Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amependekeza
katiba mpya izuie adhabu ya kifo kwa kosa la kukusudia au uhaini hapa
nchini na iruhusu elimu kutolewa bila malipo kwa shule za sekondari.
Pia amependekeza katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha
fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni za chaguzi za
kuwania uongozi na pia ifafanue rushwa ni nini kwenye chaguzi hizo.
Mapendekezo hayo, ambayo ni sehemu ya maoni ya Lowassa kuhusu uundwaji
wa katiba mpya, aliyatoa alipokutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
jijini Dar es Salaam jana.
ADHABU YA KIFO
Lowassa alisema katiba ya sasa haisemi wazi kuhusu adhabu ya kifo, badala yake inazungumzia tu haki ya uhai.
Alisema Ibara ya 14 ya katiba ya sasa inatamka kijumla tu kuwa kila mtu
ana haki ya kuishi na uhai wake kulindwa, lakini haki hiyo
inanyang’anywa na kifungu namba 196 cha sheria ya kanuni za adhabu sura
ya 16, kinachotamka kuwa adhabu ya kifo kwa kosa la mauaji ya kukusudia
na kwamba adhabu hiyo hiyo pia hutolewa kwa kosa la uhaini.
“Sasa mapendekezo yangu mimi ni kwamba, kuwe na ibara katika katiba mpya
inayotamka wazi kuwa hakutakuwa na adhabu ya kifo hapa nchini hata kwa
kosa la kukusudia au uhaini,” alisema Lowassa.
ELIMU BURE
Kuhusu elimu bila malipo, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM)
alisema moja ya haki za mtoto ni kupata elimu hivyo, alipendekeza suala
la elimu bure ya sekondari liwekwe kwenye katiba ya nchi.
“Katiba itamke wazi kuwa elimu ya sekondari ni bure,” alisema Lowassa na
kuongeza: “Nchi bado ina idadi kubwa ya watu maskini, ambao uwezo wao
wa kipato ni mdogo.”
Kutokana na hali hiyo, alisema anaamini suala hilo linawezekana na
serikali inaweza kugharimia elimu ya sekondari ili iwe bure kwa wote.
Alisema mfumo huo utatoa nafasi ya kujenga taifa lijalo lenye idadi kubwa ya vijana watakaokuwa wamepata elimu ya sekondari.
“Wabunge wenzangu bila shaka wanalijua hili. Ukweli katika majimbo yetu
wazazi wamekuwa wakishindwa kulipia karo ya shule kwa watoto wao.
Wabunge tumekuwa tukibeba mzigo huo japo kidogo. Kwa hiyo, kifungu cha
elimu bure kwa sekondari, kiwapo kwenye katiba,” alisema Lowassa.
Pendekezo la kutaka elimu ya bure linafanana na Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) ya mwaka 2010 ambayo
kiliahidi kuwa kingetoa elimu ya bure kuanzia shule za msingi hadi
sekondari.
Ilani hiyo ilisema: “Elimu ya ngazi ya msingi na sekondari itagharimiwa
na serikali kuu pamoja na serikali za mitaa. Lengo ni kuhakikisha kuwa
elimu hii ya msingi kabisa itakuwa ni haki kwa kila mtoto wa Kitanzania
na kiwango cha ubora kinalingana kwa nchi nzima.”
MATUMIZI YA FEDHA KATIKA UCHAGUZI
Lowassa alisema katika sehemu nyingi nchini, mwananchi kama hana fedha
hawezi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Hivyo, alipendekeza
katiba mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha, ambacho
mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni.
Pia alipendekeza ibara hiyo iainishe ni matumizi gani ya lazima, ambayo
mgombea hawezi kukwepa kutumia fedha katika kampeni zake.
“Mfano, kuwakusanya wapigakura kwenda kupiga kura gharama hizo nani
azibebe,” alisema Lowassa. Pia alipendekeza Katiba Mpya ifafanue rushwa
ni nini kwenye chaguzi hizo.
“Au tuwe na proportional representation (uwakilishi wa uwiano), vyama
viwe ndiyo vinaingia kwenye chaguzi kuwania majimbo na siyo wanachama,
huko kila mtu atakuwa anapigania chama chake kupata kura nyingi ili
wapate viti vingi zaidi, pengine hii itasaidia kuondoa kikwazo cha mtu
kuwa na uwezo wa kifedha ndiyo aweze kuwania uongozi,” alisema Lowassa.
ARDHI
Lowassa alisema kwa mwanadamu, kunyang’anywa haki ya kutumia ardhi ya
nchi aliyozaliwa ni sawa na kunyang’anywa haki ya uraia wake.
Alisema katiba ya sasa inawapa nguvu wakulima katika suala la ardhi na
kuwasahau wafugaji, ambao alisema wamekuwa wakimbizi katika nchi yao.
“Wamekuwa wakitangatanga kutafuta malisho ya mifugo yao. Ile ardhi
waliyokuwa wanaimiliki wakiondoka kutafuta malisho huku nyuma imekuwa
ikimilikishwa watu wengine; wakulima au wawekezaji. Hili kwakweli si
jambo jema. Tumeshuhudia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na
wafugaji,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, alipendekeza katiba mpya impe mfugaji haki katika
suala la ardhi kama wakulima na ardhi ya wafugaji ilindwe, ikiwa ni
pamoja na haki hiyo kufafanuliwa kikatiba.
Pia alipendekeza kuwapo na hali ya usawa (50,50 situation) kati ya
mfugaji na mkulima katika suala zima la umiliki wa ardhi kikatiba.
No comments:
Post a Comment