Bodaboda wapambana na polisi Mwanza

 

POLISI mkoani Mwanza wamelazimika kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waendesha bodaboda waliokuwa wakiwalazimisha askari wawaachie wenzao waliowakamata kwa makosa mbalimbali.

Wakati hayo yakitokea Mwanza, huko Arusha, madereva teksi walipandwa na jazba baada ya kuzuka kwa mzozo kati yao na uongozi wa Hoteli ya Palace kutokana na kile walichoeleza kuwa ni kuondolewa kinyemela katika eneo lao.
Huko Mwanza, ghasia hizo ziliibuka wakati polisi wa usalama barabarani na kikosi maalumu cha ukaguzi wa magari walipofanya doria kukagua leseni na uhalali wa madereva hao wanaofanya shughuli za kusafirisha abiria.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, vurugu hizo zilianza saa 2:46 asubuhi baada ya polisi kuwakamata waendesha bodaboda wapatao 26, ambao walitozwa faini za papo kwa papo kulingana na makosa yao, huku wengine wakiendelea kushikiliwa.
Hatua hiyo iliwafanya waanze kujikusanya kutoka sehemu mbalimbali na kuandamana hadi eneo kulikokuwa limetengwa kwa ukaguzi huo katika Mtaa wa Mission.
Baada ya kufika eneo hilo, walianza kuwarushia mawe askari hao, huku baadhi yao wakiendesha pikipiki kuzunguka eneo hilo na kuzuia magari kupita hali iliyozua tafrani. Baada ya kutokea hivyo, askari hao walilazimika kuwaita askari wengine ili kuwakabili vijana hao.
Vurugu hizo zilizodumu kwa saa tatu, zilisababisha kufungwa kwa barabara iendayo Uwanja wa Ndege na katika eneo la Pasiansi, huku baadhi ya abiria wakilazimika kuteremka katika daladala na kukimbia ovyo na wengine kulala katika mifereji ya maji machafu baada ya milio ya risasi na mabomu ya machozi kuanza kurindima.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu alisema jana kwamba polisi hao walikuwa katika ukaguzi wa leseni na vifaa vingine vya usalama kama kofia ngumu ndipo baadhi ya madereva hao wa bodaboda wakaanza kupinga kukamatwa kwa wenzao na kutozwa faini kutokana na makosa waliyokuwa nayo.
Mmoja wa waendesha bodaboda ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema kwamba polisi wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuwachukulia leseni zao, huku wakiwabambikiza makosa mbalimbali kwa lengo la kujipatia fedha kinyume cha sheria.
Kamanda Mangu aliwataka waendesha bodaboda hao kutoa taarifa wanaponyanyaswa au kuombwa rushwa na askari hao.

Mzozo Arusha
Huko Arusha, tafrani ilizuka jana asubuhi baada ya Umoja wa Madereva Teksi wa Baracuda kupinga amri ya kuondolewa katika eneo hilo linalodaiwa kupewa Hoteli ya Palace kwa kuondoa minyororo iliyowekwa kama uzio kuzungushia eneo hilo.
Hali ilianza kuwa tete kuanzia saa mbili wakati madereva hao walipofika kuegesha magari hapo na kukuta eneo hilo limeandikwa michoro mbalimbali kuashiria kwamba ni mali ya maegesho ya magari ya hoteli hiyo tu, huku likiwa limezungushiwa minyororo ya mipaka.
Hali hiyo iliwafanya waje juu na kuchukua hatua ya kuiondoa minyororo hiyo kwa nguvu na kusababisha mzozo baina yao na watumishi wa hoteli hiyo.
Baada ya vurugu hizo kushika kasi, mmoja wa maofisa wa polisi alifanya kazi ya ziada kuwatuliza madereva hao waliokuwa na jazba na kuwaongoza hadi katika Ofisi za Jiji la Arusha ili kupata suluhu.
Mwenyekiti wa Umoja huo, Justin Msigiti alisema wanapinga eneo hilo kupewa Hoteli ya Palace akisena ndiyo sehemu wanayofanyia biashara kwa muda mrefu na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha unalitambua hilo.
Alisema eneo hilo ni sehemu ya wazi na kilichofanyika ni baadhi ya watumishi wa Jiji la Arusha kuwazunguka na kuligawa eneo lao na kuapa kwamba kamwe hawataondoka katika eneo hilo na wako tayari kwenda mbele ya vyombo vya sheria kudai haki yao.
Huku akionyesha barua waliyoandikiwa na uongozi wa halmashauri hiyo ya kutoondoka katika eneo hilo yenye Kumbukumbu AMC/MENG/MM/VOL.1/195 iliyosainiwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa zamani wa jiji hilo, Estomi Chang’ah ya Oktoba 18, 2012 alisema:

 “Ninashangaa, tuna haki zote halafu tunaondolewa ilhali tayari kuna maagizo ya sisi kubaki katika eneo hili. Manispaa inatambua kuwapo kwa Kituo cha Teksi cha Baracuda katika Barabara ya Makongoro,” alisema.

No comments:

Post a Comment