WABUNGE: TUKO TAYARI KUWEKA WAZI MAJIBU YA UKIMWI
Baadhi
ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesema wako
tayari kuweka wazi majibu ya vipimo vya mambukizi ya virusi vya ugonjwa
wa ukimwi (VVU) hata kama watakuwa wameathirika.
Walisema hayo kwa nyakati tofauti jana muda mfupi baada ya uzinduzi wa
kitabu cha mwongozo kwa ajili ya kuwawezesha wabunge kupambana dhidi ya
Ukimwi, uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Changamoto iliyopo kwenye mabunge yetu ni kwa wabunge kujiweka wazi na
kusema mimi hapa nimeathirika. Mimi nikipimwa nikakutwa ninao, niko
tayari kujitangaza,” alisema Beatrice Shellukindo, ambaye ni Mbunge wa
Kilindi (CCM).
Pia Mbunge wa Muheza (CCM), Herbert Mtangi, alisema yuko tayari kupima afya kwani ni kawaida yake kufanya hivyo.
Aliwataka wabunge wenzake kujiweka wazi iwapo wameathirika wasiogope kwenda kuchukua Dawa za Kuongeza Nguvu (ARVs).
Uzinduzi wa kitabu hicho ulifanyika kwa ushirikiano wa Umoja wa Mabunge
Duninai (IPU) na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jina la
kitabu hicho ni ‘Raising the profile of HIV and AIDS in your
Parliament’.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Masula ya Ukimwi, ambaye pia
ni Mjumbe IPU, Lediana Mng’ong’o, alisema kitabu hicho kinalenga
kuwahamasisha wabunge kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ukimwi
ndani ya mabunge yao na majimboni mwao.
Mbunge wa Bunge la Seneti nchini Ubelgiji, ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ushauri kuhusu Masuala ya Ukimwi katika IPU, Marleen
Temmerman, aliipongeza Tanzania kwa kuwa mfano baada ya Rais pamoja na
wabunge kupima afya zao.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba.
Washiriki walikuwa ni mabalozi, wabunge pamoja na wadau wengine wa kupambana na Ukimwi kutoka nchi mbalimbali duniani.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment