Tume ya uchaguzi ingali inatangaza matokeo ya urais eneo bunge moja baada ya nyingine
Mahakama ya juu nchini Kenya hii
leo itatoa uamuzi ikiwa ina uwezo wa kusikiliza kesi iliyowasilishwa
kwake na makundi ya kijamii yakitaka tume huru ya uchaguzi nchini Kenya
kusitisha shughuli ya kuhesabu kura za urais inayoendelea katika ukumbi
wa Bomas.
Makundi hayo yanadai kuwa tume inakwenda kinyume
na katiba ambayo ambayo inasema kura zinapaswa kuhesabiwa kwa njia ya
elektroniki.
Pia Muungano wa Cord wake mmoja wa
wagombea wa urais Raila Odinga umedai kuwa tume hiyo inafanya hujuma
katika shughuli ya kujumlisha kura za urais katika ukumbi wa Bomas.
Hapo jana Muungano wa CORD ulielezea malalamishi
kuhusu shughuli yakujumlisha kura za urais na kusema hauna imani nayo
kwani ina ushahidi kuwa hujuma imefanyika wakidai wizi wa kura.
Pia wanadai kuwa katika baadhi ya maeneo, kura zilizopigwa ni nyingi kuliko idadi ya wapiga kura waliosajiliwa.
Madai haya waliyatoa hapo jana ingawa mkuu wa
tume ya uchaguzi aliyakanusha vikali na kusema hakuna mahala popote
ambapo wameshuhudia matokeo kuhujumiwa.
Chama hicho pia kilidai kuwa baadhi ya matokeo yalikuwa juu ikilinganishwa na idfadi ya wapiga kura.
Na kwa hilo, mkuu wa tume ya uchaguzi Isaack Hassan pia alikanusha vikali akisema hawajapata matokeo kama hayo.
Tume hiyo imesisitiza kuwa shughuli ya kuyahakiki matokeo inafanywa mbele ya maajenti wa vyama vyote.
Tume ya uchaguzi ingali inaendelea na shughuli ya kujumlisha kura za urais
Wakati huohuo tume hiyo imekiri kuwa kulikuwa na
tatizo la mtambo wake wa kupeperusha matangazo ikisema kuwa ilikuwa
inaongeza mara nane kura zilizoharibika.
Washika dau wengi walieleza wasiwasi kuhusu
idadi kubwa ya kura zilizoonekana kuharibika kwani zilikuwa kura zaidi
ya laki tatu. Lakini kufikia sasa zimepungua na kufika themanini.
Mkuu wa tume hiyo, Issack Hassan alisema kuwa komputa ilikuwa inaongeza idadi ya kura zilizoharibika kwa mara nane.
Shughuli ya kukusanya matokeo ilianza upya kwa
mikono kufuatia matatizo haya lakini Uhuru Kenyatta angali anaongoza
dhidi ya Raila Odinga.
"kulikuwa na makosa kwa namna ambavyo programu ya komputa ilikuwa imeundwa, '' alisema Hassan.
''Kwa kura zote zilizoharibika kwa kila mgombea
zilikuwa zinaongezeka mara nane ,'' aliongeza kusema mwenyekiti wa tume
ya uchaguzi.
No comments:
Post a Comment