Msanii wa muziki wa Hiphop nchini Rashid Makwiro maarufu ‘Chid Benz’.
Dar es Salaam. Msanii wa muziki
wa Hiphop nchini Rashid Makwiro maarufu ‘Chid Benz’, jana alasiri
alikamatwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius
Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi jana,
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, ACP Hamis Selemani,
alithibitisha kukamatwa kwa Chid Benz na kwamba bado anaendelea
kushikiliwa na polisi.
“Msanii huyu tumemkamata hapa airport akijaribu
kuvuka na dawa za kulevya kinyume cha sheria akielekea jijini Mbeya.
Alikuwa katika hatua za ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege ya Fastjet
kuelekea Mbeya akiwa na wenzake,” alisema.
Akivitaja vitu alivyokamatwa navyo, ACP Selemani
alisema msanii huyu amekutwa na kete 14 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za
kulevya na mpaka sasa bado wanaendelea uchunguzi kubaini ni aina gani za
dawa hizo.
“Mtuhumiwa huyu tumemkamata na kete 14 pamoja na
misokoto miwili ya bangi, ambayo alikuwa ameiweka katika mfuko wa shati
alilokuwa amevaa. Aidha, tumemkuta na kigae kidogo cha chungu pamoja na
kijiko, vitu vya maandalizi ya kutumia dawa hizo na hivi vyote vimekutwa
katika begi lake,” alisema.
Alisema hivi sasa msanii huyo anashikiliwa na
Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi, “Bado tunaendelea kumshikilia na
tutahakikisha sheria inafuatwa kama inavyokuwa kwa watuhumiwa wengine
wanapokamatwa na vitu kama hivi,” alisema kamanda huyo.
Msanii huyo alikuwa anakwenda jijini Mbeya, kwa
ajili ya kushiriki onyesho la ‘Instagram Party’ linalotarajiwa kufanyika
leo jijini humo.
Chidi Benz alikuwa ameongozana na msanii mwenzake
Nurdin Bilal maarufu ‘Shetta’, baada ya kukamatwa na polisi, Shetta
aliendelea na ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege kuelekea Mbeya.
Julai mwaka jana wasanii wawili Melisa Edward na
mwenzake Agnes Gerald ‘Masogange’ walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Oriver Tambo nchini Afrika Kusini, wakiwa na dawa za
kulevya aina ya Crystal Methamphetamine takriban kilo 150, zilizokuwa na
thamani ya Sh6.8 bilioni.
No comments:
Post a Comment