MBOWE: ACHENI KUINGILIA TUME YA WARIOBA

MWENYEKITI wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Taifa Freeman Mbowe, amesema Kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kuingilia tume ya jaji Joseph Warioba iliyoteuliwa na rais ili kuleta katiba mpya yenye neema kwa watanzania ni Uoga wa kuondolewa madarakani.
Amesema tume ya jaji Warioba haikujitengenezea maoni yake ili kuwafurahisha wananchi bali maoni yaliyomo kwenye rasmu ya katiba ni maoni ya wananchi ambayo hayatakiwi kuingiliwa na chama chochote.
Mbowe amesema hayo jana jumatatu kwenye uwanja wa Magereza mjini Geita ikiwa ni ziara yake ya vuguvugu la mabadiliko''M4C''Pamoja Daima akitokea wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
Amesema kuingilia tume ya mabadiliko ya katiba kuhusu maoni ya wananchi yaliyokusanya na tume unatokana na kubaini mapema kwamba kufikia mwaka 2015 chama kilichoko madarakani ccm itang'oka madarakani.

Mbowe amesema endapo serikali haitalifanyia marekebisho daftari la wapiga kura Chadema kitwahamasisha wananchi nchi nzima wasishiriki kupiga kura za maoni ya katiba.

Aidha ameitaka serikali kurekebisha daftari hilo ili kutoa fursa kwa watanzania wengi kushiriki kuipigia kura maoni ya katiba na chaguzi mbalimbali zijazo ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa,na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Majalada kesi yasombwa na mafuriko Moro

Magole. Wakati Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Magole, Fredy Mbogela akisema kesi zote zilizokuwa zikisikilizwa katika mahakama hiyo ambayo imesombwa na maji pamoja na mafaili yote, zitaanza upya, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa Morogoro wanahaha kukusanya takwimu za waathirika wa mafuriko.

Mafuriko makubwa yalitokea katikati ya wiki iliyopita Kijiji cha Magole, huku yakisababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. Pia, mafuriko hayo yalisomba majalada ya kesi mbalimbali mahakamani hapo.

Akizungumza jana, Hakimu Mbogela alisema hivi sasa kesi zote za jinai zilizokuwa zikisikilizwa mahakamani hapo zitafunguliwa na kusomwa na kusikilizwa upya.

“Polisi ndiyo watakaofungua na kuzipeleka kesi hizo katika mahakama hiyo, kwa sababu wao wanazo kumbukumbu za kesi hizo kupitia kwa waendesha mashtaka na wapelelezi,” alisema Hakimu Mbogela na kuongeza:

“Hakuna kesi itakayofutwa kutokana kuharibiwa majalada hayo, kama nilivyosema polisi watazileta kesi mahakamani, hata kama kulikuwa na kesi iliyokuwa imekaribia hukumu itaanza upya.” alisema.

Alisema: mahakama itaanza kufanya kazi baada ya kufanyiwa usafi na kuweka samani.

Alisema hatua ya awali ambayo inaendelea kufanywa, ni kusafisha jengo la mahakama hiyo ndani na nje kwa kutoa matope, magogo ya miti na taka nyingine ambazo zilikwama eneo hilo na kwamba, utaratibu wa utendaji unaendelea kufanywa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Nestory Munjunangoma alisema Idara ya Mahakama kwa kushirikina na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wapo kwenye mchakato wa ukaguzi na tathmini ya uharibifu wa jengo la mahakama hiyo.

Munjunangoma alisema hivi sasa jitihada za kufanya ukaguzi na upembuzi yakinifu zinafanyika kabla ya TBA kutoa ushauri kulingana na uharibifu uliotokea kamajengo hilo linaweza kukarabatiwa ama kujengwa upya.

Alisema hivi sasa shughuli za mahakama hiyo zimesimama, kuruhusu usafi wa mazingira.

Mauaji yazidi kutikisa Tarime

Tarime. Hali ya usalama Tarime imezidi kutoweka baada ya jambazi lisilofahamika likiwa na bunduki ambayo haijafahamika aina yake kuendelea kuua watu kwa risasi hasa wa jinsi ya kiume, ambapo idadi ya waliouawa imefikia saba hadi sasa na inadaiwa huwaua watu na kupotea bila kutambuliwa.

Jambazi hilo lisilofahamika liliua watu hao usiku wa Januari 27, mwaka huu katika maeneo ya Nkende likianza na kumuua Mwendesha Bodaboda, Juma Marwa Mkazi wa Nkende mjini Tarime akiwa anaelekea nyumbani kwake ambaye alikufa akiwa hospitali akipatiwa matibabu.

Mganga wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Marco Nega alisema tangu Januari 27 hadi sasa hospitali imeendelea kupokea watu waliouawa na majeruhi ambao wamefanyiwa uchunguzi na kugundulika wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi katika sehemu mbalimbali za mwili na kwamba watu wapatao 7 wamekwisha kufa mpaka sasa.

“Tumepokea maiti za watu na majeruhi na tumewafanyia uchunguzi wakagundulika wana majeraha ya risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo tayari watu saba wamekufa wengine wamekufa wakiwa njiani wakienda kwenye matibabu Musoma, marehemu hadi ni saba,” alisema Nega.

Waliojeruhiwa wakosa huduma ya X-ray

Watu waliojeruhiwa wameshindwa kupatiwa huduma ya X-Ray kutokana na Hospitali ya Wilaya kutokuwa na huduma hiyo kwa muda wa zaidi ya miezi 3 na kusababisha wagonjwa kusafirishwa kwenda Musoma na Mwanza kwa matibabu, ambapo Samweli Richard amekufa akiwa njiani kuelekea Musoma kwenye matibabu ikiwamo huduma hiyo ya X-ray.

Hospitali ya Wilaya yashindwa kutoa huduma

Huduma kwa wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya imeshindwa kuendela vilivyo baada ya kupatwa na misiba miwili ya watumishi wawili, ni baada ya waume zao kuuawa na jambazi hilo lisilofahamika.

Awali Januari 26 jambazi hilo lilimuuwa Robert Kisiri (45) mkazi wa Mugabiri ambapo Mstaafu wa JWTZ Zacharia Mwita(58) na Erick Makanya (25)wote wakazi wa Kijiji cha Mogabiri Kata ya Kitare Wilayani Tarime walikutwa wakiwa wameuawa na miili yao ikiwa na majeraha ya risasi mbavuni kushoto na mgongoni.

Pia jambazi hilo liliwajeruhi watu watano kwa risasi ambao ni Mgosi Marwa Mkazi wa Mogabiri, Joseph Richard Mkazi wa Rebu, Gastor Richard Mkazi wa Rebu, Juma Mwita Mkazi wa Mogabiri na Mkandarasi Binafsi wa ujenzi, Mwasi Yomami ambao kati ya hao wawili wamefariki wakati wakipatiwa matibabu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha amesema wamemkamata mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mhusika wa mauaji ambaye yuko chini ya ulinzi kwa mahojiano na kwamba anazidi kuongeza vikosi vya doria kuimarisha ulinzi na usalama na kuwasaka wahalifu.

Wananchi wacharuka

Wananchi Mjini Tarime waliitaka polisi kuhakikisha jambazi hilo linapatikana vinginevyo walitaka polisi kuwakabidhi bunduki ili waweze kumsaka jambazi huyo.

‘Kamanda kashindwa kazi haiwezekani mtu mmoja aue watu 7 ndani ya siku mbili, huu ni uzembe wa polisi katika kuimarisha ulinzi, tunaomba tukabidhiwe bunduki tulisake jambazi,” alisema mwananchi mmoja.