Rais Mstaafu Benjamin Mkapa
WITO wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kutaka
suluhu ya mgogoro wa gesi unaoendelea baina ya Serikali na wakazi wa
mikoa ya kusini, umepokewa kwa hisia tofauti. Baadhi ya wasomi
wamempongeza huku wakazi kadhaa wa Mtwara wakimpinga.
Juzi, baada ya mgogoro huo kuendelea kwa
takriban mwezi mmoja sasa, Mkapa alizitaka pande hizo mbili kutafuta
mwafaka akieleza kuwa linalowezekana leo, lisingoje kesho.
“Mtafaruku huu haufai kuachwa na kutishia
usalama, mipango ya maendeleo siyo siri, mikakati na mbinu za
utekelezaji wake siyo siri. Maelezo yake mazuri yanaweza kutolewa
yakadhihirisha namna na kasi ambayo rasilimali zinawanufaisha wananchi
wa eneo zilimo na taifa zima,” alisema Mkapa katika taarifa yake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),
Dk Benson Bana alisema jana kuwa kauli ya Mkapa ni nzuri, huku
akisisitiza kuwa katika suala hilo, lazima utaifa uwekwe mbele.
“Hata
wakati wa ujenzi wa Barabara ya Mtwara, wapo waliosema kuwa mikoa ya
kusini inatengwa, kauli hizi zilikuwapo tangu zamani, kikubwa ni suala
hili kuchukuliwa kitaifa zaidi,” alisema Dk Bana.
Wazee watafuta suluhu Dar
Wazee wa Mtwara
Mikindani wako Dar es Salaam kusaka suluhu ya mgogoro huo, baada ya
kusema kwamba wamebaini kuwa kutakuwa na uvunjifu wa amani kama suala
hilo litaachwa liendelee.
Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, wazee hao walisema suala hilo linaleta hofu kubwa kwa taifa
hivyo linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Katibu wa wazee hao, Selemani Mademu alisema wananchi wa Mtwara wako tayari kufa kuliko kuona wakidharauliwa katika suala hilo.
Mademu alisema: “Wananchi wa Mtwara wanaamini
kuwa kituo cha kuchakata gesi asilia kama kitajengwa Mtwara kitatoa
fursa kubwa ya kushawishi wawekezaji ambao watajenga viwanda
vitakavyotumia malighafi ya gesi asilia na hivyo kuchochea maendeleo ya
Mtwara kwa jumla,” alisema na kuongeza kuwa kama Serikali inaamini
kwamba wazo lake la kuisafirisha hadi Dar es Salaam ni jema na lenye
manufaa kwa wananchi wa Mtwara, ingejikita katika kutoa elimu badala ya
kukaa kimya na kuendelea na kile inachoamini.
“Wanamtwara hatupendi kuendelea kuelezwa
kwamba tutanufaika na gesi iliyogunduliwa kwa kuahidiwa viwanda kama
ambavyo imekuwa desturi ya Serikali yetu. Tunahitaji vitendo vitawale
badala ya ahadi ambazo hazitekelezeki. Kwa mfano barabara, umeme,
kuimarishwa kwa bandari, mikopo kwa ajili ya ujasiriamali, viwanda
vidogo vya kubangua korosho n.k.” alisema.
Wengine wapinga
Mwenyekiti wa Umoja wa
Maendeleo Mikoa ya Kusini (UMMK), Said Mannoro (72) alimshutumu Mkapa
akidai kuwa ndiye chanzo cha gesi ya Songosongo kupelekwa Dar es Salaam.
Mzee Mannoro ambaye alifika katika ofisi za
gazeti hili, Tabata Relini, Dar es Salaam jana alisema Mkapa anatakiwa
kueleza faida walizopata wananchi wa Lindi baada ya gesi ya Songosongo
inayozalishwa mkoani humo, kupelekwa Dar es Salaam.
Mbali na mzee huyo, baadhi ya viongozi wa dini
na vyama vya siasa nao wamempinga Mkapa wakisema kuwa ushauri wake
umeegemea upande mmoja na kwamba alipaswa kumshauri Rais Jakaya Kikwete.
Askofu Mteule wa Kanisa la KKKT Dayosisi Mpya
ya Kusini Mashariki, Mchungaji Lucas Mbedule alisema Mkapa, amechelewa
kutoa ushauri wake na kwamba kwa hali ya sasa alipaswa kumshauri Rais
Kikwete akubaliane na matakwa ya wananchi.
“Namheshimu sana Mkapa, lakini amechelewa kutoa kauli yake,
yeye alipaswa kumshauri Rais mwenzie. Kutoa tamko lake saa hizi
kunatufanya tuwe na shaka naye. Nasikitika kuwa kauli aliyoitoa
haitakuwa na msukumo kwa wakati huu,” alisema Mchungaji Mbedule ambaye
alishawahi kutoa msimamo wake wa akipinga mradi huo na kuongeza:
“Usiwalaumu kwa kuandamana na kuitisha
mikutano, jiulize ungejuaje kama wananchi hawataki mpango wa Serikali wa
kusafirisha gesi, kama siyo kupitia maandamano, mikutano na mihadhara?
Atambue kuwa suala hili lilianza kabla ya maandamano nani alijua kuwa
Mtwara hawataki gesi itoke? Nilidhani amshauri Rais Kikwete asitishe
mradi huo.”
Msemaji wa Shura ya Maimamu mkoani Mtwara,
Sheikh Abubakari Mbuki alisema: “Tunamheshimu sana Mkapa lakini nachelea
kusema amekosea… siku nyingi alikuwapo Mtwara, suala la gesi
alilifahamu kwa nini asiliseme mapema? Anaotaka kuzungumza nao wapo
Mtwara kwa nini akazungumzie Dar es Salaam?” alisema Sheikh Mbuki na
kuongeza:
“Tutaendelea na makongamano, kwa nini
afedheheshwe na harakati zetu na asifedheheshwe na kauli za Mkuu wa Mkoa
(wa Mtwara, Joseph Simbakalia), Waziri wa Nishati na Madini (Profesa
Sospeter Muhongo) na Rais Kikwete, anadhani wao wapo sahihi?... Kubeza
maandamano na mikutano ni kuwakosea Wanamtwara.”
Askofu wa Kanisa la Angalikana Dayosisi ya
Newala, Oscar Mnung’a akizungumzia tamko la Mkapa alisema: “Nadhani
amechelewa… awaite viongozi aliowaachia madaraka awaambie wasipuuzie
jambo hili … naunga mkono hoja ya Serikali kukaa pamoja na wananchi wa
Mtwara… maandamano ni haki ya msingi ya Kikatiba wasipuuzwe unafikiri
wangefanya nini kama hawasikilizwi?”
Aliongeza: “Tanzania tumekuwa mafundi wa
kutatua migogoro ya wenzetu, kinawashinda nini katika hili? Hapa ni
suala la kuweka wazi mikataba, kama kweli Serikali ina mipango mizuri na
wananchi wa Mtwara si iweke wazi. Wanashindwaje kujieleza, kuna nini
hapa? Wajibu hoja wasitafute mchawi, mjusi ukimfukuza sana mwisho
anakuwa nyoka… wananchi hawa wamesema basi.”
“Lazima sisi (viongozi wa dini) tuseme kwa
sababu kwenye waumini wetu wapo maskini… sasa tunaposema, mtu mwingine
asianze kumtafuta aliyesema, sioni kama ni busara badala ya kutatua
tatizo, anawalaumu watu kuwa ndiyo chanzo cha tatizo… kigugumizi cha
nini kama mradi una maslahi na watu wa Mtwara?”
No comments:
Post a Comment