Spika wa Bunge, Anne Makinda (aliyekaa) akiwa na Wajumbe wa Tume ya
Utumishi wa Bunge wakati wakikagua Ukumbi wa Bunge, ambao utatumika kwa
ajili ya Bunge la Katiba, mjini Dodoma jana. Picha na Ofisi ya Bunge
Dodoma. Matengenezo
yaliyotarajiwa ndani ya ukumbi wa bunge la Muungano ambao ndio
utakaotumika kwa bunge la Katiba, yamekamilika na sasa ukumbi huo uko
tayari kwa kazi inayotarajia kuanza Februari 18 mwaka huu.
Kukamilika kwa ukumbi huo kunaondoa hofu iliyoanza
kutanda kuwa huenda bunge hilo lingesogezwa mbele kwa siku tatu kwani
kulikuwa na mashaka kwa kazi hiyo.
Jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, William Lukuvi alitembelea ukumbi huo kwa mara ya
mwisho na kujiridhisha katika maeneo muhimu yaliyokuwa yakifanyiwa
marekebisho .
Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ukumbi
huo, Lukuvi alisema tayari viti 676 vimeshafungwa pamoja vipaza sauti
vyake ambavyo Rais Jakaya Kikwete alionyesha mashaka kama vingekamilika
kwa wakati.
Februari Mosi, Rais Kikwete alipita kukagua ukumbi
huo wakati akielekea mkoani Mbeya ambapo alionyesha kutokuridhika hasa
akatilia mashaka katika eneo la vipaza sauti ambako alisema kuwa bado
kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya.
Hata hivyo, jana Lukuvi licha ya kushuhudia kuwa
vimefungwa katika viti vyote, lakini alipotakiwa na waandishi kuwasha
kwa majaribio, wajenzi wa ukumbi walizuia na kusema kitaalamu hakutakiwa
kuwasha jana kwani kazi ilikuwa bado inaendelea.
Alisema kuwa Ofisi ya Bunge imeshatafuta kumbi
nyingine nje ya bunge kwa ajili ya kufanyika mikutano ambayo itahitaji
wajumbe zaidi ya 60.
No comments:
Post a Comment