MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi amesema
ardhi ya Bagamoyo imevamiwa na watu wenye fedha kutoka Dar es Salaam
ambapo wanataka kuipora bila kufuata kanuni na taratibu za ardhi kutoka
kwa manispaa husika.
Kipozi alitoa kauli hiyo jana kwa waandishi wa
habari Bagamoyo muda mfupi baada ya kufunga mkutano ulioandaliwa na
Mtandao wa Taasisi za kiraia Bagamoyo (Bango Net) ulioshirikisha asasi
mbalimbali za kijamii ili kujadili namna ya kutumia Sh78 milioni katika
miradi ya kimaendeleo katika suala la mazingira kwa eneo hilo.
Alisema watu hao kutoka Dar es salaam wamekuwa
wakitumia fedha zao kuwarubuni baadhi ya wanavijiji wasio na ufahamu
mkubwa katika suala la ardhi,ili wawauzie ardhi matokeo yake
wanasababisha migogoro ya ardhi.
“Mimi nasema wazi kuwa Bagamoyo imevamiwa na watu
wenye fedha kutoka Dar es Salaam wanaokuja kuwarubuni wanavijiji ili
wawauzie ardhi bila kufuata sheria na kanuni na hao ndiyo wanaotuletea
matatizo ya migogoro ya ardhi katika Bagamoyo yetu. Hivyo natamka wazi
kuwa hatutaki watuletee matatizo ya migogoro ya ardhi Bagamoyo ,’’
alisema Kipozi.
Kipozi alishauri kuwa endapo watu hao anaowatuhumu
kuvamia ardhi ya Bagamoyo wafike katika halmashauri ya mji huo kwa
lengo la kufuata sheria kisha watauziwa ardhi wanazotaka na jambo hilo
litaondoa migongano ya ardhi katika eneo hilo.
Naye mkurugenzi wa Programu ya Taifa ya Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira, Jeremiah Daffa alisema Wanabagamoyo hawatakiwi
kujikweza kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete anatokea katika mkoa wao, bali
watumie fedha za miradi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuwasaidia
viongozi wanaosaidia fedha hizo za miradi kuelekezwa katika wilaya
hiyo.
“Mimi naona kuwa Bagamoyo isipojiandaa itakosa
kila kitu,mimi nashauri fedha tunazopata kwa ajili ya miradi mbalimbali
zitekelezwe kwa ufanisi ili hata wale viongozi wanaosaidia kushawishi
fedha hizo kuelekezwa katika maeneo yetu waweze kutufikiria tena na
kujivunia huko walipo, lakini tuna mfano mbaya katika fedha za Mancemp.
Huku kwetu hakuna kitu cha maana kilichofanyika kutokana na fedha hizo
jambo ambalo hatutaki lijirudie katika eneo letu,’’ alisema Daffa.
No comments:
Post a Comment