‘Presha’ ya uchaguzi, ahadi zawatorosha wabunge Dodoma

 

 Bunge likiendelea katika Kikao cha tisa cha mkutano wa 11wa Bunge mjini  Dodoma jana.
 Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Sharon Sauwa


Dodoma. Baadhi ya wabunge wamesema kukosekana bungeni kwa wenzao wanaofikia 200 hata kuhesabiwa ni watoro, kumetokana na wengi wao kutokamilisha ahadi kwa wapigakura wao walizotoa mwaka 2010, hivyo kulazimika kukimbilia majimboni ili kujaribu kuzikamilisha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti bungeni hivi karibuni, walisema wengi wao bado hawajakamilisha ahadi walizoahidi walipoomba kura na sasa umefika mwaka wa uchaguzi.

“Wengine wamesafiri nje ya nchi kikazi. Si unajua hiki ni kipindi kigumu kwa sababu tunaingia kwenye uchaguzi. Wamekwenda majimboni kufanya maandalizi ya uchaguzi,” alisema Mbunge wa Mufindi Kusini (CCM), Mendard Kigora.

Alisema yeye yupo bungeni tangu Mkutano wa 19 ulipoanza kwa sababu ameshakamilisha ahadi zake kwa asilimia 90.

“Sina wasiwasi, nimekuja bungeni kuhakikisha nashiriki kutunga sheria zote, ili ‘next year’ (mwaka ujao) tuzisimamie vizuri. Sitaki muswada hata mmoja unipite,” alisema Kigora.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christowaja Mtinda alisema wabunge wengi wako majimboni kwa sababu huu ni wakati wa lala salama na hawajakamilisha ahadi walizoahidi.

“Wapo majimboni kuwaweka sawa wananchi wao kabla ya uchaguzi hasa kwa upande CCM, wengine wako huko kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa,” alisema.

Alisema wabunge walio chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wana ratiba kila wanapokamilisha mikutano ya Bunge hurudi majimboni kwao kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao.

“Sisi hatuko kama upande wa pili (CCM), hatusubiri hadi uchaguzi ukaribie. Tuna ratiba, tukitoka hapa tunakwenda moja kwa moja majimboni kukamilisha ahadi zetu,” alisema.

Mbunge wa Karagwe (CCM), Godbless Blandes alisema kuwa wabunge wengine wako katika kamati mbalimbali za Bunge wakijadili miswada itakayowasilishwa katika vikao vinavyoendelea.

“Miswada ni mingi inayoingia katika Bunge hili, kwa hiyo wakati mwingine unakuta wabunge wako katika kamati zao wakijadili miswada yao,” alisema.

Alisema wabunge wengine wana dharura za kuugua au majimboni mwao kuna kero hali inayowalazimu kwenda huko kuzitatua kabla ya kurejea tena kwenye vikao vya Bunge.

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR Mageuzi), Moses Machali alisema wabunge wengi wana wasiwasi na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, hivyo wako majimboni.

“Presha imepanda, wako majimboni wanajitahidi kuweka mambo sawa kabla ya uchaguzi,” alisema.

Hata hivyo, alisema yeye hana wasiwasi kwani anajua wenye haki ya kumpa kura katika uchaguzi ni wananchi.

“Hakimu wa ubunge wangu ni mwananchi. Kama wanaona nilifanya vyema basi watanichagua tena, wao ndiyo wenye ‘kisu’ bwana wanaamua, nipite, nisipite ni sawa tu kwa kuwa mimi sina uamuzi wa mwisho,” alisema Machali.

Kukithiri kwa utoro kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano vinavyoendelea ilibainika hivi karibuni baada ya ofisi ya chombo hicho cha kutunga sheria kusema kuwa kina taarifa za wabunge 15 pekee walioomba ruhusa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Bunge hilo, linalotakiwa kuwa na wabunge 357, lilishindwa kupitisha miswada mitatu iliyohitaji theluthi mbili ya wabunge wa kila upande wa Muungano.

Wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama wiki iliyopita kulikuwa na wabunge 81 ndani ya Ukumbi wa Bunge, jambo linalomaanisha kuwa takriban wabunge 250 hawakuwamo.

Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati kikao cha Bunge hilo kilipoanza kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi kwani kulikuwa na wabunge 29 tu ukumbini.

