Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeingilia kati
wizi wa fedha kwa kutumia mashine za kutolea fedha (ATM), ambao umeibua
hofu kubwa katika sekta ya benki nchini.
Kutokana na wizi huo kukithiri katika baadhi
ya benki, wafanyabiashara na wananchi wameanza kujipanga kuondoa fedha
zao katika akaunti.
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu
alizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki kwamba wameziagiza benki
kuweka kifaa cha umeme (electronic chip) kwenye kadi zao za ATM ambazo
si rahisi kughushi.
“Wizi kama huo unatokea wakati mtu anaweka
namba za siri kwenye ATM kwani kuna watu huweka kamera ambazo husoma na
namba hizo kufanikiwa kuzipata kisha kufanya wizi ,” alisema Profesa
Ndullu.
Alisema kuwa kutokana na wizi kukithiri
wamezitaka benki zote kuweka mifuniko katika eneo la namba za siri ili
wezi wanaoweka kamera ili kuzinasa wakati mtu anatoa fedha washindwe
kufanya hivyo.
Profesa Ndullu alisema wanafuatilia mfumo wa
utendaji wa benki ili kuondokana na tatizo hilo ambalo hivi sasa
limeibua mijadala na hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Benki kubwa nchini zimekumbwa na mtikisiko wa
wizi wa fedha kwa kadi za ATM, ambao umeongezeka kwa kasi kiasi cha
kufanya wananchi wengi kuhifadhi fedha zao kwenye mitandao ya makampuni
mbalimbali ya simu za mikononi ambayo hata hivyo ripoti zimekuwa
zikieleza kuwa nako usalama wake si wa kiwango cha juu.
Baadhi ya benki ambazo zimekumbwa na matukio
hayo zimekuwa zikisita kutoa taarifa kueleza sababu za kushindwa kuzuia
wizi huo na badala yake zimekaa kimya kuhofia kupoteza wateja.
Kukua kwa teknolojia za kifedha ambako
kumerahisisha ufanisi wa matumizi na utunzaji wa fedha, sasa kunaonekana
kugeuka na kuwa balaa kutokana na kuibuka kwa wizi mkubwa mahala
zinakohifadhiwa kwenye akaunti za wateja kwa kutumia njia ya mtandao.
Taarifa za wizi huo zilianza kurindima mwezi
Machi, 2010, ambako kiasi cha mabilioni ziliibwa kupitia katika mashine
za ATM huku kati ya kiasi hicho jumla ya Sh360 milioni zikihusisha benki
moja nchini.
Hata hivyo, mwaka huo watu wanne walikamatwa
baada ya kuripotiwa wizi huo mkubwa. Sambamba na kukamatwa kwa watu hao,
pia alikamatwa mfanyabiashara mmoja aliyekuwa akifanya jaribio la kuiba
kimafia Sh221 milioni kutoka benki ya NBC.
Wimbi la wizi huo limeibuka tena katika
kipindi cha Oktoba 2012 hadi Februari 2013 na inakadiriwa kuwa jumla ya
kiasi cha Sh700 milioni kimeibwa katika benki mbalimbali kwa nyakati
tofauti.
Hivi karibuni, Polisi mkoani Mwanza kwa kusaidiana na maofisa wa
Benki ya NMB, iliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa kuiba kiasi
cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti.
Watuhumiwa hao walinaswa baada ya kuwekewa
mtego na maofisa wa benki pamoja na polisi usiku wa Februari 10, mwaka
huu. Mtuhumiwa mmoja alinaswa akichukua fedha katika mashine ya ATM ya
NMB kwenye Tawi la PPF Plaza.
Baada ya kunaswa kwa mtuhumiwa huyo, alisaidia
kuwaelekeza polisi walipo wenzake, ambao walikutwa katika hoteli moja
jijini Mwanza wakiwa wamejipumzisha.
No comments:
Post a Comment