Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Dk Gervas Mbasa
SAKATA la wizi wa fedha katika akaunti za wateja
wa benki, sasa limeingia katika sura mpya baada ya Mbunge wa Biharamulo
Magharibi, Dk Gervas Mbasa (Chadema) naye kuibuka na kudai kuwa
ameibiwa Sh6 milioni kutoka kwenye akaunti yake.
Akizungumzia wizi huo, mbunge huyo alisema
fedha zake ziliibwa kwa nyakati tofauti kati ya Desemba 20 mwaka jana na
Januari 3, mwaka huu.
Alisema kitendo hicho kilifanywa na mtu mmoja
aliyempigia simu na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa
Makao Makuu ya Kampuni ya Airtel na kwamba alikuwa katika zoezi la
kuhakiki namba zote za zamani.
“Alinieleza kwamba kwa niaba ya Airtel yupo
katika zoezi la kuhakiki namba zote zilizosajiliwa zamani na yangu
ilikuwa ni ya miaka 10 na akaniuliza namba ya mwisho kuwasiliana na mtu
kupitia simu yangu. Nilimtajia namba ya mke wangu na baada ya maelezo
hayo aliniomba nisizime simu yangu wakati wakiwa wanashughulika na
kuisajili na kwamba muda wowote nitapatiwa maelekezo,” alieleza mbunge
huyo.
Kilichotokea baada ya muda ni kwamba simu
yangu, haikuweza kufanya kazi, hatua hiyo iliyonilazimisha kuwasiliana
na watoa huduma wa kampuni hiyo huko jimboni ili kujua tatizo ni nini,
lakini kila aliyejaribu kuirejesha katika mawasiliano alinijibu kuwa
haiwezekani mpaka makao makuu,” alisema Mbasa.
“Kila wakala wa Airtel niliyemfuata na
kumweleza kuwa simu yangu haifanyi kazi, alipoingia kwenye mtandao wao
kwa ajili ya kuirejeshea mawasiliano alinijibu kuwa hiyo haiwezekani
mpaka makao makuu ya kampuni hiyo,” alisema.
Mbunge huyo alisema majibu hayo yalimlazimisha
kutulia bila mawasiliano hadi Januari mwaka huu alipokwenda katika
Makao Makuu ya Aritel na kufanikiwa kuirejeshea simu yake mawasiliano.
Dk Mbasa alisema baadaye aligundua kuwa wakati
simu yake ikiwa imekosa mawasiliano watu hao walikuwa wakishughulikia
kuhamisha fedha zake kutoka katika akaunti yake.
Alisema Januari 6, mwaka huu alifanikiwa
kwenda Tawi la Benki ya NMB la Mazengo ambapo baada ya kuangalia salio
katika akaunti yake, alibaini kuwapo kwa wizi huo na baadaye
aliwasiliana na maofisa wa benki hiyo ambao walimthibitishia kuwa
ameibiwa.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, maofisa hao walimpatia fomu za
kujaza, ili kusitisha kutumia huduma ya `Sim Banking’ katika akaunti
yake.
Dk Mbasa alisema baadaye aliwasiliana na
meneja wa benki hiyo na kutakiwa kuandika maelezo ya wizi ikiwa ni
pamoja na kukabidhiwa kwa wataalamu wa masuala ya ufuatiliaji wa uhalifu
kwa njia ya mitandao.
Alisema baada ya kuangalia katika mtandao,
wataalamu hao walibaini kuwa fedha zake zilitolewa na wahusika katika
kipindi cha kati ya Desemba 20 mwaka jana na Januari 3, mwaka huu.
“Kwa mujibu wa mtandao wa Benki inaonyesha
fedha zangu zilitolewa kwa kutumia huduma ya `Sim Banking’ ya NMB Mobile
ambapo zilikuwa zikihamishwa kutoka katika akaunti yangu kwenda `Pesa
Faster Collection’ na kwa watu wengine wawili,” alifafanua.
Alisema kutokana na maelezo hayo ya NMB,
alilazimika kufungua jalada katika Kitengo cha Polisi cha Kupambana na
Wizi kwa Njia ya mtandao lakini, hadi sasa hakuna lolote lililofanyika.
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, David Misime alisema hana
kumbukumbu kuhusu madai ya mbunge huyo kuibiwa na kuomba muda ili
afuatilie kwa maofisa wake.
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Simu ya
Mkononi Airtel, Ally Maswanya alisema hakuna zoezi la uhakiki wa namba
lililoendeshwa na kampuni yake na kwamba anavyotambua kuna watu wahuni
ambao wamekuwa wakijifanya kuwa ni maofisa wa kampuni na kisha
kuziingilia namba za wateja wao.
No comments:
Post a Comment