Alawitiwa na kuambukizwa virusi vya ukimwi Polisi naye adaiwa kumbaka akiwa kituoni
Nyumba inayoonekana ni ghorofa inayodaiwa kutumiwa kama danguro iliyopo Mwananyamala Magengeni jijini Dar es Salaam
Msichana yatima, mkazi wa mkoani Manyara, amefungiwa
kwenye danguro kwa zaidi ya miaka 10 akinyanyaswa kingono, kuteswa na
kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Msichana huyo aliyeondolewa nyumbani kwao Oysterbay mjini Babat,i
alilaghaiwa na mwanamke aliyejifanya kuwa msamaria mwema, akitangaza
nia ya kumsaidia kielimu na kimaisha, kufuatia kifo cha mama yake mzazi.
Msichana aliyefikwa na masahibu hayo ni Sara Tarimo (27) ambaye
aliangukia mikononi mwa mwanamke mwenye danguro hilo, Abia Lucas (44)
anayeishi Mwananyamala Magengeni.
Ilikuwa ni baada ya kifo cha mama yake Magreth Kitinati, aliyekuwa akiishi naye Oysterbay huko Manyara.
Sara anasema mwanamke huyo alimtoa kijijini kwao hadi jijini Dar es
Salaam, na kumshinikiza kwenye `utumwa wa ngono’ kwa kipindi cha miaka
10 akiwa amefungiwa ndani.
Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, mama yake mzazi alifariki, hivyo
ujio wa msamaria huyo ulikuwa faraja na tumaini jipya kwa maisha yake.
Haikuwa hivyo.
Sara alisema alipoteza bikra yake baada ya kumlazimisha kufanya ngono
na mwanamume mtu mzima, aliyembaka na ukawa mwanzo wa kutumiwa kingoni
na wanaume wa kila aina.
Sara alisema alifanywa unyanyasaji huo akiwa na miaka 13 na kwamba hilo lilikuwa tukio lake la kwanza kukutana na mwanaume.
Baada ya kufanikiwa kutoroka na kuwataarifu polisi nyendo za mama huyo
ambaye sasa anashikiliwa kwa mahojiano, Sara anasimulia kumbukumbu za
kusikitisha za miaka aliyoipoteza katika himaya ya danguro la
‘msamaria.’
HISTORIA YAKE
Sara ni mmoja wa watoto watatu katika familia yao. Kaka yake Emmanuel Tarimo (31) na dada yake Neema Tarimo.
Wakati akipochukuliwa na ‘msamaria’ alimuacha kaka yake huko Babati
akijitafutia riziki kwa kubeba mizigo na dada yake akiendelea na masomo
ya shule ya msingi.
Anasikitika kuwa katika maisha yake hakubahatika kumfahamu baba yake,
lakini aliwahi kuelezwa na mama yake kuwa ni mwenyeji wa Kilimanjaro.
Mama yake ndiye aliyekuwa anatunza familia yao licha ya kwamba hakuwa na ajira rasmi, wala biashara za kudumu.
Mazingira hayo, yalimlazimisha kukatisha masomo akiwa darasa la tatu katika shule ya Msingi Idangunyii.
Anasema alikuwa na ndoto ya kupata elimu zaidi, lakini kifo cha mama yake kilisababisha ajione kuwa hana bahati.
MAISHA KWENYE DANGURO
Alisimulia kuwa, baada ya ‘msamaria ‘ kujitokeza na kumwahidi kuwa
atamtafutia shule na kugharamia elimu alimsikiliza na kumfuata hadi
jijini Dar es Salaam.
Sara alieleza kuwa mwanamke huyo alipofika nyumbani kwao Babat, alieleza
kuwa anatafuta wasichana 10 kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwa
familia za Dar es Salaam.
“Aliiambia familia yangu kuwa, hata kama wasichana watakaopatikana
watakuwa wanasoma wataendelezwa mara baada ya kufika mjini wakati
wakiendelea na kazi ,’’ anasema na kuongeza:
“Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa mwaka 2003, tuliondoka kwa usafiri wa
basi tukiwa 10 ingawa sikuwatambua wenzangu kwa sababu alituchukua
kutoka katika vijiji tofauti.”
Alisimulia kuwa walifika nyumbani kwa mwanamke huyo Mwananyamala
Magengeni kwenye ghorofa mbili, ambayo juu linaonyesha ujenzi
unaendelea.
Alisema wakiwa nyumbani kwa mama huyo, walibadilishwa mavazi kutoka yale
waliyotoka nayo kijijini na kupewa nguo nyingine- sketi fupi, kaptula
na blauzi maarufu kama ‘vitop’.
Alikumbuka kuwa baada ya kupewa nguo hizo, walitakiwa kila mmoja
akajipumzishe kwenye chumba chake vilivyokuwa ghorofa ya kwanza.
KUBAKWA MARA YA KWANZA
Alieleza kuwa siku hiyo akiwa chumbani kwake mlango uligongwa na alipouliza ni nani, alijibiwa na sauti ya kiume kuwa ni mlinzi.
Alipofungua, mwanaume mtu mzima alimwambia wakati huo sio wa kulala
bali ni wa kazi na kumtaka avue nguo huku akimtisha na bisibisi.
Vitisho vilitawala akilazimishwa kufanya ngono kwa nguvu na mwanaume
huyo aliyetumia bisibisi kumchoma mdomoni na mkononi karibu na
kiwiko.
“Nilipiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna aliyekuja kunisaidia
hadi yule mzee alipomaliza haja yake na kuniacha nikiwa kwenye maumivu
makali.”
Anasema hakuamini kilichotokea na kulalamika kwa mwenyeji
wake….“Nilimfuata yule mama kumweleza yaliyonitokea cha ajabu aliniambia
hiyo ndiyo kazi niliyofuata mjini.”
Anasema “baada ya kupewa maneno hayo makali nilipelekwa kwa daktari wa hospitali ya Mwananyamala kwa uchunguzi zaidi.”
Anasema aliendelea kuwa mtumwa wa ngono kwa sababu baada ya matibabu akawa anaendelea na kazi hiyo.
Sara anasema katika hospitali hiyo ndiko walikokuwa wanatibiwa na mwanamke huyo alimweleza kuwa huyo ni daktari wao.
Anasema aliwahi kudhalilishwa kingono na wanaume zaidi ya 10 kwa siku moja, wakiwa wa rika, tabia na maumbile tofauti.
“Nakumbuka siku moja alikuja mteja aliyekuwa amelewa, akaniambia
amelipa fedha nyingi kwa mama na anachotaka ni kunitumia kinyume cha
maumbile.”
“Sijawahi kufanya hivyo, nilipokataa alitoa kisu na
kunitishia…alinilazimisha nivue nguo na kulala kitandani kabla
hajanijeruhi.” Anasema.
“Nikiwa kitandani alidondosha kisu tumboni mwangu, akakilalia na
kunijeruhi, nikakimbizwa Mwananyamala na kutibiwa na yule daktari wa
mwanzo niliyeambiwa ni tabibu wetu ambaye alinishona sehemu
nilizojeruhiwa na alikuja nyumbani kunitoa nyuzi,” anasema
MALIPO
Sara anasema hakuwahi kulipwa japo wakati wakiendelea na kazi hiyo,
mwanamke huyo aliwaeleza kuwa malipo yao ni Sh. 30,000 kwa mwezi na
kwamba wangelipwa baada ya kukamilisha alichokitaka.
Akielezea faida waliyomtengenezea mama huyo alisema alikuwa akitoza kati
ya Sh. 10,000 hadi 15,000 kwa wateja waliofanya ngono kwa njia ya
kawaida na wale waliokuwa wakiwaingilia kinyume cha maumbile ilikuwa
aliwalipisha kati ya Sh. 30,000 na 50,000.
Anaeleza kuwa walikuwa wakipatiwa matibabu, chakula na kununuliwa mavazi lakini hawakuruhusiwa kutoka nje ya nyumba hiyo.
“Niliwahi kumhoji mama kwa nini alitudanganya unatuleta mjini kwa ajili ya kufanya kazi za ndani na kutusomesha?”
“ Nilimuomba anirudishe nyumbani, lakini alikataa na kuniambia kazi yake
itakapokwisha nitarudi sikuyaelewa majibu haya,” anasema. ALIVYOTOROKA
Alisema baada ya kutumikishwa kwa muongo mmoja, Februari 4, 2013,
siku aliyofanikiwa kutoroka baada ya mwanaume aliyefanya naye mapenzi
siku ya kwanza kufika kwenye danguro hilo akihitaji huduma yake.
“Alilipia na kuja chumbani kwangu na kunieleza kuwa lile embe
lililokula kipindi kile lilikuwa bichi, hivyo amekuja kwa mara
nyingine likiwa limeiva na baada ya kumaliza haja zake.”
“Aliniambia anataka kunipa zawadi hivyo niliporuhusiwa na mama
tuliondoka naye, tukipita maeneo tofauti akinielekeza majina ya mitaa na
mwishowe tuliingia sokoni Kariakoo,” anasimulia.
Waliondoka na gari aina ya Volkswagen hadi Kariakoo na wakati huo
alihisi njaa na kumuomba kabla ya kumnunulia zawadi, wanunue kwanza
chakula.
Mteja huyo katika mazungumzo yake alimfahamisha kuwa ni mwanasheria anayefanya kazi manispaa japo hakutaja jina.
“Tukiwa njiani alikokuwa amekusudia kunipeleka nilikuwa nikitembea nyuma
yake, hapo ndipo nilipotoroka nikikimbia bila kujua ninaelekea wapi,
nilizunguka na hatimaye giza liliingia na watu walipungua kwenye eneo
nililokuwapo.”
“Sijui ilikuwa saa ngapi, lakini niliona gari la polisi niliamua kuwafuata nikamueleza askari wa kike mkasa mzima,” alisema.
Anasema walikwenda kituo kikuu cha polisi na kuchukuliwa maelezo lakini
pia alimpatia nguo nyingine kwa vile alikuwa amevaa mavazi yasiyo na
staha.
“Siku iliyofuata niliambiwa kuna dawati la kushughulikia masuala ya
wanawake, lakini kwa wakati huo wahusika hawakupo. Ilipofika Alhamisi
nilikabidhiwa kwa askari mwingine anaitwa Happy.”
Aliongeza: “tuliondoka naye hadi Oysterbay polisi, huko walitoka askari kadhaa kwenda Mwananyamala nyumbani kwa mama huyo.”
Sara alisema walifanya upekuzi kwenye vyumba walivyokuwa wakilala bila
mafanikio, walishuka chini na kumuamuru afungue moja ya vyumba
vilivyokuwa vimefungwa lakini mwanamke huyo alikataa na polisi
walimuagiza aende kituoni kuandika maelezo dhidi ya tuhuma hizo.
Alieleza kuwa wakati mtuhumiwa huyo akiwa mahabusu watoto wake anaoishi
nao mmoja mwanaume mwenye miaka 27 na mwingine wa kike walimsihi afute
kesi hiyo, lakini alikataa na kuongeza kwa alifungua jalada la uchunguzi
lenye kumbukumbu RB/2468/2013 la Februari 7.
VYOMBO VYA HABARI
Alisema amefikisha suala hili kwenye vyombo vya habari akiomba msaada wa nauli ili aweze kurudi kwao pamoja na chakula.
“Kabla sijafika NIPASHE nilitoa taarifa kwenye Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu ambacho kimeahidi kulifanyia kazi suala langu,” anasema.
AFYA YAKE
Sara analalamikia kuwa na vivimbe mbavuni na sehemu za siri na anahofu kuwa huenda ameambukizwa magonjwa ya ngono na Ukimwi.
Anasema ana wasiwasi kwa vile aliwahi kupata vipele vingi mwilini
japo daktari wao alimueleza kuwa vilisababishwa na joto lakini sasa
vimekuwa uvimbe mkubwa.
Anasema wakiwa kwenye danguro hilo daktari wao alikuwa anawapa dawa mara
kwa mara ambazo hawafahamu zilikusudiwa kutibu nini na zilipomalizika
aliendelea kuzileta japo hakuwahi kutumia tiba hiyo.
KONDOMU
Anasema baadhi ya wanaume wenye ndoa walitumia kondomu wakati wa
kufanya ngono lakini asilimia kubwa ya wateja wa danguro hilo walikuwa
hawatumii mipira hiyo ya kiume.
“Walikuwa wananiambia nina mke ninampenda hivyo natumia kondomu lakini
wengine walikuwa hawatumii, chumbani tulikuwa tunawekewa kondomu lakini
ukiwaambia wazitumie wanakataa.”
KUGUNDULIKA NA VVU
Sara anasema Jumatatu Februari 11, akiwa polisi Oysterbay, aliamriwa
kuondoka eneo hilo kwani si sehemu ya kuishi nail kufungua mashtaka.
“Nilikwenda kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo lakini usiku nilizidiwa
ilipofika asubuhi nilikwenda zahanati ya Mwenge nilikotibiwa na
kuelezwa kuwa nimeambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kutakiwa kuanza
kutumia dawa.”
KULAWITIWA NA POLISI
Wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Abia ukiendelea, inadaiwa kuwa
usiku wa Jumatano polisi wa kituo cha Oysterbay alimlawiti Sara eneo
lenye migomba kituoni hapo.
Akizungumza na NIPASHE kwenye kituo cha trafiki kilichopo kituo cha
mabasi ya mikoani Ubungo, alisema alifanyiwa unyama huo baada ya
polisi kumfuata akiwa amelala kwenye maegesho ya magari.
Anasema alikwenda Ubungo kuchukua nguo alizozificha hapo na akiwa huko
alikutana na askari huyo ambaye alimueleza matatizo yake, ndipo
akamtaka wakale chakula.
“Baada ya chakula wakati tunarudi kituoni, aliniambia nimlipe kwa
kumruhusu kunifanyia tendo hilo lakini nilikataa na askari huyo
alinishika kwa nguvu na kunilawiti.”
Anaongeza kuwa kutokana na kitendo hicho aliondoka kituoni hapo saa
12:00 asubuhi na kufikisha taarifa ITV kwa vile aliona polisi hawakuwa
na msaada kwake.
Baada ya kutoa malalamiko yake na kusaidiwa na wafanyakazi wa ITV
alijitokeza polisi mwanamke na kumchukua kwa matibabu kwenye zahanati
ambayo Sara alisema haifahamu na baadaye kupelekwa kituo cha mabasi
Ubungo ili kurudishwa nyumbani kwao Manyara.
Alimweleza Mwandishi Wetu kuwa aliomba simu kutoka mtu aliyekuwa kituoni
hapo ili awasiliane naye kabla hajasafirishwa na polisi hao.
Baada ya mwandishi kufika Ubungo na kufanya mahojiano na Sara gari la
polisi lenye namba PT 2083 lilifika na kumpeleka polisi Oysterbay
na kuandikisha maelezo. MAELEZO YA POLISI
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, John Mtalimbo,
alipofuatwa alisema taarifa zipo kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya Kinondoni
(OCD).
Aidha, alisema kwa mujibu wa OCD msichana huyo amekuwa akitangatanga maeneo ya Buguruni na sehemu nyingine ambazo hakuzitaja.
“Naona lengo lake ni kutuchafua, kwa nini asubuhi alikuja ITV na sio
kutoa taarifa kwetu kama amelawitiwa na askari wetu, anatuchafua,”
alisisitiza Kamanda Mtalimbo.
Alikiri kuwa siku mbili zilizopita polisi ilimtafutia tiketi ili kumrudisha kwao lakini haikufanikiwa.
Kamanda alipoulizwa sababu za kumsafirisha Sara wakati amefungua kesi ya
kuuzwa kimwili kwenye danguro alisema ni kutokana na kukosa makazi.
Awali, Mwandishi Wetu alinasa mawasiliano ya simu ya Kamanda Mtalimbo na
mtu aliyeelezwa kuwa ni OCD akimwelekeza jinsi yakuandika maelezo
dhidi ya binti huyo.
Alisikika akisema: “Inabidi tujipange, hapa watakuja waandishi wa
habari, (bila kujua kama mwandishi wetu alikuwepo eneo hilo), watataka
kujua kinachoendelea na kumshauri andike kuwa walikubaliana kufanya
ngono.”
Licha ya kusikia kilichozungumzwa juu ya mlalamikaji huyo alipoingia
ofisi kwake na kujitambulisha na kuuliza habari za Sara Mtalimbo
alimweleza kuwa hana taarifa hizo na kwamba anasubiri zitoke kwa OCD.
Akisoma maelezo ya OCD wa Kinondoni, Mtalimbo alisema Februari 2, mwaka
huu Sara aliripoti kituo hapo kuwa alikuwa akiishi Mwananyamala
alikokuwa akifanyishwa kazi za kuuza mwili na mtuhumiwa aliyemtaja kwa
jina la Abia.
Alisema baada ya polisi kupokea malalamiko hayo walikwenda
Mwananyamala kuonyeshwa danguro hilo na polisi walipomkamata Abia
mlalamikaji alishindwa kumtambua na kuongeza kuwa walifungua jalada la
uchunguzi na kwa sasa mtuhumiwa yuko nje kwa dhamana na Sara aliendelea
kubaki kituoni hapo hadi alipoonekana ITV jana asubuhi.
Kamanda alielezwa kuwa katika mahojiano ya Sara na OCD alimfahamisha
kuwa Jumatano wiki hii akiwa Ubungo alitongozwa na askari aliyemuahidi
kumpatia Sh. 10,000 baada ya kumlawiti.
“Walikwenda kwa makubaliano migombani na baada ya kufanya kitendo
hicho, askari alimpa Sh. 20,000 ,” alisema na kuhoji sababu za msichana
huyo kutofikisha tukio hilo kituoni badala yake alikimbilia ITV.
Hata hivyo alipoulizwa iwapo mlalamikaji amemtambua askari huyo kupitia
gwaride la utambuzi na iwapo alichukuliwa hatua alisema bado na
kuongeza:”Maelezo niliyokupa ndiyo mambo mengine yatafuata baadaye.” NYUMBANI KWA ABIA
Gazeti hili likafika nyumbani kwa Abia na kukutana na binti
alijitambulisha kuwa anafanyakazi za ndani na kueleza kuwa mwenye
nyumba hakuwepo na hajui alikokwenda.
Alipoulizwa kuhusu danguro binti huyo mwenye miaka kati ya 13 na 20
alisema hafahamu kinachoendelea kwani mwajiri wake anamkataza kutoka nje
kukutana na majirani lakini akadokeza kuwa Jumatatu wiki hii walikuja
polisi wakamkamata mama huyo ambaye siku iliyofuata alirudi nyumbani.
KUWEPO MADANGURO
Majirani wa mtuhumiwa walikataa kutoa ushirikiano kwa kuhofia
wanazungumza na polisi lakini Mwenyekiti Serikali ya Mtaa Kata ya
Makumbusho, Said Muhunzi, alisema uchunguzi uliofanyika umebaini kuwepo
kwa danguro hilo.
“Nimebaini wapo wasichana wenye umri mdogo ambao wanaonekana na
majirani wakiingizwa hapo kila mara na baadhi ya watu, majirani
wamethibitisha hili,” alisema.
Aliongeza kuwa, Jumatano iliyopita kikundi chake cha ulinzi shirikishi,
kilifika kwenye nyumba hiyo saa 7:00 usiku na kumkuta mtuhumiwa Abia
na watu wengine wakiwa nje na kuwataka waingie ndani kwa kwani
haukuwa muda wa kukaa nje.
“Ijumaa iliyopita niliwaambia walinzi waende tena saa 8:00 usiku
kuangalia kama watawakuta nje, waliona watu watano wakinywa pombe nje,”
alisema na kuongeza:
Aliongeza kuwa watu hao ni Abia, Salome, mtoto wa marehemu mumewe na
wanaume watatu na kuongeza kuwa kijana mmoja anayeitwa Juma alifahamika
baada ya wenzake kumtaja kutokana na kuwatishia walinzi hao kwa bastola.
Muhunzi alisema Salome anatumiwa na Abia kutafuta mabinti kwa ajili ya
danguro hilo na kwamba kufuatia tukio hilo la walinzi kutishiwa
walifungua kesi tatu katika kituo cha polisi Minazini alizozitaja kuwa
ni kukutwa nje wakinywa pombe usiku,kutishia kuua na kuzuia ulinzi
usifanyike
Alisema walifungua jalada lenye kumbukumbua RB/118/2013 na kesi hiyo
ilifikishwa kituo cha polisi Oysterbay na kukuabidhiwa kwa mpelelezi
aliyemtaja kwa jina moja la Mwesiga
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo, alisema eneo lake moja ya
changamoto zilizopo ni kuibuka kwa madanguro na baadhi ya wasichana
wenye umri mdogo kujiuza kwenye baa nyakati za usiku.
Alitaja baadhi ya baa (majina tunayo ) kuwa zinaongoza kwa kuwa na
wasichana wengi wanaojiuza na kwamba wanatoa elimu kupitia kamati ya
Ukimwi na kufanya msako lakini tatizo ni kubwa.
Alitaja danguro maarufu liitwalo ‘kwa wahaya’ lililopo Minazini na kusema kuwa ofisi yake inawajua watuhumiwa kwa majina.
Habari zilizozifikia gazeti hili jana asubuhi, Sara alikuwa amewekwa mahabusu kituoni hapo.
No comments:
Post a Comment