WAFANYABIASHARA wa Kituo cha Mabasi Mwenge Da es
Salaam, wamelalamikia miundombinu mibovu na uchakavu wa nguzo za
Shirika la Umeme (Tanesco) kuwa chanzo cha ajali za moto zinazotokea
mara kwa mara.
Hayo yalibainishwa na wafanyabiashara wa kituo
hicho wakati mwandishi wa gazeti hili alipokuwa akifanya mahojiano na
baadhi yao kwenye kituo hicho ikiwa ni takribani siku saba tangu ajali
hiyo ilipotokea. Emmanuel Temba ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa
kituo hicho alisema, miundombinu ya shirika hilo ni mibovu licha ya kuwa
watu wanalipa bili za umeme kila mwisho wa mwezi lakini hakuna
mabadiliko yoyote katika sekta hiyo.
Temba alisema, shirika hilo linatakiwa
liwajibishwe ili liweze kuboresha miundombinu yake, lakini kinyume na
hapo ajali za moto zitaendelea kutokea na kusababisha hasara ya mali na
wakati mwingine watu kupoteza maisha.
“Naamini kuwa Tanesco wakifanya maboresha
kwenye nguzo chakavu na transfoma za umeme hakutakuwa na hitilafu za
umeme ambazo ndizo chanzo cha ajali za umeme,” alisema Temba.
Akizungumzia wafanyabiashara wenzake
waliopatwa na ajali hiyo, Ashura Muhamed alisema hadi kufikia jana
hakuna hata mmoja wao aliyerejea kwenye biashara kutokana na hasara
walizopata baada ya bidhaa zao kuteketea kwa moto.
Muhamed alisema,licha ya kuwa wanasubiri
matengenezo yafanyike kwenye maduka yaliyoteketea kwa moto, bado
wanachangamoto nyingine ya kuimarisha kipato kutokana na hasara
walizopata baada ya ajali hiyo.
“Ajali iliteketeza bidhaa nyingi na hivyo ni
vigumu kwa wao kuendelea na biashara kwa sasa labda hadi hapo
watakapoweza kuimarisha vipato vyao na kununua bidhaa nyingine kwa ajili
ya kuanza kuuza tena,” alisema
Hata hivyo, baada ya kufanya mawasiliano na
shirika hilo juhudi za kumpata afisa uhusino zilikwama, lakini tuliweza
kuwasiliana na Kaimu Mgurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alikanusha
habari hizo na kusema kuwa sio za kweli bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Ajali hiyo ilitokea Jumanne Februari 5, mwaka
huu kwenye kituo cha Mabasi cha Mwenge Dar es Salaam, ambapo maduka 19
ya kuuza bidhaa mbalimbali yaliteketea kwa moto na kusabababisha hasara
ambapo hadi sasa wafanyabiashara hao hawajatoa tamko.
No comments:
Post a Comment