Mauaji ya Padri

Akina mama wakilia baada ya kifo cha ghafla cha Padri Evarist Mushi kilichotokea jana asubuhi kwa kupigwa risasi muda mfupi kabla ya kuanza misa ya Jumapili kwenye Kanisa Katoliki la Kigango cha Mtoni, Zanzibar.


PADRI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Minara Miwili lililoko Mji Mkongwe Zanzibar, Evaristus Mushi ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana jana asubuhi wakati akielekea kanisani kuendesha ibada.

Tukio hilo limetokea majira ya saa moja asubuhi wakati padri huyo akijitayarisha kwenda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtoni nje kidogo na Mji wa Zanzibar.

Hilo ni tukio la pili kutokea kwa padri kupigwa risasi Zanzibar baada ya Desemba 26, mwaka jana Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki, Mjini Zanzibar kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake saa 1:45 jioni wakati akitokea kanisani.

Akizungumzia tukio la jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema pamoja na kuthibitisha, alisema ametuma timu ya wapelelezi kwenda Zanzibar kuchunguza kwa undani kuhusu tukio hilo.

“Watu wasiojulikana wamempiga risasi Padri Mushi, na baada ya tukio alipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja na kufariki dunia. Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo,” alisema IGP Mwema.

Alisema hadi sasa watu watatu wameshakamatwa kuhusiana na tukio hilo na msako mkali unaendelea na kuchunguza tukio zima.

IGP Mwema alisema ametuma timu Zanzibar itakayoongozwa na Manaibu Kamishna wa Polisi wawili ambao ni Samson Kasalla na Peter Kivuyo wakiwa pamoja na Kamanda wa Operesheni wa jeshi hilo, Simon Sirro.

“Tumekuwa tukifuatilia nyendo hizi na hivi sasa tutapambana na wahalifu ipasavyo, vurugu zozote zile lazima tupambane nazo ipasavyo,” alisema Mwema na kuongeza: “Kama kwenye tukio hili kutakuwa na masuala ya kigaidi nayo tutachunguza.”
Alisema watawatafuta kwa udi na uvumba wale wote wanaochochea au kufadhili yanayotokea kwa kuwa wanachokifanya ni uhalifu.
Mwili wa padri huyo sasa umehifadhiwa katika mochwari ya Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Katika Kanisa la Minara Miwili, Mji Mkongwe waumini walikusanyika wakionyesha hali ya kuchanganyikiwa baada ya kupata taarifa za kifo hicho cha ghafla.
 Wakizungumza kwa masikitiko waumini hao wamesema hawakuwa wakijua chochote kilichotokea hadi hapo walipofika katika kanisa kwa ajili ya kufanya ibada.
 “Tumetoka nyumbani tukiwa na matumaini makubwa ya kufanya ibada zetu kwa amani, lakini tulipofika hapa tumepokea taarifa kuwa padri wetu amepigwa risasi, jamani Mungu hiki ni nini, mbona Zanzibar imegeuka kuwa nchi isiyo na amani, vipi tutaishi katika hali kama hii ya kuhofu na wasiwasi...Mungu tusaidie waja wako sisi,” alisema mama mmoja huku akilia kwa majonzi.”
Mashuhuda
Walioshuhudia tukio hilo wanasema kawaida Padri Mushi huwa anakwenda kusalisha katika Kanisa la Mtoni na kwamba jana, baada ya kufika kanisani hapo wakati akitaka kuegesha gari lake walifika watu kwenye gari lake na kumfyatulia risasi na kisha kukimbia kusikojulikana.
Makamu Askofu wa kanisa hilo Zanzibar, John Mfoi alisema kuwa watu waliompiga risasi Padri Mushi walikuwa wapo kwenye pikipiki aina ya Vespa na walikuwa wakimfuatilia kwa nyuma wakati akieleke kanisani.
“Baada ya kufika karibu na kanisa alipigwa risasi na gari kupoteza mwelekeo kisha kwenda kuonga nyumba,”alisema na kuongeza: “Uchunguzi wa hospitali umegundua alipigwa risasi tatu mbili zimetolewa kichwani na nyingine haijulikani iliko.”
Matukio kama hayo ya kihalifu yamekuwa yakitokea mara kwa mara Zanzibar ambapo katika kipindi cha mwezi mmoja watu watatu walipigwa risasi maeneo ya Bububu na Mbweni, lakini hii ni mara ya pili kwa padri kupigwa risasi katika historia ya Zanzibar.

TEC wasikitika
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Severin Niwemugizi alisema tukio hilo linatia mashaka kwa kuwa mauaji hayo yanaonyesha kuwa ni ya kupanga.
“Nimepata taarifa kwamba kuna mwenzetu ameuawa huko, lakini inaonekana ni mauaji ya kupangwa kwa kadiri ya hamasa ambazo zinatolewa na dini fulani, kwani waliwahi kusema hatutaifurahia Pasaka, nadhani ndiyo wanatekeleza hilo,” alisema Niwemugizi.

Alisema tukio hilo ni la kuogopesha na linaonyesha nchi inakoelekea si kuzuri kwa kuwa kikundi fulani kimeachiwa na kinafanya mauaji na kuwatendea maovu wengine lakini viongozi wamekaa kimya.

“Hii ni ishara mbaya kwani Serikali ipo hivyo tunahitaji kauli yao kuhusu haya mambo, kwa kweli nina mashaka na yanayotokea ili yasije yakatufikisha kwenye mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda,”alisema Niwemugizi.

JK atuma rambirambi
Rais Jakaya Kikwete alisema amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Mushi.

“Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.”

 

Alisema pia ameagiza polisi washirikiane na vyombo vingine vya usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.”

Dk Nchimbi asema ni ugaidi
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema kuwa mauaji hayo ni ya kigaidi  hivyo Serikali itachukua hatua kali kuhakikisha waliohusika wanakamatwa.
“Tutahakikisha kuwa Serikali inawakamata waliohusika na kuwatia mbaroni,”alisema Dk Nchimbi.

Mwinyi aonya
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi amewaonya viongozi wa dini kuhusiana na matukio ya vurugu yanayoendelea kujitokeza nchini akisema kuwa Tanzania ni sawa na gunia lililokusanya mchanyanyiko wa watu wenye kufuata mikondo ya dini inayotofautiana. Hivyo hakuna dini inayoweza kujigamba ni bora zaidi ya nyingine.

Aliwataka viongozi wa dini kuwakemea waumini wanaojihusisha na mienendo korofi kwa kuwa bila kufanya hivyo taifa linaweza kutumbukia kwenye mgogoro wa kidini na kusababisha upotevu wa hali ya amani na mshikamano.

Rais mstaafu Mwinyi ambaye alikuwa akizungumza kwenye sherehe za Maulidi iliyoadhimishwa jana na waumini wa Madhehebu ya Shia, alisema kuwa Tanzania iko kwenye wakati mgumu ikiandamwa na misukosuko ya aina mbalimbali ikiwemo ile yenye sura za kidini na kisiasa.
Alisema kuwa Tanzania iliyosifikia duniani kwa ustaarabu wake wa amani na mshikamano sasa inaanza kupoteza mwelekeo kwa raia wake kuingia kwenye maisha ya hofu na kushindwa kuaminiana.

“Ngoja niwapeni mfano mmoja hata kama mfano huu utakuwa mbaya kwenu, lakini nataka muelewe maana yangu… Tanzania ni sawa na gunia lililokusanya watu wa aina mbalimbali, wapo wale wenye dini, kuna wale hawana dini na wapo ambao wana dini inayotofautiana na dini nyingine...Hakuna upande unaoweza kujivuna kuwa ni bora kushinda mwenzake,” alisema na kuongeza;

“Ni wajibu wote tuliomo ndani ya gunia hili kushikamana na kuvumiliana kwani tukisema huyu ni bora zaidi ya mwingine, hatutafika mbali.”

