Msanii wa fani ya maigizo, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu
MSANII wa fani ya maigizo, Elizabeth Michael,
maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia ameiomba
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imwachie huru kwa dhamana.
Lulu kupitia kwa wakili wake aliwasilisha ombi
hilo Mahakama Kuu ya Tanzania na Ijumaa jaji anayeisikiliza kesi hiyo
anatarajia kutoa uamuzi.
Tangu kilipotokea kifo cha msanii mwenzake, Steven
Kanumba, Aprili 7, mwaka jana Lulu amekuwa akisota mahabusu na dhamana
yake ikawa imezuiwa kwa mujibu wa kesi za mauaji.
Hata hivyo baada ya kukamilika kwa upelelezi,
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alimbadilishia mashtaka na kuwa ya kuua
bila kukusudia hivyo kumuweka katika mazingira ya kupatiwa dhamana.
Habari zilizopatikana mahakamani hapo jana zilisema kuwa tayari maombi
hayo ya dhamana yamepangwa kusikilizwa na Jaji Zainabu Muruke, Januari
25 ,2013.
Maombi hayo yamewasilishwa chini ya hati ya
dharura wakiomba yasikilizwe na kuamuriwa mapema kwa madai kuwa
mshtakiwa amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kwamba kosa lake
linadhaminika.
Katika hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya
kiapo cha wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba
mahakama iamuru mshtakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na
wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo mahakama itaona
yanafaa.
Hati hiyo ya maombi ya dhamana inasema, “Kwamba
tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshtakiwa akiwa na au bila
kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake
ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, iliyoko katika mahakama
hii tukufu.”
Alidai kuwa akiwa wakili wa mwombaji, anatambua
kuwa mwombaji anao wadhamini wa kuaminika ambao wako tayari kufika
mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.
Wakili Kibatala katika hati yake hiyo ya kiapo
anadai kuwa akiwa wakili wa mshtakiwa, ikiwa mshtakiwa huyo atakubaliwa
dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana
yatakayotolewa na mahakama.
Aliendelea kudai kwamba kwa muda ambao ameiendesha
kesi hiyo amepata fursa kubwa ya kufahamiana na mwombaji pamoja na
familia yake na kwamba kwa msingi huo anajua kuwa mwombaji huyo ana
tabia nzuri na ni wa kuaminika.
“Mwombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi
wake ambao wako tayari kuhakikisha kuwa anatimiza masharti na
kuhakikisha kuwa anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika
kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote’, alisema.
“Mwombaji ni mtu maarufu na mkazi wa Dar es Salaam
na hivyo kwa mazingira haya ni rahisi kumfuatilia katika utekelezaji wa
masharti yoyote ya dhamana,” anasisitiza Wakili Kibatala na kuongeza:
“Pia niko tayari, kama wakili wake kutimiza wajibu wangu kuhakikisha
mwombaji anatimiza masharti yote kikamilifu, na kufika mahakamani kadri
na wakati atakapohitajika.
Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, Aprili 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment