Ubakaji India : Aliyemtetea mbakaji kufutiwa leseni

Baadhi ya waandamanaji wakiandamana kupinga vitendo vya ubakaji.


Tofauti na Tanzania, nchini India Serikali inaonekana kuwawajibisha ipasavyo wenye kuendesha vitendo vichafu vikiwamo vya ubakaji.

Lilivyo kubwa tatizo la ubakaji nchini India, ni sawa na hapa kwetu Tanzania lilivyo la dawa za kulevya. Hata hivyo, tofauti kubwa ni namna viongozi wanavyotoa uamuzi kwa wenye kutenda maovu. Wiki hii nchi hiyo imetoa hukumu ambayo imetoa matumaini kwa wananchi wake.

Mfagizi,  Akshay Thakur, Mwalimu wa Mazoezi,  Vinay Sharma, Muuza Matunda, Pawan Gupta na Mukesh Singh walihukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kubaka, kuua na kula njama za kupoteza ushahidi.

Mahakama iliwahukumu wote wanne kunyongwa na mmoja ambaye alikuwa chini ya umri wa miaka 18, mwezi uliopita alihukumiwa kifungo maalumu cha miaka mitatu.

Hata hivyo wakati hukumu hiyo ikiwa katika hatua za utekelezaji, wakili, AP Singh aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa wawili kati ya hao huenda akafutiwa leseni yake.

Singh ameingia matatani baada ya kutoa kauli ambayo imewakera mawakili wenzake na kumwamuru aombe msamaha na iwapo hata fanya hivyo atafutiwa leseni yake.

Wakili huyo baada ya kusikia hukumu hiyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mwenye makosa katika kesi hiyo ni binti huyo ambaye alikuwa akitembea usiku.

“Binti yangu akitembea usiku kama huyu, nitamnyonga mbele za watu, tunatakiwa tuwafundishe adabu mabinti zetu ili wasipate mabalaa kama haya, tukio hili liwe fundisho,” anasema Singh.

Umoja wa Wanasheria nchini India, The Delhi Bar Council (DBC) umemtaka Singh kuomba msamaha kwa jamii na familia ya binti huyo kwa kuwa kama mwanasheria alipaswa kusimamia haki.

Katibu wa umoja huo, Murari Tiwari amesema Singh anapaswa kuomba radhi kwani kitendo chake cha kukubali kuwatetea watuhumiwa wa ubakaji na kauli yake, vinashusha hadhi yake.

Hata hivyo Singh amesema anasimamia kauli yake na anajivunia kuwa mmoja wa watetezi wa vijana hao. Ameongeza kuwa anasubiri kufutiwa leseni naye atachukua hatua nyingine kupigania haki yake kama wakili.

Shambulio la kutisha

Binti wa miaka 22 akiwa na mpenzi wake walitekwa baada ya kupanda basi walilokuwemo wabakaji hao. Walikuwa wakitokea kuangalia sinema, wakalisimamisha basi hilo.

Mwanamume ambaye alinusurika katika tukio hilo anasema baada ya kuwateka waliwapiga , kuwang’ata kwa meno na kisha kuingiza chuma katika sehemu za siri za mwanamke huyo.

Baadaye waliwatupa kandokando ya barabara na wao kutokomea. Walipoamka walijikuta hospitalini lakini hali ya mwanamke ilikuwa mbaya zaidi na alihitaji matibabu ya hali ya juu. Alipelekwa nchini Indonesia hata hivyo hakupona  na kufariki dunia wiki mbili baadaye. Nchini India kuna zaidi ya kesi 1,098 za ubakaji.

Ingawa familia za watuhumiwa zinasema Serikali imewatumia vijana hao kama njia ya kuwaridhisha raia wake, lakini vipimo vya vinasaba (DNA) katika alama za meno zinaonyesha ni za vijana hao. Hata mwanamume aliyenusurika katika tukio hilo anathibitisha kuwa washambuliaji ni vijana hao sita.

“Binti yangu amepata haki leo, tumefurahishwa sana na hukumu hii,” anasema baba wa binti aliyefariki katika tukio hilo.

Wakati hukumu hiyo ikisomwa, baba wa binti huyo alikuwa amekaa chini  amejiinamia huku akibubujikwa machozi lakini ghafla aliibuka na kuruka juu baada ya kusikia wamehukumiwa kunyongwa.

Anasema tangu binti yake aliposhambuliwa, alibatizwa jina la Nirbhaya ambayo maana yake ni Isiyo na Woga.

Nirbhaya amekuwa nembo ya wanawake ambao hushambuliwa kila baada ya dakika 21. Nchini India matukio ya ubakaji, udhalilishaji na matukio ya kumwagiwa tindikali hutokea kila baada ya dakika 21.

Hukumu hiyo itapelekwa mahakama kuu ya nchi hiyo na majaji wawili wataiangalia na kuipitisha au kuifuta adhabu hiyo.Hata hivyo utekelezaji wake unaweza kuchukua miaka mingi.

Tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, mmoja wa watuhumiwa, Ram Sigh alijinyonga akiwa katika chumba chake gerezani Machi mwaka huu.

Hata hivyo hali ya mambo hapa nchini inaonekana kuwa tofauti, ni suala la kawaida kuona mawakili wakitetea hata wauza dawa za kulevya au watu wengine ambao wanaonekana wazi kufanya maovu yenye ushahidi kwa jamii.

Ni wakati wa Watanzania kuweka masilahi ya taifa mbele kwa kupigana vilivyo na watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wanachangia kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

 Makala haya yameandikwa na Julieth Kulangwa kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari.

No comments:

Post a Comment