Mikoani. Sakata la matumizi ya
Mashine za Elektroniki za Kutolea Risiti (EFD), limechukua sura mpya
baada ya wafanyabiashara mikoa mbalimbali kuja juu wakisema matumizi
yake yanalenga kuwaangamiza katika biashara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara
hao wameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufikiria upya mfumo wa
kuzitumia, vinginenyo watajikuta wanaingia kwenye mgogoro mkubwa baina
yao.
Tayari, wafanyabiashara miji ya Iringa, Songea na
Mara wametoa msimamo wa kugomea matumizi ya mashine hizo na kuazimia
kufunga biashara zao kama njia ya kupinga matumizi yake.
Wafanyabiashara wa Manispaa ya Iringa, jana
walitangaza mgomo usio na kikomo kwa sababu mashine hizo
zinawasababishia hasara. Wanadai mashine hizo licha ya kununuliwa kwa
bei kubwa, inawabidi kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi na kodi nyingine
wanajikuta wakitumia sehemu za mitaji yao.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma
aliwataka wafanyabiashara kuacha migomo isiokuwa na tija wala sababu,
badala yake wafikishe malalamiko yao kwa uongozi husika kupitia viongozi
wao.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa
Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Mara, Baltazar Gibogo alisema mgomo huo
ni halali yao, kwani Serikali inawanyanyasa wananchi wake.
Gibogo alikanusha kuwa Serikali imeshindwa
kukusanya kodi hadi kubuni kutumia mashine, bali chanzo kikubwa ni
kukithiri kwa rushwa baina ya wafanyabiashara wakubwa na wafanyakazi wa
TRA.
Mjini Mbeya, wafanyabiashara walishauri Serikali
kuzitoa bure mashine za EFD ili kuwasaidia wafanyabiashara kujijenga
kibiashara badala ya kufilisika.
“Pamoja na kwamba Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA)
inasema mfanyabiashara akinunua anaweza kurudisha fedha zake kwa
kupunguza zile za kodi, ukweli unabaki palepale kwamba wafanyabiashara
hawana fedha taslimu kununua kitu ambacho siyo cha kuuza na kupata fedha
kwa wakati huo,’’ alisema Anania Kasisi.
Imeandikwa na Florence Focas , Musoma; Geofrey Nyang’oro na Zainab Maeda, Iringa na Lauden Mwambona, Mbeya
No comments:
Post a Comment