Daladala
HALMASHAURI ya Manispaa ya Temeke, jijini Dar es
Salaam, ina mpango wa kupeleka operesheni usafi kwenye mabasi ya
daladala yanayotoa huduma ndani ya manispaa hiyo.
Hayo yalisemwa jana na Ofisa Uhusiano wa
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Joyce Msumba alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa habari hii kuhusu maendeleo ya operesheni ya kusafisha
manispaa hiyo.
Alisema mpango huo unatokana na kukithiri kwa
vitendo vya abiria wa mabasai hayo kutupa ovyo takataka hasa baada ya
kukosa mahali pa kuhifadhi takataka hizo ndani ya mabasi hayo.
“Tutawaagiza madereva ili waweke vifaa vya
kuhifadhi takataka ndani ya mabasi yao, ili kuepuka mtindo wa abiria
kutupa takataka ovyo,” alisema. Ofisa Uhusiano huyo alisema bila
matumizi ya nguvu na vitendo , Jiji la Dar es Salaam halitaweza kuwa
safi.
Msumba alisema halmashauri inalazimika kutumia mgambo ili kuhakikisha kuwa watu wanafanya usafi katika maeneo yao.
“Kuna mama lishe ambao hawazingatii usafi kabisa
katika maeneo yao ya biashara, unakuta mtu amefunga gunia chini kuna
maji machafu yanatiririka lakini hawajali,” alisema
Alisema hata
hivyo halmashauri itahakikisha kuwa hakuna watu watakofanya biashara za
vyakula kando kando ya barabara kuu zilizo kwenye manispaa hiyo.
“Lakini kuna watu wengine wana tabia ya
kutiririsha maji ya vyooni na kuyaelekezea kwenye mitaro jambo ambalo ni
hatari kiafya kwani linaweza kusababisha magonjwa ya milipuko kama
kipindupindu,” alisema.
Kwa kuonyesha kuwa wamedhamiria kufanya kile
wanachokisema, Msumba alifafanua kuwa wanawatoza faini kati ya Sh20,000
hadi 50,000 kwa wale wanaokiuka taratibu za usafi.
No comments:
Post a Comment