Mwanasheria Mkuu SMZ haujui waraka wa Kificho

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Amir Pandu Kificho akimkaribisha kwenye kiti, Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge hilo, Samuel Sitta baada ya kuapishwa kushika nafasi hiyo, bungeni Dodoma jana.  
Picha na Emmanuel Herman 


Zanzibar. Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Masoud Othman Masoud amesema hajawahi kuuona waraka ulioandikwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) na kusainiwa na Spika Pandu Ameir Kificho unaopendekeza Tanganyika na Zanzibar kuwa na mamlaka huru za dola na kuwasilishwa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akizungumza na Mwananchi AG Masoud amesema waraka huo ulitayarishwa na kamati ya uongozi chini ya Mwenyekiti wa kamati hiyo Spika Kificho, baada ya kufanyika vikao vilivyowahusisha wajumbe wa kamati ya uongozi ya Baraza hilo na kutoa mapendekezo yake.

Masoud alisema licha yeye kuwa si mjumbe wa kamati hiyo lakini huingia kama mjumbe mualikwa, ambapo kikao cha kwanza alishiriki kujadili mambo ya msingi yanayotakiwa kuwasilishwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba kama maoni ya taasisi lakini hakumbuki kuhudhuria kikao cha mwisho ambacho kiliandaa mapendekezo hayo.

“Mpaka sasa waraka uliowasilishwa mbele ya Tume ya Jaji Warioba bado sijauona kwa macho yangu, siwezi kusema kama ulikuwa waraka halali au batili ila nasikia mivutano inayojitokeza miongoni mwa wajumbe wake,” alisema AG Masoud.

Alisema Baraza kama Taasisi lilitoa maoni kama walivyotoa maoni baadhi ya makatibu wakuu wa SMZ na taasisi nyingine ambazo zinaguswa au kufanya kazi zinazohusiana na mambo ya msingi yaliomo katika orodha ya mambo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, alisema kama kamati ya uongozi ya Baraza akidi ya wajumbe ikitimia ina uwezo wa kutoa mapendekezo kwa niaba ya taasisi na kusema si mwafaka kwa sasa kumjadili Spika peke yake, kama kuna ukiukwaji wa sheria au kanuni za Baraza kulikojitokeza.

Pia Mwanasheria Mkuu huyo wa SMZ alibeza kitendo cha Baraza la Wazee wa CCM kuondoa imani kwa Spika Kificho na kumtaka ajiuzulu, badala yake alisema kama kuna makosa yamefanyika, basi kamati nzima ya uongozi ya Baraza hilo inatakiwa ijiuzulu.

“Si haki na sahihi kumshinikiza Spika ajiuzulu, kama kuna kasoro zimefanyika, kamati nzima ya uongozi ya BLW nayo inapaswa kuwajibika. Suala hilo halikuwa la Spika ila ni la taasisi,” alisema Mwanashseria Mkuu huyo wa SMZ.

Alisema kimsingi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haina maoni wala mapendekezo yake kuhusu mabadiliko ya muundo wa Muungano uweje na hata Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, hajawahi kuweka bayana msimamo wake kama kiongozi Mkuu wa Zanzibar.

Hata hivyo AG Masoud alikiri kuwa msimamo pekee ambao Dk Shein amekuwa akiutetea ni ule wa chama chake wa kuendelea kuwapo muundo wa Muungano wa Serikali mbili ambao hautokani na msimamo wa SMZ.

Mwanasheria Mkuu huyo pia alisema ni mapema kwake kutoa tathmini na mwelekeo wa mjadala wa Bunge la Katiba kama Zanzibar itaweza kufikia malengo yake ya kupata katiba yenye masilahi na Zanzibar, kutokana na mgawanyiko uliopo wa wajumbe kutoka Zanzibar uliojitokeza unaoegemea sera za vyama na itikadi za kisiasa.

Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar tayari limetoa tamko la kupoteza imani na Spika Kificho kwa kitendo chake cha kuandika waraka unaopendekeza Zanzibar na Tanganyika zipate mamlaka huru za dola, bila ya kuwepo kwa mapatano na uamuzi wa pamoja wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Wazee hao wamesema hiyo ni aina ya hujuma na usaliti kinyume na utaratibu wa hadhi ya Spika aliyekabidhiwa dhamana hiyo nyeti katika mgawanyo wa madaraka chini ya mihimili mitatu.

Kwa upande wake Spika Kificho amekiri kuwa hakuna uamuzi wa pamoja uliofikiwa na Baraza lake katika kupendekeza aina ya muundo wa mfumo wa Muungano, kutokana na pande mbili za kisiasa za CCM na CUF kila moja kuwa na msimamo wake kisera.

Kificho ameendelea kusisitiza kuwa waraka aliousaini na kuuwasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, ulijadiliwa na kuridhiwa na kamati ya uongozi jambo ambalo limekanushwa na Mnadhimu wa Baraza hilo upande wa CCM, Salmin Awadh Salmin ambaye alisema waliotoa mapendekezo hayo ni kigenge cha watu watano kinyume na utaratibu wa pamoja wa kamati ya uongozi yenye wajumbe 15.

No comments:

Post a Comment