Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
akijibu hoja za wabunge waliochangia Makadirio na Mapato ya wizara yake
kwa mwaka wa fedha 2013/14, bungeni, Dodoma jana.
Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema kuwa kitendo cha kuvutana na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhusu kesi ya ardhi iliyomhusu raia wa
Tanzania mwenye asili ya Kichina, Jingling Li ilikuwa ni kuzingatia
sheria na siyo kwamba alikuwa na urafiki naye.
Alisema hayo akinukuu taarifa iliyoandikwa na
gazeti hili toleo la wiki iliyopita, wakati akijibu hoja za wabunge
wake kuhusu bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2013/14.
Alinukuu taarifa ya gezeti hili akisema kuwa NHC
walishindwa kwenye kesi hiyo hatua ya rufani kama alivyokuwa ametabiri
hapo awali akionyesha umuhimu wa kufahamu sheria za ardhi na makazi.
“Gazeti la Mwananchi waliandika ninavutana na
Shirika la Nyumba ikaonekana kana kwamba namtetea Mchina labda kutokana
na kwamba kuna masilahi ninayopata,” alisema Profesa Tibaijuka na
kuendelea:
“Huyu raia wa Tanzania mwenye asili ya China,
alikuwa ni mkalimani wa Baba wa Taifa (Hayati) Mwalimu (Julius) Nyerere.
Alishinda kwenye kesi hiyo na kurejeshwa kwenye nyumba hiyo,” alisema
Profesa Tibaijuka.
Alisema kwa sasa NHC hawana namna nyingine ya
kufanya kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa kwenye ngazi ya rufaa. Alizungumza
hayo akionyesha umuhimu wa kuwepo na vyombo vya usuluhishi wa kesi
zinazohusiana na ardhi.
Gazeti hili liliripoti kuwako kwa mvutano wa chini kwa chini baina ya Profesa Tibaijuka na uongozi wa NHC.
Mvutano huo ulitokana na uamuzi wa NHC kuukatia
rufaa uamuzi wa Mahakama Kuu (Kitengo cha Ardhi), uliompa haki, Jingling
Li katika kesi ya ardhi namba 129 ya 2006 dhidi ya shirika hilo na
wadaiwa wengine wawili.
Katika kesi hiyo, Li alikuwa akilalamikia hatua
ya kuondolewa kwenye nyumba Nambari 103 iliyopo katika vitalu namba 3,
5, 7 na 8, Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay, Dar es Salaam.
Kesi dhidi ya NHC ilifunguliwa mwaka 2006 wakati
shirika hilo likiongozwa na Martin Madekwe na imedumu kwa miaka sita
hadi Aprili mwaka jana ilipotolewa hukumu wakati shirika hilo likiwa
chini ya Nehemia Mchechu aliyeteuliwa mwaka 2010.
Katika hukumu yake ya Aprili 27, 2012, Jaji
Atuganile Ngwala aliamuru NHC pamoja na washtakiwa wa pili na wa tatu
katika shauri hilo; Lars Eric Hulstrom na Kampuni ya Udalali ya Manyoni,
wamlipe Li karibu Sh478 milioni ikiwa ni fidia ya hasara na usumbufu
uliosababishwa na kuhamishwa kwake kinyume cha sheria katika nyumba
hiyo.
Mchanganuo huo unahusisha Sh70 milioni na Dola za
Marekani 177,450 (Sawa na Sh283, 920,000 - Dola moja ni sawa na
Sh1,600), gharama za kesi pamoja na riba ambazo pia zinapaswa kulipwa.
Pia Mahakama hiyo iliamuru Li arejeshwe katika makazi hayo, amri
ambayo inamaanisha kuondolewa katika nyumba hiyo kwa mpangaji
aliyeingizwa badala ya Li ambaye ni Hulstrom aliyekuwa mdaiwa wa pili
katika kesi hiyo.
Baada ya kupokea nakala ya hukumu ya Jaji Ngwala,
NHC waliazimia kukata rufaa kupinga uamuzi huo, lakini habari kutoka
ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinadai kwamba
Waziri Tibaijuka alitoa maelekezo ya mdomo kwamba hakukuwa na haja kwa
shirika hilo kukata rufaa. Hata hivyo, NHC walishindwa rufaa hiyo.
No comments:
Post a Comment