgogoro wa gesi Mtwara

Tangu mgogoro wa kupinga gesi itakayozalishwa mkoani Mtwara uliponza kufukuta Desemba 2012, Serikali imeshindwa kutatua kiini chake, badala yake nguvu kubwa za kijeshi zimetumika kiasi cha kusababisha mauaji, majeruhi na chuki kwa wananchi.

Kimsingi mgogoro huu unatokana na maoni ya wananchi kuhusu rasilimali ya gesi inayotarajiwa kuchimbwa mkoani humo wakitaka gesi hiyo isisafirishwe kwa bomba kwenda Dar es Salaam.

Awali Serikali ndiyo iliyounda kamati ya Nishati na Madini ambayo ilipita kwa wanachi nchini kote kutaka maoni yao. Ilipofika Mtwara, wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirishwa kwa gesi.

Desemba mwaka 2012, vyama tisa vilifanya mikutano na hatimaye maandamano ambayo hata hivyo yalisusiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Joseph Simbakalia.

Mbali na maandamano hayo, mapema mwaka huu, kulijitokeza vurugu wilayani Masasi ambazo zilihusishwa na madai ya gesi japo chanzo chake hakikuwa hicho.

Hapo ndipo viongozi wa Serikali wakaanza kutembelea Mtwara ili kutuliza hali ya mambo. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika Mtwara mapema mwaka huu na kuzungumza na makundi ya wananchi, yaani, vyama vya siasa, Maaskofu na Masheikh, wazee na vijana.

Baada ya hapo yakafanyika majumuisho yaliyohusisha makundi hayo ambayo hata hivyo hayakuwaridhisha wananchi.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda alizuia mjadala wa suala hilo Bungeni,  akidai kuwa kuna kamati imeundwa kuchunguza.

Licha ya Waziri Mkuu Pinda kushindwa kuafikiana na Wanamtwara katika ziara yake, akarudi Bungeni na kutoa taarifa kuwa mambo yamekwisha, hivyo na ile kamati ya Bunge iliyotumwa kuchunguzwa ikayeyuka.

Kama wanavyosema Waswahili, ‘La kuvunda halina ubani’, ule uvundo aliouacha Pinda Mtwara, sasa umezua vurugu upya Mei 22 ambapo watu wamekufa, kujeruhiwa na wengine kubakwa.

Pinda amerudi tena Mtwara kufanya mazingaombwe yake. Bunge nalo baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, imeunda tena kamati ya Wabunge iende kufuatilia suala hilo.

Tujiulize, kwa nini ile kamati ya kwanza ya Bunge iliyosababisha suala hilo lisijadiliwe ilivunjwa kabla haijaanza kazi?

Hii yote ni kuonyesha kuwa Serikali ndiyo inayoulea mgogoro huu, kwa sababu haitaki kuwasikiliza wananchi ili kufikia mwafaka. Huo ndiyo mzizi wa tatizo.

Suluhisho siyo kuleta majeshi ya kutuliza ghasia, ni kuwasikiliza wananchi, kwani wao ndiyo msingi wa mamlaka ya Serikali  kwa mujibu wa Katiba ibara ya nane.

No comments:

Post a Comment