HARAKATI za kupanga safu za uongozi ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimehitimishwa usiku wa kuamkia leo baada ya
Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) kuchagua wajumbe wa Kamati Kuu
(CC).
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao cha
NEC jana, walioula kuingia katika chombo hicho kikuu cha uamuzi ndani ya
CCM ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim na
mawaziri kadhaa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
Dk Salim ambaye aligombea urais dhidi ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa 2005,
aliteuliwa jana kuwa mjumbe wa NEC na baadaye jina lake kupendekezwa
kuwa miongoni mwa waliopigiwa kura za kuwa wajumbe wa CC.
Makada 14 wa CCM, saba kutoka kila upande wa
muungano walipigiwa kura katika uchaguzi huo ambao matokeo yake
yalitangazwa usiku wa manane.
Kutoka Tanzania Bara, waliochaguliwa ni pamoja na
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa
Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa na
Mbunge wa Viti Maalum, Pindi Chana.
Kutoka Tanzania Zanzibar mbali na Dk Salim,
wengine ni Waziri wa Ulinzi, Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi.
Pia wamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano), Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa zamani wa Mawasiliano
na Uchukuzi, Dk Maua Abeid Daftari pamoja na Khadija Aboud. Wajumbe
hao wapya wanaunda Kamati Kuu pamoja na wengine wanaoingia kwa nyadhifa
zao.
Vigogo urais watoswa
Uteuzi wa makada
waliopigiwa kura uliwaweka kando vigogo ambao wamekuwa wakitajwa kuusaka
urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2015.
Miongoni mwa waliowekwa kando ni Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa na mawaziri waandamizi wawili katika Serikali ya
Rais Kikwete, Samuel Sitta (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Bernard
Membe (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).
Kadhalika, majina makubwa ndani ya chama hicho
kama vile January Makamba, Martin Shigela, Willison Mukama, Mohamed Seif
Khatib, Omar Yusufu Mzee na wengineo hayakuwamo kwenye orodha ya
waliopigiwa kura.
Baadhi ya makada walioanguka Balozi Ali Karume, Gwaride Jabu, Dk
Raphael Chegeni, Dk Cyril Chami, Michael Lekule
Laizer, Ramadhan Madabida, Hassan Wakasuvi, Dk Fenella Mukangara, Shamsa
Mwangunga na Said Mtanda.
No comments:
Post a Comment