Magole. Wakati Hakimu Mkazi
Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Magole, Fredy Mbogela akisema kesi zote
zilizokuwa zikisikilizwa katika mahakama hiyo ambayo imesombwa na maji
pamoja na mafaili yote, zitaanza upya, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa
Morogoro wanahaha kukusanya takwimu za waathirika wa mafuriko.
Mafuriko makubwa yalitokea katikati ya wiki
iliyopita Kijiji cha Magole, huku yakisababisha uharibifu mkubwa wa mali
na miundombinu. Pia, mafuriko hayo yalisomba majalada ya kesi
mbalimbali mahakamani hapo.
Akizungumza jana, Hakimu Mbogela alisema hivi sasa
kesi zote za jinai zilizokuwa zikisikilizwa mahakamani hapo
zitafunguliwa na kusomwa na kusikilizwa upya.
“Polisi ndiyo watakaofungua na kuzipeleka kesi
hizo katika mahakama hiyo, kwa sababu wao wanazo kumbukumbu za kesi hizo
kupitia kwa waendesha mashtaka na wapelelezi,” alisema Hakimu Mbogela
na kuongeza:
“Hakuna kesi itakayofutwa kutokana kuharibiwa
majalada hayo, kama nilivyosema polisi watazileta kesi mahakamani, hata
kama kulikuwa na kesi iliyokuwa imekaribia hukumu itaanza upya.”
alisema.
Alisema: mahakama itaanza kufanya kazi baada ya kufanyiwa usafi na kuweka samani.
Alisema hatua ya awali ambayo inaendelea kufanywa,
ni kusafisha jengo la mahakama hiyo ndani na nje kwa kutoa matope,
magogo ya miti na taka nyingine ambazo zilikwama eneo hilo na kwamba,
utaratibu wa utendaji unaendelea kufanywa.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Mkoa wa Morogoro, Nestory Munjunangoma alisema Idara ya Mahakama kwa
kushirikina na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wapo kwenye mchakato wa
ukaguzi na tathmini ya uharibifu wa jengo la mahakama hiyo.
Munjunangoma alisema hivi sasa jitihada za kufanya
ukaguzi na upembuzi yakinifu zinafanyika kabla ya TBA kutoa ushauri
kulingana na uharibifu uliotokea kamajengo hilo linaweza kukarabatiwa
ama kujengwa upya.
Alisema hivi sasa shughuli za mahakama hiyo zimesimama, kuruhusu usafi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment