Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen-Kijo Bisimba
Dar na Dodoma. Wakati Spika wa
Bunge, Anne Makinda akitangaza kuanza kuwatoa nje ya Ukumbi wa Bunge
wanaotumia lugha za matusi, baadhi ya wanasiasa, wanaharakati na
wanazuoni wamesema wabunge wanatumia mamilioni ya kodi za wananchi,
hivyo wanatakiwa kuheshimu hilo na kujikita zaidi kuzungumzia masuala ya
msingi.
Juzi Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), Juma Nkamia na
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliwapiga vijembe viongozi
wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakisema kwamba
kuna wabunge ambao wana “mimba zisizotarajiwa bungeni.”
Kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu
(Chadema), Paulina Gekul akitumia Kanuni ya 68 (7), alikilaumu kiti cha
Spika kwa kukaa kimya wakati wabunge hao wanatukana bungeni.
Pia Moses Machali (Kasulu Mjini-NCCR-Mageuzi) na
Magdalena Sakaya (Viti Maalumu-CUF) waliomba mwongozo wa Spika wakitumia
Kanuni ya 64 inayozuia lugha za kuudhi bungeni.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti Profesa
Simon Mbilinyi alisema, “Wabunge hawa wanatumia vibaya fedha za
walipakodi ambao wanaishi maisha duni, hawakuchaguliwa kwa ajili ya
kupigana vijembe bungeni.”
Mwenyekiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Helen-Kijo Bisimba alisema, “Inaonekana hawajui cha kufanya
wala kilichowapeleka bungeni.”
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
(CWT), Ezekiel Oluoch alisema kuwa moja ya mambo yaliyotakiwa kujadiliwa
na wabunge hao ni pamoja na madai ya walimu ya muda mrefu.
“Walimu wanaidai Serikali Sh25 bilioni, kuna suala
la kutokuwapo kwa mitalaa, haya yote hawayaoni wanaishia kutupiana
vijembe tu,” alisema Oluoch.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Nchini (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema tatizo siyo wabunge, bali ni Spika, Makinda.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper
Ngowi alisema wabunge wanatakiwa kutambua kuwa wapo bungeni kwa fedha
za wananchi, hivyo wanatakiwa kulipa fadhila.
“Wananchi wanawategemea wabunge wasimamie haki na
usawa na kujenga hoja za kutetea masilahi yao,naona 2015 ndiyo uwe muda
wa wananchi kuchagua anayewafaa ,” alisema Profesa Ngowi.
Makinda kuwaitia polisi
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema iko haja ya kuwatenga na wanaotaka kutukanane na wale wastaarabu .
Alisema kitendo cha wabunge kujadili matusi huku
wengine wakishangilia, kinaonyesha ni namna gani ambavyo watu hawako
makini ndani ya jengo hili. Spika Makinda alitoa kauli hiyo jana asubuhi
bungeni.
No comments:
Post a Comment