Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana. Kulia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu.
Mvutano uliopo hivi sasa kati ya Chadema na
Bunge ulianza Februari 4 katika kikao cha Bunge mjini Dodoma baada ya
wabunge wa Chadema kupinga msimamo wa kiti cha Spika wakieleza
unapendelea
Boniface Meena na Mussa Juma, Mwananchi
Kutokana
na mvutano ambao umekuwapo mara kwa mara kati ya Chadema na Spika wa
Bunge, Anne Makinda, chama hicho kimemkumbuka aliyekuwa Spika wa Bunge
la 10, Samuel Sitta kikieleza kuwa alikuwa hapindishi sheria na kanuni
za Bunge na ndiyo maana lilikuwa limetulia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana
kuhusu wabunge wa chama hicho kutakiwa kuhojiwa na Kamati ya Haki, Kinga
na Maadili ya Bunge, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
Spika Makinda amekuwa akipindisha kanuni na ndiyo maana kumekuwa hakuna
utulivu bungeni.
“Spika Sitta aliyekuwepo kabla ya Makinda
alikuwa hapindishi sheria na alikuwa anajirekebisha pale anapokosea na
tulikuwa tukishauriana kwamba asijihusishe na mambo ya vyama,” alisema
Dk Slaa.
Alisema Sitta, ambaye hivi sasa ni Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikuwa hafuati mambo ya vyama kwa kuwa
alitakiwa kuwa ni mtu ambaye hapendelei upande wowote. Sitta, ambaye
alikuwa Spika kuanzia mwaka 2005-2010, alikuwa anajinadi kwa kuendesha
Bunge kwa spidi na viwango.
“Makinda aachane na ushabiki wa CCM kwani
anajua kabisa kanuni ya nane inamtaka Spika asifungamane na upande
wowote hivyo aache kufanya hivyo,” alisema Dk Slaa.
Alisema ni muhimu Spika akawaeleza kimaandishi
amepata wapi mamlaka ya kuruhusu kamati iendelee wakati zote
zilivunjika rasmi katika Bunge lililopita.
“Spika kama hajui kanuni aende shule kujifunza kuliko kututia aibu, wanasheria, wabunge wamsaidie ili aweze kuelewa.”
Dk Slaa alisema katika mabunge ya
kidemokrasia, kupongeza ni jambo halali na kuzomea pia ni jambo halali
hivyo kitendo cha wabunge wao kuzomea ni sawa kwa kuwa ni njia yao ya
kufikisha ujumbe. Akizungumzia suala la wabunge wake kuhojiwa na kamati
hiyo ya Bunge, alisema hawatakwenda kuhojiwa na kamati hiyo na kama
Bunge litaamua kuwafukuza lifanye hivyo ili wananchi waelewe.
“Hawawezi kwenda kuhojiwa na kamati ambayo
haipo kisheria, nilipokuwepo bungeni nilishiriki kuandaa kanuni hizi za
Bunge, Spika hana mamlaka anayojipa ya kuongeza muda wa kamati, hivyo
aache kulidhoofisha Bunge na badala yake alisaidie,” alisema Dk Slaa.
Akizungumzia suala hilo, Mnadhimu Mkuu wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema anashangazwa na
Naibu Spika, Job Ndugai kusema kuwa kuna kamati ambazo huwa zinaendelea
wakati nyingine zinapokuwa zimemaliza muda wake.
Lema aitisha maandamano
Mbunge wa Jimbo la
Arusha Mjini, Godbless Lema, ametangaza kuandaa maandamano makubwa
yatakayoshirikisha wanawake na watoto katika Jiji la Arusha ili
kushinikiza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (AUWSA) kuwasambazia
maji.
Akizungumza jana, Lema alisema ameamua kuandaa
maandamano hayo ya kudai maji kwani kwa zaidi ya miezi sita sasa
asilimia 70 ya wakazi wa Jiji la Arusha hawapati maji safi.
“Nimewaandikia barua AUWSA wiki mbili sasa
nikiwataka wanipe mipango yao ya muda mfupi na mrefu ya kuondoa tatizo
la maji Arusha, kwani mimi kama mbunge ninaweza kushirikiana nao
kupunguza tatizo hili, lakini hawajajibu sasa tutawashinikiza kwa nguvu
wa umma,” alisema Lema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa AUWSA, Mhandisi Ruth Koya hakupatikana
kuelezea kama amepokea barua hiyo baada ya kutopatikana ofisini, pia
simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani
No comments:
Post a Comment