Wakimbizi wa Burundi nchini TZ warejeshwa makwao



Ramani ya Burundi

Serikali ya Tanzania imeanza rasmi hatua za kuwarejesha makwao raia wa Burundi waliovuliwa hadhi ya ukimbizi.

Ni katika hatua za kuifunga rasmi kambi ya Mtabila ambayo ni kambi pekee iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi nchini humo wapatao elfu thelathini na saba.

Sanjari na uamuzi wa kuwarejesha makwao raia hao, shughuli hii inaambatana na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote ambao hawako tayari kurejea Burundi.

Shughuli ya kuwarejesha makwao kwa hiyari raia wa Burundi waliokuwa wakimbizi hadi mwezi Agosti mwaka huu kabla ya kuvuliwa hadhi ya ukimbizi na serikali ya Tanzania,ilimalizika rasmi Jumatatu ambapo kuanzia leo kinachofuata dhidi ya wakimbizi hao ni kuandikishwa kwa kufuatwa kwenye maeneo wanakoishi kambini na kisha kupakiwa kwenye magari na kurejeshwa Burundi.

Akizungumza na mwandishi wa BBC mjini Dar es Salam Eric David Nampesya, mkuu wa kambi hiyo ambaye ni mwakilishi wa wizara ya Mambo ya ndani nchini humo, Bwana Frederick Nisajile, alisema utaratibu huo utakavyokuwa baada ya kukamilika kwa shughuli ya kurejea kwa hiyari ya 'Kimombo Voluntary repatriarition.'

Bwana Nisajile alisema inatarajiwa kuwa raia wa Burundi wapatao elfu moja watarejeshwa makwao kila siku katika utaratibu huu ambao pia utawahusisha maafisa wa idara ya Uhamiaji ili kuwakamata wale wote watakaokaidi kurejea makwao.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi UNHCR Bi Chansa Kapaya anasema hakuna uwezekano kwa Raia hao wa Burundi kutafutiwa nchi ya tatu kwa sababu wao si wakimbizi tena kwa wakati huu.

Nafasi hiyo haipo tena,nafasi kama hiyo hutolewa kwa wakimbizi,hawa walipokuwa wakimbizi zamani na kwa sasa walishavuliwa hadhi ya kuwa wakimbizi,kwa maana hiyo hawawezi kupewa nafasi ya kutafutiwa hifadhi katika nchi ya tatu,kwa maana hiyo suluhisho pekee kwao ni kurejea Burundi.

Kuanza kufungwa kwa Kambi hiyo ya Mtabila kunahitimisha miaka 19 tangu ilipofunguliwa mnamo mwaka 1993,wakati huo ilipoanza kupokea raia wa Burundi waliokimbia machafuko ya kivita yaliyofuatia mauaji ya aliyekuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Burundi hayati Melchior Ndadaye.

No comments:

Post a Comment