Vurugu kubwa Iringa, Mchungaji Msigwa mbaroni

Iringa. Mji wa Iringa uligeuka kuwa uwanja wa vita kati ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wafanyabiashara jana asubuhi. Watu 50 walikamatwa kutokana na tukio hilo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.

Katika vurugu hizo, gari la zimamoto lilivunjwa kioo na gari lingine dogo liliharibiwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamhanda alisema Mchungaji Msigwa alikamatwa saa saba mchana kwa tuhuma za kuhusika na vurugu hizo na kwamba watu wapatao 50 walikuwa wamekamatwa katika fujo hizo zilizochukua karibu saa tatu.

“Mchungaji Msigwa amekamatwa kwa makosa ya uchochezi, kufanya maandamano bila kibali na kuhamasisha watu kufanya biashara kwenye eneo ambalo limekatazwa kisheria.

Tumemkamata na hatutamwachia hadi uchunguzi wa suala hili utakapokamilika. Pia na hao watu wengine,” alisema Kamanda Kamhanda.

Alisema waliamua kufanya doria katika eneo hilo baada ya kupata taarifa za kiitelijensia kuwa wafanyabiashara walikuwa na mpango wa kuwashambulia mgambo wa Iringa kama wangekwenda kuwazuia.

Vurugu hizo zilichangiwa na mvutano uliokuwa unafukuta kwa muda mrefu kati ya Uongozi wa Manispaa na Mbunge huyo kuhusu amri ya kuzuia watu kufanya biashara kwenye Barabara ya Mashine Tatu, Iringa.

Uongozi wa Manispaa ya Iringa ulitoa tangazo Aprili 28, mwaka huu ukipiga marufuku kufanya biashara katika eneo hilo jambo ambalo lilipingwa na Mchungaji Msigwa na wafanyabiashara hao.

Alfajiri

FFU walianza kuimarisha ulinzi katika Barabara ya Mashine Tatu tangu alfajiri jana na wafanyabiashara hao walipofika kwenye eneo hilo walikuta limezingirwa na polisi.

Kusambaa kwa taarifa hizo kulimfikia Mchungaji Msigwa ambaye alifika hapo saa mbili asubuhi na kuanza kuzungumza na wafanyabiashara hao.

Watu walipomwona ndipo wakamzunguka na kuanza kuimba nyimbo za kumsifu na kumshangilia: “Rais wetu... Rais wetu... Rais wetu.”

Maofisa wa Polisi walimfuata Mchungaji Msigwa na kumwomba aondoke lakini aligoma akidai ni mwakilishi halali wa wananchi kwa hiyo hawezi kuondoka.

Badala yake alipanda kwenye gari lake na kuanza kuzunguka eneo hilo huku akifuatwa na umati wa watu. Polisi nao walikuwa wakimfuatilia kwa magari yao.

No comments:

Post a Comment