Pretoria. Wanawake wawili
wanaodai kuwa watoto wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela,
wamejitokeza na kutaka watambuliwe kwenye mirathi ya familia yake.
Kwa mujibu wa mwanasheria anayesimamia mirathi
hiyo, Michael Katz, wanawake hao wanadai kwamba ni watoto wa Mandela na
kwamba wanashangaa kutotajwa katika mirathi yake iliyotangazwa wiki
iliyopita.
Wakili Katz alisema wawakilishi wa wanawake hao,
Onica Mothoa na Mpho Pule, wamewasiliana naye wakitaka utata uliopo sasa
utatuliwe, ili nao waweze kupata haki yao kama watoto wengine wa
marehemu.
Katz alisema, Mothoa na Pule wanadaiwa kuzaliwa na
Mandela wakati akiwa katika ndoa ya mke wake wa kwanza, Evelyn Mase,
aliyeachana naye mwishoni mwa miaka ya 1950.
Taarifa ya kipindi cha televisheni cha Carte
Blanche, iliripoti juzi jioni kwamba tayari wanasheria wawili
wanaowawakilisha wanawake hao, wameshawasiliana na wasimamizi wa
mahakama, kutaka kusitishwa mgawanyo wa mali kama ilivyoelezwa katika
wosia wa mirathi wa Mandela, hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
Naibu Jaji Mkuu, Dikgang Moseneke, aliwaeleza
wanahabari Jumatatu wiki iliyopita kwamba mali za Mandela zinafikia
Randi 46 milioni (sawa na Sh5.6 bilioni).
“Kiasi hicho hakijumuishi mapato yatokanayo na kazi zake nyingine na uwekezaji aliowahi kuufanya,” alieleza.
Wosia wa mgawanyo wa mali zake uliandikwa mwaka 2004 na kurekebishwa kwa mara ya mwisho mwaka 2008.
Mwanasheria Katz, alisema wanawake hao wanataka
kutambuliwa rasmi katika wosia wake na si kwamba wanahitaji kiasi
chochote cha fedha.
Alisema anatarajia kukutana na wasimamizi wa wosia wa Mandela kwa ajili ya kujadili kwa kina kuhusu suala hilo.
Katika kipindi cha Carte Blanche, watu wa karibu
wa Mothoa na Pule walidai kwamba waliwahi kujaribu kuzungumza na Mandela
ili akubali kwamba ni baba halisi wa watoto hao.
Hata hivyo, hakuwahi kujibu au kutoa msimamo wake.
No comments:
Post a Comment