Mbatia, Kafulila kumaliza tofauti zao za kisiasa
James Mbatia
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James
Mbatia amesema chama hicho bado kinatafuta njia bora ya kumaliza tofauti
zake na mbunge wake, David Kafulila (Kigoma Kusini).
Kafulila alifukuzwa uanachama Desemba, 2011 pamoja
na wajumbe wengine sita akiwamo aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho
katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Hashim Rungwe.
Uamuzi huo ulitolewa kwenye kikao cha dharura cha
Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho kilichoketi Dar es Salaam na
kutawaliwa na vurugu mpaka polisi wakaitwa ili kuongeza ulinzi.
Licha
ya kuomba msamaha wajumbe wa mkutano huo hawakubadili uamuzi wao, licha
ya Kafulila kupinga uamuzi wa kikao hicho kumvua uanachama kwa madai
ya utovu wa nidhamu kwa kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam.
Baada ya siku kadhaa Mahakama hiyo ilitoa amri ya
muda ya kusitisha utekelezwaji wa azimio la kikao cha Nec kilichomvua
uanachama Kafulila, kumfanya apoteze sifa ya kuwa mbunge.
Katika
vipindi tofauti aliwahi kufanya mikutano ya hadhara katika jimbo lake,
na kumfanya Katibu Mkuu wa NCCR, Samwel Ruhuza kuibuka na kumtaka aache
kufanya mikutano hiyo kwa tiketi ya chama hicho.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbatia alisema
bado chama kinatafuta njia nzuri ya kumaliza tofauti hiyo, kwamba kauli
alizowahi kuzitoa mbunge huyo ziliwaudhi baadhi ya watu ndani ya chama
hicho.
“NCCR ni taasisi ambayo sio mali ya Mbatia wala mtu yoyote na
itaendelea kuwepo hivyo ni lazima masuala ya chama tukayajadili kama
chama,”alisema Mbatia.
Alifafanua kuwa suala la mbunge huyo bado linatafutiwa njia nzuri ya kumalizwa.
Mbatia
alisema siyo muda mwafaka kulizungumzia suala hilo kwa kuwa NCCR ni
chama kinachofanya mambo yake kwa njia za kidemokrasia.
Hata hivyo, alipoulizwa kama suala hilo
litajadiliwa nje ya Mahakama alisema kuwa hawezi kueleza kiundani. “Hayo
ni mambo ya chama, nisingependa kulizungumzia suala hili, tuacheni
tutamaliza mambo yetu ndani ya chama” alisema Mbatia.
Kwa upande wake, Kafulila aliwahi kulieleza gazeti
hili kuwa kama chama hicho kitakuwa tayari kufanya naye mazungumzo yupo
tayari kuondoa kesi hiyo mahakamani.
No comments:
Post a Comment