Hali hiyo ilimaanisha kwamba zaidi ya wabunge 320 hawakuwamo ndani kujadili suala hilo nyeti kwa mustakabali wa Taifa.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema : “Wabunge 15 tu ndiyo wenye ruhusa, wengine wapo lakini wanaingia na kutoka bungeni. Kutokuwapo kwao kunaathiri sana wakati wa kupitisha miswada kutokana na kutotimia kwa akidi.”

Idadi ya wabunge walio na ruhusa ni ndogo ikilinganishwa na viti vingi vinavyokuwa vitupu wakati wa mijadala mbalimbali kwenye vikao vya Mkutano wa 19 vinavyoendelea mjini Dodoma.

Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa jambo hilo linathiri shughuli mbalimbali za Bunge zinazotakiwa kufanyika.

Kaimu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu anasema utoro wa wabunge unakwamisha mambo mengi ya msingi bungeni, huku akibainisha kuwa miswada haiwezi kupitishwa huku kukiwa na idadi ndogo ya wabunge na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka kanuni.

“Ukiingia bungeni unakuta ukumbi mtupu kabisa, lakini ukitoka nje unakutana na wabunge wengi wakizurura. Kanuni zinasema kuwa ili muswada upitishwe inatakiwa kuwe na wabunge walau nusu,” alisema Lissu.

Lissu alisema huenda kukosekana kwa wabunge hao kukawa kunachangiwa na Uchaguzi Mkuu, kwani wengi wamejikita majimboni.

“Pia wapo ambao wamekwenda safari za kibunge, lakini si wengi kufanya Bunge liwe tupu.”

Wabunge wengi hawaonekani bungeni, lakini wamekuwa vinara wa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii katika majimbo yao hasa kipindi hiki, kitu kinachoonekana kuwa ni kujiweka karibu na wananchi.

Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu katika majimbo yao.

Mbali na kutoonekana bungeni kutokana na kujikita kuweka mikakati ya ushindi majimboni, baadhi ya wabunge pia wamekuwa watoro wa kuhudhuria vikao vya Bunge, kama wakionekana asubuhi, jioni ni nadra kuwaona.

Baada ya kujadili muswada wa Uhamiaji wiki iliyopita, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib Mnyaa aliomba mwongozo wa Spika kuhusu idadi ya wabunge kuwa ndogo.

Mbunge huyo alisema kwa idadi hiyo itakuwa kinyume na kanuni kama Bunge litapitisha muswada. “Ninavyofahamu ili tuweze kupitisha muswada huu wabunge tunaotakiwa kuwemo humu ndani ni kuanzia 176, lakini nikitizama idadi yetu hata 100 hatufiki, kutokana na suala hili naomba mwongozo wako,” alisema Mnyaa.

Akijibu suala hilo, Spika Makinda alisema: “Naona kuna watu wapo kwa ajili ya kukwamisha vitu tu. Haya tuendelee.”

Baada ya majibu ya Spika, idadi ya wabunge iliongezeka kidogo na kufikia 139.

Akizungumzia muswada huo, Lissu alisema itakuwa vigumu kupitishwa kwa sababu unatakiwa kupigiwa kura na theluthi mbili ya wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar.

“Sijui kama muswada huu utaweza kupita maana ukitizama idadi ya wabunge si rahisi kupata theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara,” alisema Lissu. Licha ya idadi kuwa ndogo, mjadala uliendelea na hatimaye muswada huo ukapitishwa.

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema utoro huo hautoi picha nzuri kwa wananchi kwani wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wanatakiwa kuhudhuria vikao vya Bunge.

Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alisema: “Kukosekana kwa mbunge kuna sababu nyingi, wapo walioomba ruhusa kutokana na kuwa na sababu maalumu na pia wapo waliopo majimboni. Ila binafsi naona ushiriki wetu bungeni ni jambo muhimu.”

Tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge Machi 17 mwaka huu, idadi ya wabunge imekuwa ndogo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliokuwa na mahudhurio makubwa kutokana na kujadili sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Katika mkutano wa 18 ulioisha Februari mwaka huu, wabunge wengi waliokuwa wakichangia hoja, walijikita katika kuzungumzia matatizo ya majimbo yao na kuacha mjadala uliokuwa mezani.

Jambo hilo lilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wajikite kwenye hoja za msingi na si kuzungumzia masuala ya majimbo

No comments:

Post a Comment