Mjadala wa kwanza kati
ya wagombea wa urais kuwahi kufanyika Kenya ulifanyika Jumatatu usiku
kati ya wagombea 8 wanaowania wadhifa huo.
Ingawa wagombea wote walishiriki kwenye mjadala
huo, kura ya maoni inaonyesha kuwa kinyang'anyiro kitakuwa kikali kati
ya Naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta na waziri mkuu Raila Odinga.
Akihutubia wakati wa mjadala huo
Bwana Kenyatta, alisema kuwa ukabila umekuwa donda sugu ambalo limekumba
nchi nzima kwa muda mrefu.
Zaidi ya watu elfu moja waliuawa wakati wa ghasia za kikabila baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 uliokumbwa na utata.
Kenyatta anakabiliwa na kesi ya uhalifu wa
kivita katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC, baada ya kuhusishwa na
ghasia hizo. Mgombea mwenza wake William Ruto pia anatakiwa na mahakama
hiyo kwa kuhusika na ghasia hizo.
Wakenya walikusanyika kwenye vituo mbali mbali
kushuhudia mjadala huo. Hoja kuu kwenye mjadala huo ilikuwa swala la ICC
ambalo wagombea wengine walitaka Uhuru kuelezea atakavyoongoza nchi
ikiwa atapatikana na hatia kwa makosa anayokabiliwa nayo.
Kenyatta alisema kuwa haoni kama kesi yake
katika mahakama ya ICC haitaathiri kwa vyovyote atakavyoongoza nchi
ikiwa atashinda uchaguzi huo.
Lakini mpinzani wake mkuu Raila Odinga, alipuuza
hilo akisema kuwa Uhuru atakuwa na wakati mgumu kuongoza nchi kupitia
kwa mtandao wa kijamii wa Skype wakati kesi yake ikisikilizwa Hague.
Wagombea wote walizungumzia swala la ukabila
wakisema ni moja ya changamoto kubwa katika uongozi wa nchi kwani tatizo
hilo limekita mizizi.
No comments:
Post a Comment