Mtumiaji wa shisha akipata kilevi hicho
Dar es Salaam. Umeibuka ulevi mpya nchini ambao umethibitika kuwateka vijana hasa wa jiji la Dar es Salaam, huku kukiwa na taarifa za kitaalamu kwamba ulevi huo una athari za kiafya kwa watumiaji.
Ulevi huo ni kupitia starehe au anasa mpya ya uvutaji shisha; ulevi ambao watengenezaji hutumia chombo maalumu chenye bomba la kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa tumbaku huwekwa katika chombo hicho na kuunguzwa kwa moto, kisha moshi wa tumbaku hupita kwenye maji na huingia kwenye bomba, kisha watumiaji huanza kuvuta.
Sehemu maarufu ambako shisha inauzwa ni Ufukwe wa Coco, maeneo ya Kinondoni, Mwananyamala, Sinza Barabara ya Shekilango na maeneo kadhaa ya mitaa ya mjini.
Mmoja wa watumiaji wa shisha, Ismail Ndunguru alisema yeye na vijana wenzake hutumia siku za mwisho wa wiki kwenda kuburudika kwa uvutaji katika hoteli moja iliyopo mjini, Mtaa wa Garden jijini Dar es Salaam.
“Kuvuta shisha kwa siku nzima ni Shilingi 10,000, mkimaliza, mnarudisha bomba. Tukiwa vijana wengi inafurahisha sana kuvuta,” alisema Ndunguru.
Taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaeleza kuwa, mkupuo mmoja wa shisha, una kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na maradhi ya mfumo wa upumuaji.
WHO inaeleza kuwa, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 100 au 200.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili na mfumo wa hewa, Meshack Shimwela alisema madhara ya shisha ni kama yale yanayosababishwa na uvutaji wa sigara pengine na zaidi kutokana na kilevi hicho kuwa na tumbaku nyingi.
Dk Shimwela alisema licha ya kuwa watengenezaji na wavutaji wa shisha hudai kuwa haina madhara kwa sababu huchanganywa na maji, lakini bado madhara yake ni makubwa.
“Maradhi yote yanayosababishwa na uvutaji wa sigara ndiyo yanayosababishwa na shisha, kwa mfano saratani ya mapafu na mdomo, kifua kikuu na mzio ambao unaweza kusababisha pumu,” alisema Dk. Shimwela.
Dk. Shimwela alisema ni vizuri watumiaji wakajua madhara ya shisha, badala ya kuchukulia kuwa ni mtindo wa maisha tu au starehe isiyo na madhara.
Hivi karibuni, Profesa Twalib Ngoma, Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alisema asilimia 40 ya saratani zote nchini zinasababishwa na matumizi ya tumbaku.
Biashara inavyofanyika
Shisha inauzwa katika sehemu kadhaa za starehe za Jiji la Dar es Salaam kwa sasa na maeneo yanayouza bidhaa hiyo yanafahamika kama ‘shisha lounge au shisha point’.
Mwandishi wa Mwananchi akiambatana na Ndunguru walikwenda hadi Kinondoni katika hoteli moja ambako wavutaji wa shisha walikuwa wakiendelea ‘kuburudika’ huku wakipuliza moshi hewani.
Waliitozwa Sh15,000 kisha nao waliletewa chombo cha kuvutia. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa bei ya shisha hutegemea sehemu inapouzwa, hivyo huuzwa kati Sh10,000 na 70,000.
Ndunguru alisema shisha haina madhara kwake ingawa alipovuta kwa mara ya kwanza, alikohoa sana lakini sasa anaiona kuwa kiburudisho kinachompa faraja kama wavutaji wa sigara na kwamba hamu ya kuvuta kila mara imeingia mwilini mwake.
Ilibainika kuwa kwenye shisha huwekwa ladha kadhaa kama vile vanila, strawberry, mint, chocolate au kahawa ili kuwavutia wavutaji. Ladha hizo zinatajwa kuwa kivutio cha mabinti ambao wameingia kwa kasi kwenye uvutaji huo.
Kadhalika uchunguzi ulibaini kwamba wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu, kwa makundi hujikusanya na kuchanga fedha kwa ajili ya kuvuta shisha.
Habari zaidi zinadai kuwa wafanyabiashara wa shisha hivi sasa wanachanganya dawa za kulevya kama heroin na bangi katika shisha kama kivutio kwa watumiaji.
“Hii ni biashara kubwa sana sasa hivi, kwa siku moja, mimi naingiza zaidi ya Sh150,000 kwa kuuza bomba la shisha,” anasema mfanyabiashara mmoja wa Kinondoni.
Muuzaji wa shisha katika eneo la Coco Beach, Said Coco alisema biashara hiyo ni nzuri na kwamba wateja wamekuwa wakiongezeka kadiri kila siku.
Coco alisema wateja wake wakubwa ni vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 40 ambao huvuta shisha kila mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, alikanusha habari kwamba wafanyabiashara wanaweka dawa za kulevya na bangi kwenye shisha, ingawa anasema kama wapo wanaofanya hivyo basi wanaharibu starehe hiyo ambayo yeye anasema haina madhara.
Serikali inasemaje?
Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alisema anafahamu kuwa shisha imepata umaarufu nchini hususan Dar es Salaam, lakini ni vigumu kuwakamata watumiaji.
Alisema wizara haiungi mkono matumizi ya shisha kwani inafahamu kuwa ni kilevi hatari pengine kuliko sigara za kawaida na pombe.
“Shisha ni hatari na sisi hatuungi mkono, lakini hatuwezi kuwakamata watumiaji kama ambavyo hatuwezi kuwakamata walevi wa sigara na pombe. Lakini tunawaasa watengenezaji wa shisha kuweka nembo ionyeshayo kuwa ni kilevi hatari,” anasema.
Dk. Rashid alisema matumizi ya tumbaku yanasababisha maradhi mengine hasa saratani ambayo inasababisha kiharusi, maradhi ya moyo na ngozi.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema hana taarifa za ongezeko la matumizi ya shisha nchini, ingawa aliwahi kuona kilevi hicho nchini Misri.
Nzowa alisema ikiwa itagundulika kuwa shisha ina wingi wa Nicotine, atachukua hatua kali dhidi ya wahusika, huku akitoa mfano wa kilevi cha kuber kilichowahi kupigwa marufuku.
Asili ya shisha
Shisha ni jina lenye asili ya Misri (sheesha) lenye maana ya bomba la maji lililounganishwa kwenye kontena.
Tumbaku iliyochanganywa na ladha ya matunda, hujazwa kwenye chombo mfano wa chetezo, moto huwekwa kati na sehemu moja huwekwa maji.
Moshi wenye harufu au ladha hutoka kupitia bomba hilo na kuvutwa.
Mvutaji huvuta kwa kutumia bomba (huweza kuwa la plastiki) na mabomba mengine yanaweza kutumiwa na kutupwa (disposable).
Athari zake kiafya
Kuharibu ogani; Shisha inatajwa kuwa na hewa ya carbon monoxide ambayo huingia kwenye mapafu na kuchukua nafasi ya hewa safi ya oxygen, hivyo ogani muhimu kuharibika.
Saratani; Shisha ina wingi wa nicotine, kiwango cha kemikali za tar, carbon monoxide, metali za kiwango cha juu kama cobalt na lead ambavyo ni visababishi vya saratani.
Utegemezi (adiction); Uvutaji wa shisha husababisha kutengenezwa kwa kiwango kikubwa cha nicotine kwenye damu, hivyo mtu akishazoea kuvuta hawezi kuacha kwani kilichomo kwenye shisha huvutwa kwenye neva za fahamu na kusababisha mishipa hiyo kwenye ubongo kuhisi kupata faraja na raha ya kipekee.
Maradhi ya kuambukiza; Uvutaji wa shisha hutumia bomba ambalo watu kadhaa hushirikiana. Hali hii husababisha maradhi ya kuambukiza kama Kifua Kikuu (TB) na hepatitis B (homa ya ini).
No comments:
Post a Comment