Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi
MAOFISA wa Shirika la Upelelezi la Marekani
(FBI), wamekubali kufanya upelelezi wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi
yaliyotokea Zanzibar Februari 17, mwaka huu.
Kwa mujibu wa habari za kuaminika
zilizopatikana jana maofisa hao wako nchini na tayari wamekutana na
baadhi ya viongozi wa Serikali kwa ajili ya kuanza kazi hiyo.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa maofisa
hao walikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi
kwa ajili ya kuangalia ni namna gani watafanya shughuli zao katika
upelelezi huo.
Kutua kwa maofisa hao kumekuja baada ya kauli
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za rambirambi
baada ya mauaji ya Padri Mushi kuwa ameliagiza Jeshi la Polisi kutumia
nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama vya
hapa nchini na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika kufanya
uchunguzi wa mauaji hayo.
Pamoja na ushiriki wa FBI, pia Serikali
inazungumza na nchi nyingine rafiki ili kushirikiana nao katika
upelelezi ya matukio mengine ya mauaji ya hivi karibuni.
Taarifa zinaeleza kuwa maofisa wa Serikali
wamezungumza na taasisi za upelelezi za nchi tano ili kuongeza nguvu
katika kazi hiyo.
Taasisi nyingine inayotajwa kwamba huenda
ikashiriki katika uchunguzi huo ni Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai
ya Uingereza ya Scotland Yard.
Hatua hizi zinakuja baada ya Dk Nchimbi kutoa
tamko la Serikali, Jumapili iliyopita, akidai kuwa mauaji ya Padri Mushi
yalikuwa ya kigaidi hivyo Serikali itachukua hatua kali kuhakikisha
waliohusika wanakamatwa.
Haitakuwa mara ya kwanza kwa Serikali ya
Tanzania kushirikiana na asasi za kimataifa katika ku chunguza matukio
ya uhalifu na yale ya kigaidi.
Hii itakuwa mara ya pili kwa FBI kuja
nchini kufanya operesheni kubwa ya upelelezi. Mwaka 1998, walifika
kuchunguza kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani na kugundua ilikuwa kazi
ya Kundi la Al-Qaeda.
Pia mwaka 1984 walikuja wapelelezi kutoka Scotland Yard kuchunguza kuungua kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Pereira Ame Silima alithibitisha Serikali kuanza mazungumzo na mashirika
mbalimbali ya upelelezi duniani kwa ajili ya kushirikiana nayo
kuchunguza mauaji ya Padri Mushi.
Alisema tayari wameanza kufanya
mazungumzo na mashirika hayo kutoka nchi mbalimbali, lakini alisema ni
mapema mno kuyataja... “Ila
tukikamilisha kila kitu tutawaiteni na kuwaeleza
hatua tuliyofikia, ila tumeanza kufanya mazungumzo nayo. Kama unavyojua
Rais Kikwete alitoa agizo hilo, sisi tumeanza kulitekeleza.”
Waziri
Silima alisema kwanza wataanza kuchunguza mauaji ya Padri Mushi...
“Tutaanza kuchunguza kwanza chanzo cha mauaji haya ili tujue kila kitu.”
Watuhumiwa wakamatwa
Polisi Zanzibar inawashikilia watu kadhaa wakihusishwa na mauaji ya Padri Mushi.
“Tumekamata watu kadhaa kuhusiana na kifo cha
Padri na tunaendelea kuwahoji na wengine tutawaachia,” alisema Kamishna
wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa jana.
Kamishna Mussa hakutaka kutaja idadi ya watu waliowakamata hadi sasa na kuwahoji akisema: “Tunakamata na kuhoji na kuachia.”
Wananchi
a wa Zanzibar wamepunguza matembezi ya usiku tangu Jumapili wakihofia
kukamatwa na vyombo vya ulinzi ambavyo vimeimarisha ulinzi kutokana na
tukio hilo.
Jimbo la Bububu ambalo ndiko marehemu
alikouawa linaongoza kwa wananchi kujifungia mapema majumbani mwao kwa
hofu hiyo ya kukumbwa na mikono ya maofisa usalama.
Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el
Raas, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar limefungwa tangu Jumapili baada ya
Padre Mushi kuuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akienda kuongoza ibada
katika kanisa hilo.
Padri Mushi aliyekuwa kiongozi katika Kanisa la
Minara Miwili, alizikwa Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja kwenye makaburi
ya viongozi wa kanisa hilo juzi.
Kuuawa kwake ni tukio la tatu kubwa la
kushambuliwa kwa viongozi wa dini baada ya kumwagiwa tindikali kwa
Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga na kushambuliwa kwa
risasi Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki mwaka jana.
Aidha, viti vya Kanisa la Sloam liliopo
Kianga, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja vilichomwa moto na watu
wasiojulikana alfajiri ya Jumanne iliyopita.
No comments:
Post a Comment