Mahakama yahamia kanisa lililoharibiwa Mbagala

Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Walialwande Lema ( kushoto), akipata vielelezo ikiwa ni ushahidi katika kesi ya uchomaji makanisa Mbagala kutoka kwa Mhasibu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbagala, Bernard Maimu ( kulia), wakati mahakama hiyo ilipohamia katika kanisa hilo jana.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilihamia kwa muda katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbagala wilayani Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, kushuhudia uharibifu ulitokana na majengo yake kuchomwa moto na kuvunjwa.

Kanisa hilo ni miongoni mwa makanisa yaliyochomwa moto katika vurugu za dini zinazodaiwa kufanywa na kikundi kilichokuwa katika mwavuli wa dini ya Kiislamu Oktoba mwaka jana.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, kuwasilisha ombo ili ishuhudie  uharibifu huo.

Mahakama hiyo ilikubaliana na ombi hilo na msafara kuongozwa na Hakimu Mkazi, Walialuande Lema.

Awali kesi hilo ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Augustina Mbando, lakini jana ilikuwa kwa Hakimu Lema.

Katika msafara huo kulikuwa na magari yapatayo nane yakiwamo manne ya Jeshi la Polisi, matatu yalikuwa yamebeba askari na moja Hakimu  Lema.

Kulikuwa na mabasi mawili ya Jeshi la Magereza ambayo yalikuwa yamebeba washtakiwa hao 10 na maaskari wake yakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Hamadi Sokodo, Shego Mussa, Mashaka Iman, Hamza Mohamed, Mikidadi Sadiki, Issa Selemani, Juma Jumanne, Hamisi Masud, Ramadhani Mbulu na Mohamed Yusuph.

Vilevile, kulikuwa na magari ambayo yalikuwa yamewabeba mawakili wa Jamhuri na utetezi na wafanyakazi wa mahakama hiyo.

Baada ya kuwasili kanisani hapo majira ya saa 5:30 asubuhi,   ulipokelewa na uongozi wa kanisa hilo ukiongozwa na Mhasibu wake, Bernard Maimu na kujionea uharibifu huo.

Maimu alimuonyesha Hakimu Lema na watu waliokuwepo katika msafara huo mali zilizoharibiwa  zikiwamo feni, milango, kiyoyozi, mfumo wa umeme, samani, madhabahu na uzio wa kanisa vyenye thamani ya Sh. milioni 500.

Kadhalika, Hakimu Lema na msafara wake, walishuhudia Ofisi ya Mchungaji wa Kanisa hilo lilivyoharibiwa kwa kuchomwa moto, ofisi ya Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) ya kanisa ilivyovunjwa.

 Baada ya kushuhudia hayo, upande wa utetezi ulidai hauna pingamizi, hivyo upande wa Jamhuri uliomba ipange  tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Pia, uongozi wa kanisa hilo ulimuomba Hakimu Lema ruhusa ya kukarabati ofisi hizo kwa sababu ameshuhudia uharibifu huo.

Hakimu Lema alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, mwaka huu itakapoanza kusikilizwa na kuamuru washtakiwa hao kurejeshwaa rumande.

Awali Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, alidai kuwa  Oktoba 10, mwaka jana katika eneo la Mbagala Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walitenda kosa hilo baada ya mmoja wa watoto waliokuwa wakicheza na kubadilisha mawazo ya kidini kukojolea Kur'ani.

Alidai kuwa kitendo hicho kilisababisha watu wanaosadikiwa kuwa ni waislam kuvamia kanisa hilo lililopo Mbagala  Zakhem Oktoba 12, mwaka jana, kuvunja uzio kisha kuchoma moto ofisi hiyo na kuvunja nyingine.

Alidai vilevile walivunja milango na kuharibu madirisha, feni, madhabahu, makabati ya kuwekea vitabu, mfumo wa umeme,  kiyoyozi na kuiba kompyuta, printa na spika.

Alidai kabla ya matukio hayo, walitishia kumuua mlinzi wa kanisa hilo, Michael Samweli na kusababisha kujihami kwa kukimbia na kuacha lindo lake.  Washtakiwa hao walikana mashtaka.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa wapatao 36 walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 17, mwaka jana na kusomewa mashtaka.

No comments:

Post a Comment