Dar es Salaam. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimetangaza mgawanyo wa majimbo 253 kati ya 265 ya ubunge huku 12 yaliyokuwa kwenye mvutano yakibaki kiporo.
Katika mgawanyo huo uliotangazwa kwa wanahabari jana, Chadema kimepata majimbo 138, sawa na asilimia 73 ya majimbo yote huku CUF ikichukua 99, NCCR – Mageuzi 14 na NLD matatu.
Hiyo ni pamoja na kujumlisha majimbo 51 ya Zanzibar ambayo yote yalikwenda kwa CUF isipokuwa moja lililoachwa kwa Chadema.
Mgawanyo huo ambao umechapishwa katika ukurasa wa 36 wa gazeti hili, umetangazwa wakati mgombea urais wa Ukawa akihutubia mkutano wake wa nne wa kujitambulisha kwa wananchi katika Uwanja wa Demokrasia, Kibandamaiti, Zanzibar; baada ya kufanya hivyo katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Mwanza.
Majimbo hayo yalitangazwa na wawakilishi wa makatibu wakuu wa umoja, John Mnyika (Chadema), Nderakindo Kessy (NCCR – Mageuzi), Shaweji Mketo (CUF) na Masudi Makujunga (NLD) waliokutana katika Ofisi za Makao Makuu ya za NCCR – Mageuzi.
Miongoni mwa majimbo ambayo hayajagawanywa ni, Segerea, Kigamboni, Mbarali, Geita Vijijini, Gairo, Mtwara, Mpwapwa na Geita Mjini, Mwanga na Serengeti ambalo Katibu Mkuu wa NCCR – Mageuzi, Mosena Nyambabe jana alichukua fomu kuliwania.
Taswira ya mgawanyo
Chadema ambacho katika uchaguzi uliopita kilipata majimbo 24 dhidi ya manne ya NCCR-Mageuzi na mawili ya CUF Bara, kimeachiwa majimbo karibu yote katika mikoa ya Mara, Shinyanga, Geita, Njombe, Rukwa, Arusha, Manyara, Singida, Katavi huku Cuf ikibeba mkoa wote wa Lindi na NCCR-Mageuzi ikibeba ngome ya Kigoma.
Katika mgawanyo huo, NLD ambayo haikuwa na jimbo hata moja imeachiwa majimbo matatu tu ya Lulindi, Masasi na Ndanda mkoani Mtwara.
Katika mkutano huo, Kessy alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya majadiliano ya muda mrefu, kuhusu kuachiana majimbo ya ubunge kwa vyama vinavyounda Ukawa.
Mnyika alisema katika uchukuaji wa fomu za Tume ya Uchaguzi, hatatambuliwa mgombea kutoka vyama hivyo, nje ya makubaliano yaliyofikiwa na Ukawa.
Akizungumzia mvutano wa baadhi ya majimbo, mfano Segerea, Mnyika alisema wananchi wanatakiwa kuvuta subira.
Vigezo
Mketo alitaja vigezo sita vilivyotumika katika mgawanyo huo kwa chama husika kuwa ni matokeo ya Uchaguzi wa Serikali Mitaa, matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, kukubalika kwa mgombea, hali ya kisiasa ndani ya jimbo na mtandao wa chama husika.
“Taarifa hii ni rasmi kutoka CUF kwani kila chama kilitoa mapendekezo ya majimbo ndani ya vikao vya Ukawa na yalijadiliwa kupima vigezo hivyo kwa hivyo tunaomba viongozi wote waheshimu uamuzi uliofikiwa,” alisema Mketo.
Agosti 2014, viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Ukawa walisaini makubaliano (MoU) ya kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais wa Muungano na Rais wa Zanzibar.
Lowassa Zanzibar
Wakati huohuo, mgombea urais kupitia Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana alitambulishwa Zanzibar na kusema umefika wakati wa kuikomboa nchi dhidi ya mfumo kandamizi wa CCM.
Alisema jukumu la awali ni kuiondoa CCM madarakani na kutoa nafasi kwa rais kupitia Ukawa ili kuikwamua Tanzania kimaendeleo.
“Mkituchagua mimi na Maalim Seif (mgombea urais wa Zanzibar) mtaiona Tanzania inakwenda kasi ya ajabu, haijawahi kutokea. Hatuwezi kushindwa na Rwanda! Hatuwezi kuachwa na Malawi! Hatuwezi kushindwa na Kenya na Uganda! Tupeni nafasi tuikwamue nchi yetu kutokana na ufukara na umaskini,” alisema.
Kama ilivyokuwa katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Mwanza, Lowassa alionya kuhusu mwenendo aliouita wa hujuma na ubadhirifu wa CCM hasa katika uchaguzi, akisisitiza kuwa hakuna msaada wowote wa kukinusuru chama hicho kikongwe kwa sasa kisiondoke madarakani kwa kuwa muda wake umekwisha.
“Ninawasihi ndugu zangu wale mliobaki CCM njooni haraka muungane nasi kuikomboa nchi hii, wakati ni huu, hakuna namna ya kuzuia wimbi hili la umma katika safari hii ambayo inaelekea katika ushindi wa kihistoria na mwisho wa utawala wa CCM,” aliongeza.
Lowassa aliweka msisitizo juu ya azma ya kusimamia kikamilifu mapendekezo ya Katiba kwa mujibu wa maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
“Hatuhitaji kusimama na batili ambayo haikuwa chaguo wala mapendekezo ya wananchi walio wengi, tutalinda masilahi ya Zanzibar katika Muungano kama nchi kamili yenye heshima yake,” alisema Lowassa.
Alisema iwapo atachaguliwa, Serikali yake itahakikisha haki za masheikh waliopo kizuizini zinapatikana haraka iwezekanavyo.
Mgombea mwenza, Juma Duni Haji alisema upepo mkali wa mabadiliko na nguvu isiyozuilika ya Ukawa dhidi ya CCM ni ujumbe tosha kwamba mwisho wa chama hicho umewadia.
“Someni yaliyojiri Urusi, Ukraine, Misri na kila pembe ya mabadiliko duniani, muangalie ni wapi dola iliposhinda nguvu za umma,” alihoji Duni ambaye hivi karibuni alijivua uanachama wa CUF, alikokuwa Makamu Mwenyekiti na pia kujiuzulu uwaziri katika Baraza la Mawaziri Zanzibar.
Maalim Seif
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alimtahadharisha Rais Jakaya Kikwete juu ya matumizi mabaya ya vyombo vya dola.
“Ndugu yangu, rafiki yangu kipenzi, Rais Kikwete nakuomba umechukua nchi kwa amani ondoka kwa amani,” alisema huku akilaumu tabia ya watu aliowaita “Janjaweed”, waliodaiwa kumpora Abdi Seif Hamad fomu ya kugombea Ubunge kupitia CUF katika Jimbo la Shaurimoyo jana.
Abdi ni miongoni mwa watu waliohama CCM siku za karibuni na kujiunga CUF kwa matarajio ya kuungwa mkono na Ukawa.
Mamia ya mashabiki jamii wa Kimasai walimiminika katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume kumlaki Lowassa na katika hali ambayo haikuzoeleka, walionekana kupiga saluti wakiwa wamejipanga barabarani wakati msafara wa viongozi wa Ukawa ukipita Barabara ya Kiembe Samaki, Mwanakwerekwe kuelekea Kibandamaiti.
Wamasai hao walimiminika kwa wingi uwanjani hapo na kupata fursa ya kuburudisha umati wa watu kwa wimbo wa Kimasai wenye maana ya ‘tunampenda Lowassa’.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema safari ya Ukawa ni ndefu, imepitia majaribu mengi lakini bado umoja huo uko imara hivyo wananchi hawana budi kujitokeza kwa wingi kuunga mkono umoja huo kuelekea ukombozi wa pili wa Tanzania.
“Ndugu zangu tumetoka mbali tutasimama imara kuhakikisha safari yetu inafikia tunakohitaji katika mafanikio na ushindi na hatimaye kushika uongozi wa nchi,” alisema.
James Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR, Mageuzi, James Mbatia alisema: “Tumeshawaagiza mawakili wetu kurekodi kila tukio kila udhalimu na kila uonevu, tunamuomba Bensouda (Fatou, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa) kufutilia namna zote za uvunjaji wa haki na ifikapo Novemba tunampeleka yeyote ICC.”
Khamis Mgeja
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja aliwahamasisha Wana-CCM kujiunga na Ukawa na kumpigia kura Lowassa, wakielewa kwamba hatima ya chama hicho kikongwe imewadia.
Wengine wachukua fomu za uraisi
Wakati mkutano wa Ukawa ukiendelea, wagombea wengine wa urais Zanzibar walijitokeza jana katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.
Waliojitokeza ni Juma Ali Khatib wa Tadea na Said Soud Said wa Chama cha Wakulima (AFP). Khatib ni Katibu Mkuu wa Tadea na Soud ni mwenyekiti wa AFP.
Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Borrice Bwire (Dar) na Hussein Ali (Zanzibar).
No comments:
Post a Comment