Ripoti ya kuteswa Kibanda bado giza nene

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.

Kitendawili cha nani aliyehusika kumteka na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, zaidi ya mwezi sasa kimekuwa kigumu kuteguliwa, baada ya Jeshi la Polisi kutamka kwamba, upelelezi wa sakata hilo bado haujakamilika.

Kutokana na hali hiyo, jeshi hilo limevitaka vyombo vya habari na wananchi kwa jumla kusubiri hadi hapo upelelezi juu ya sakata hilo unaofanywa na timu maalum ya wapelelezi wake utakapokamilika.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Ofisa Mwandamizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Hussein Nassoro, alipozungumza na NIPASHE, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.

Nassoro alitoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku 10 tangu Kaimu DCI, Isaya Mngulu, kuahidi kwamba ripoti ambayo ingewataja watuhumiwa wote waliohusika na sakata hilo, ingewekwa hadharani kati ya juzi, jana au leo.

Mngulu aliondoka nchini juzi usiku kwenda nchini Ufaransa kikazi.

“Upelelezi kuhusu suala hilo (la kutekwa na kuteswa Kibanda) unaendelea kufanyika. Na mara tu uchunguzi utakapokamilika vyombo vya habari na wananchi watafahamishwa. Tunaomba tuendelee kuvuta subira,” alisema Nassoro.

Wasiwasi wa ripoti hiyo kutowekwa hadharani kama ilivyoahidiwa na Mngulu Aprili 8, mwaka huu, ulizuka baada ya Kaimu huyo wa DCI juzi kubadili ahadi yake kwa kuliambia NIPASHE kwamba, asingeweza kuahidi kwamba, ingetolewa jana kwa kuwa sakata hilo bado linaendelea kupelelezwa.

Ahadi ya kuweka hadharani ripoti hiyo Aprili 15 au 16 au 17, mwaka huu, ilitolewa na Mngulu wakati akihojiwa katika kipindi cha ‘Kumepambazuka’ kinachorushwa hewani na Radio One Stereo.

Alisema ripoti hiyo ndiyo itakayobainisha kama kuna watu wanaostahili kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na sakata hilo au la.

“Hapo ndipo itakapojulikana kama kuna washtakiwa au hakuna washtakiwa,” alisema Mngulu.

Alisema miongoni mwa watu waliohojiwa katika upelelezi uliofanywa na timu hiyo, ni pamoja na Kibanda mwenyewe.

Akijibu swali kwa nini upelelezi wa sakata hilo umechukua muda mrefu, Mngulu alisema hakuna muda maalum uliowekwa na sheria wa kupeleleza jambo. Kutokana na hali hiyo, alisema upelelezi unaweza kuchukua hata miaka 10 na zaidi.

Mngulu ambaye alizungumza kwa ufundi na kwa tahadhari kubwa katika mahojiano hayo, alisema hata katika kumsaka Osama bin Laden, ilichukua zaidi ya miaka 10 ndipo akanaswa. Alisema sheria, kanuni na taratibu za upelelezi haziruhusu kueleza mwenendo, mbinu na maendeleo ya upelelezi wakati kazi hiyo inapokuwa inafanyika.

Hivyo, akawataka Watanzania kuwa wastahimilivu na wenye subira hadi upelelezi huo utakapokamilika na ripoti hiyo kutolewa.

Kibanda alivamiwa na watu ambao hawajafahamika wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu.

Katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto.

Hali hiyo ilisababisha Kibanda kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baadaye katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa Afrika Kusini ambako anaendelea na matibabu zaidi. 

Kufuatia tukio hilo, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, Advera Nsenso, alikaririwa akisema Mkuu wa Jeshi hilo nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, ameunda timu ya wapelelezi wazoefu kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kuwabaini waliohusika na uhalifu huo na kuwatia mbaroni mara moja.

Timu hiyo ya makachero wanne kutoka makao makuu ya polisi iliunganisha nguvu na makachero wa Jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Hadi kufikia jana, hakukuwa na taarifa zozote za kukamatwa mtu kuhusiana na tukio hilo.

Habari ambazo NIPASHE inazo, kigogo mmoja wa polisi alikwenda Afrika Kusini kumhoji Kibanda ikiwa ni pamoja na kuchukua maelezo yake juu ya mkasa mzima wa kufanyiwa unyama wa kutisha unaofanana na ule aliofanyiwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.

No comments:

Post a Comment