Alisema kuwa Watanzania wanapawa kujenga tabia ya kuvumiliana na kutatua tofauti zao kwa njia ya majadiliano bila kujiingiza katika matukio yanayoweza kuharibu amani ya nchi.
“Waswahili walisema, maneno matamu humtoa nyoka pangoni. Hivyo nawatamanieni viongozi wa dini kazaneni kuwahimiza waumini wenu kutojihusisha na mienendo hatarishi kwa amani yetu,” alieleza Mwinyi, ambaye alioongoza Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995.

Sheikh DSM aonya
Akizungumzia tukio la mauaji ya padri huyo, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhaji Mussa Salum pamoja na kulitaka Jeshi la Polisi kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo.

Alisema kuwa hali ya hewa visiwani humo imechafuka na kuonyesha wasiwasi wake kuhusiana na kujitokeza kwa matukio hayo.

Alisema kuna haja kwa mamlaka kutafakari kwa makini na kujiuliza kwa nini matukio hayo yanajitokeza wakati huu ambapo baadhi ya viongozi wa dini wameendelea kushikiliwa kizuizini.
“Kwangu mimi haya ya Zanzibar yanajadilika, pia lazima tujiulize kwa nini matukio haya ya mashambulizi yanajitokeza zaidi wakati huu,” alisema.

Lowassa: Waislamu, Wakristo waungane
Waziri Mkuu aliyejiuzulu,  Edward Lowassa  amewataka Waislamu na Wakristo wote nchini kuungana kwa pamoja kuitetea na kuilinda amani iliyopo kwa vitendo.
Akizungumza katika Harambee ya Kanisa la Moravian Kanda ya Magharibi iliyofanyika katika Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, Lowassa alisema kuwa waumini hao kwa pamoja wanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja katika kuitetea amani iliyopo kwa vitendo.
Aliendelea kusisitiza kwamba kwa sasa kuna baadhi ya Watanzania wanaichezea amani iliyopo kwa sasa hapa nchini na kufanya mauaji ya watumishi wa Mungu.

 

“Hii ni Tanzania tunayoitaka kwa Waislamu na Wakristo kushirikiana katika ibada kama hii leo hapa kanisani,” alisema Lowassa.

Lowassa aliendelea kusisitiza kwamba Watanzania wanapaswa kuhakikisha kila siku wanamuomba Mungu, ili kuendeleza amani hapa nchini inadumishwa kwa hali na mali.

Alisema kwamba watu wanaomsema vibaya kila kukicha waendelea kufanya hivyo, kwani kwa kufanya hivyo wanaendelea kumuimarisha kiimani na nguvu kubwa ya ushawishi kwa watu wa Mungu ambao ndiyo wamekuwa wakimuunga mkono kila siku katika kazi ya Mungu.

Alirudia kauli yake aliyoitoa mkoani Mbeya hivi karibuni, “Mimi ni tajiri wa watu na siyo tajiri wa fedha kama wanavyosema huko mitaani  na watu wasiokuwa na mapenzi mema na Mungu,”alisema Lowassa.

Katika harambee walikuwapo baadhi ya Waislamu kutoka Mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora pamoja na viongozi mbalimbali wa siasa kutoka sehemu mbalimbli hapa nchini.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Kanda ya Magharibi, Issack Nicodemo alisema kuwa Waislamu na Wakristo hapa nchini ni ndugu kutokana na uhusiano uliopo tangu zamani.
Alisema kuwa vitendo vinavyoendelea kufanyika hapa nchini vya mauaji kwa viongozi wa dini ni vya kulaaniwa.

Imeandikwa na Salma Saidi, Elias Msuya, Zanzibar, Mustapha Kapalata, Nzega, Boniface Meena na George Njogopa, Dar

No comments:

Post a Comment