Lowassa
WAKATI Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
akiinyooshea kidole Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za
kata, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema
hatajiuzulu ng’o kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Bavicha), nalo limetishia kuitisha maandamano ya nchi nzima
kwa kushirikisha wanafunzi wote waliopata sifuri ikiwa waziri huyo
hatajiuzulu.
Taifa limeshikwa na mshtuko kutokana na
matokeo hayo ambayo yanaonyesha kuwa asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya
mtihani huo mwaka jana, walipata sifuri.
Dk Kawambwa
Akizungumza
jana katika uzinduzi wa Mpango Maalumu wa Mafunzo ya Kompyuta katika
Shule ya Msingi ya Majengo wilayani Bagamoyo, Dk Kawambwa alisema hawezi
kuachia ngazi kwa shinikizo la wanasiasa.
Alisema yeye si wa kulaumiwa kutokana na
wanafunzi hao kufanya vibaya kwenye mtihani wa kidato cha nne na kwamba
wanaosema waziri anapaswa kujiuzulu hawana hoja za msingi zaidi ya
kutaka kujipatia umaarufu kwa kudandia hoja zinazokuwapo kwa wakati
husika.
“Unajua katika mfumo wa vyama vingi, kila linapotokea jambo
baya basi wanaona dawa ni kiongozi mhusika kung’oka. Unapozungumza
waziri kujiuzulu hiyo ni lugha ya kisiasa lakini hata akijiuzulu inakuwa
bado tatizo halijaweza kupatiwa ufumbuzi,” alisema.
Dk Kawambwa alisema hata Serikali
haijafurahishwa na matokeo hayo mabaya na kushauri njia nzuri ni
kutafuta dawa ya kukabiliana na tatizo la wanafunzi kufeli huku akiahidi
kuwa wizara yake inaangalia tatizo hilo kwa karibu zaidi ili kujua
chanzo chake.
Alisema amesikitika kuona hata shule ambazo
zilikuwa zinategemewa kufanya vizuri zikiwamo za seminari, watu binafsi
na kongwe za Serikali, nazo zimefanya vibaya.
Aliunga mkono maoni ya kutaka mfumo mzima wa elimu nchini uangaliwe upya kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu.
Lowassa
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Lowassa alisema matokeo hayo ni aibu kwa
taifa na kuilaumu Serikali kwa kuzitelekeza shule za sekondari za kata.
Alisema taifa kwa sasa linazalisha wabeba kuni na maji na siyo wasomi ambao wanaweza kushindana kwenye soko la ajira.
Alisema sekondari za kata ambazo zilianzishwa
chini ya usimamizi wake akiwa Waziri Mkuu, zilikuwa ukombozi kwa
Watanzania wengi wa kipato cha kawaida na ndiyo sababu waliitikia wito
kwa kuchangia ujenzi, hatua ambayo alisema ilimpa faraja kubwa.
“Serikali tuliahidi kuzikamilisha shule hizo
kwa kuzijengea maabara na kuhakikisha zina walimu. Ni wajibu wake
kutimiza. Mimi ndiyo maana hata kwenye Katiba Mpya nilipendekeza
uwezekano wa elimu ya sekondari kuwa bure, elimu ni kama mapigo ya moyo
ya taifa ukiona hayaendi vyema lazima ujiulize,” alisema.
Lowassa, ambaye alijiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008, alisema tangu aondoke madarakani, shule hizo nazo zimetelekezwa.
Alimwomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua
za makusudi, ikiwa ni pamoja na kuunda tume ili ichunguze kwa makini
kiini cha matokeo hayo mabaya.
“Matokeo hayo ni aibu kwa taifa, walimu,
wazazi na wanafunzi wenyewe. Namwomba kwa dhati Rais afanye kitu cha
ziada, natambua mchango wa juhudi zake katika sekta nyingine ikiwamo
ujenzi wa barabara nchini lakini elimu ndiyo iwe ya kwanza,” alisema.
Alitaka ufike wakati nchi iamue kuwekeza
katika elimu tofauti na ilivyo sasa kwa Tanzania kuwa nchi inayotenga
fedha kidogo zaidi katika sekta hiyo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC).Alisema Tanzania inatumia asilimia 1.4 ya bajeti yake, Kenya asilimia saba, Rwanda 5.8%, Uganda 4.8% na Burundi ni 3.2%.
Bavicha na maandamano
Bavicha
imetishia kuitisha maandamano hayo yatakayowahusisha wanafunzi wote
waliofeli ikiwa Waziri Kawambwa hatajiuzulu ndani ya siku 14 kama
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alivyomtaka Jumanne wiki hii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es
Salaam jana, Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratius Munishi alisema
wameshaanza kuwajulisha viongozi wa mikoa na wilaya kuhusu taratibu zote
za kuandaa maandamano hayo.
Alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni
kutaka kushinikiza pia Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shule za
Sekondari wa Wizara ya Elimu kujiuzulu ili kupisha wengine
watakaosimamia kikamilifu mabadiliko ya mfumo wa elimu nchini.
“Tunaitaka pia Serikali ya CCM ieleze hatima
ya maisha ya vijana waliofelishwa na mfumo mbovu wa elimu,” alisema na
kuongeza kuwa kuna wanafunzi 800,000 waliofeli ambao wako mitaani tangu
tatizo la matokeo ya kidato cha nne lilipoanza mwaka 2009.
Alisema Serikali ya CCM ilikuwa na lengo la ufaulu
wa asilimia 70 kwa kidato cha nne tangu mwaka 2009 lakini imekuwa
kinyume chake.
“Ukweli usiofichika ni kuwa Serikali ya CCM
haiwezi kufikia lengo la kuwa na taifa lililoelimika ifikapo 2025 kama
ilivyobainisha kwenye dira yake ‘Vision 2025’ na badala yake itajenga
taifa la watu mbumbumbu kwa wakati huo,” alisema.
No comments:
Post a Comment