Atupa kichanga

Na John Banda, Dodoma

JESHI la polisi mkaoani Dodoma linamshikilia Mwanamke mmoja kwa kosa la kumtumbukiza mtoto chooni akiwa hospitali ya mkoa alikopelekwa kujifungua.

Tukio la kukamatwa kwa mwanamke huyo aliyekuwa amepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoani hapa baada ya kushikwa na uchungu wa kujifungua lilitokea majira ya saa tisa usiku.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Damas Nyanda Alimtaja mwanamke huyo kuwa anaitwa Sinsia Laurent 28 msandawe mkazi wa uhindini mjini hapa.

Nyanda alisema baada ya kufikishwa hospitalini aliomba kwenda chooni kujisaidia na baadae manesi walibaini kulikuwa na mwili wa kichanga muda mfupi baada  ya mtuhumiwa huyo kutoka chooni.

‘’tulipokea taarifa muda huo na tulipofika tulikuta mwili wa kichanga cha jinsia ya kiume ukiwa nje wakati kichwa kikiwa tayali kimesukumwa ndani ya choo hicho tulipomtoa alikuwa tayali ameshafariki’’, alisema Nyanda.

Aidha nyanda alisema wanaendelea kumshikilia mwanamke huyo  na uchunguzi utakakamilika atafikishwa mahakamani.    

Kwa upande wake Leah aliyempeleka hospilini hapo ambae ni mfanyakazi mwenzie katika baa ya CDA Clab iliyopo Uhindini alisema mtuhumiwa huyo siyo mkweli kwa kutoweka wazi kuwa mimba yake ilikuwa na miezi mingapi maana wao waliambiwa ilikwa na miezi 5.

Aliongeza kuwa kitendo hicho alichokifanya Mwenzao ni cha kinyama na hakikustahili kufanywa katika nyakati tulizonazo maana kuna njia nyingi za kuzuia mimba kama anakuwa hayuko tayali kupata mtoto.

Unyama Kenya : Waliouawa na magaidi wafikia 69

Baadhi ya raia, waliokuwa ndani ya jengo hilo wakitoka nje kwa hofu kubwa jana,


Bado jengo hilo limezingirwa na wanajeshi, kuhakikisha magaidi hao hawatoki nje kuhatarisha usalama wa wananchi.

Nairobi. Magaidi wanaokadiriwa kuwa kati ya 10 na 15 wamelitikisa Jiji la Nairobi kwa siku mbili mfululizo baada ya kuteka jengo kubwa la biashara la Westgate lililopo Westlands na kuua watu wapatao 69 hadi leo asubuhi.

Magaidi hao walivamia jengo hilo juzi saa tano asubuhi na hadi jana, jitihada za kuwadhibiti zilikuwa hazijafanikiwa. Zaidi ya watu 1,000 wameokolewa na wengine zaidi ya 170 wamejeruhiwa.

Tukio hilo limesababisha shughuli mbalimbali katika Jiji la Nairobi kusimama na hata maduka mengine makubwa ya Nakumatt kufungwa, hivyo kusababisha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kuwa shida kwa wakazi wengi wa Nairobi.

Wakazi wengi wa eneo la Westlands jana walikwama kufika katika maeneo yao na watu wengi waliokuwa kwenye jengo hilo waliacha magari yao na kukimbia huku na huko ili kujiokoa huku vyombo vya usalama vikiwataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo.

Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia kupambana nao.

Risasi zimekuwa zikisikika usiku kucha na watu zaidi wameendelea kuuawa huku Serikali ikisema mateka wanaodaiwa kuwepo ndani ya jengo hilo wakiwa chini ya magaidi hao ni 30.

Jengo hilo limezingirwa na vyombo vya usalama vya ndani na nje ya Kenya vikiongozwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya pamoja Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), David Kimaiyo, ambaye amekuwa akitoa taarifa mbalimbali za tukio hilo kupitia account yake ya Tweeter ili kuhakikisha vyombo vya habari na jamii vinajua kinachoendelea.

Pia Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitoa taarifa kupitia mitandao yake, huku televisheni zote za Kenya zikirusha tukio hilo moja kwa moja tangu lilipotokea juzi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku akizungumza na vyombo vya habari alisema watu 69 waliouawa ni pamoja na raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali. Hata hivyo, alisema haijajulikana ni wangapi na wanatoka nchi gani haswa.

Canada imethibitisha kuwa raia wake wawili wameuawa kwenye tuko hilo, pia raia wawili wa Ufaransa nao wameuawa.

Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na tukio hilo ambalo ni kubwa kutokea Kenya tangu ubalozi wa Marekani ulipolipuliwa mwaka 1998 jijini Nairobi.

 

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI NOVEMBA 23

.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

Ubakaji India : Aliyemtetea mbakaji kufutiwa leseni

Baadhi ya waandamanaji wakiandamana kupinga vitendo vya ubakaji.


Tofauti na Tanzania, nchini India Serikali inaonekana kuwawajibisha ipasavyo wenye kuendesha vitendo vichafu vikiwamo vya ubakaji.

Lilivyo kubwa tatizo la ubakaji nchini India, ni sawa na hapa kwetu Tanzania lilivyo la dawa za kulevya. Hata hivyo, tofauti kubwa ni namna viongozi wanavyotoa uamuzi kwa wenye kutenda maovu. Wiki hii nchi hiyo imetoa hukumu ambayo imetoa matumaini kwa wananchi wake.

Mfagizi,  Akshay Thakur, Mwalimu wa Mazoezi,  Vinay Sharma, Muuza Matunda, Pawan Gupta na Mukesh Singh walihukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya kubaka, kuua na kula njama za kupoteza ushahidi.

Mahakama iliwahukumu wote wanne kunyongwa na mmoja ambaye alikuwa chini ya umri wa miaka 18, mwezi uliopita alihukumiwa kifungo maalumu cha miaka mitatu.

Hata hivyo wakati hukumu hiyo ikiwa katika hatua za utekelezaji, wakili, AP Singh aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa wawili kati ya hao huenda akafutiwa leseni yake.

Singh ameingia matatani baada ya kutoa kauli ambayo imewakera mawakili wenzake na kumwamuru aombe msamaha na iwapo hata fanya hivyo atafutiwa leseni yake.

Wakili huyo baada ya kusikia hukumu hiyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mwenye makosa katika kesi hiyo ni binti huyo ambaye alikuwa akitembea usiku.

“Binti yangu akitembea usiku kama huyu, nitamnyonga mbele za watu, tunatakiwa tuwafundishe adabu mabinti zetu ili wasipate mabalaa kama haya, tukio hili liwe fundisho,” anasema Singh.

Umoja wa Wanasheria nchini India, The Delhi Bar Council (DBC) umemtaka Singh kuomba msamaha kwa jamii na familia ya binti huyo kwa kuwa kama mwanasheria alipaswa kusimamia haki.

Katibu wa umoja huo, Murari Tiwari amesema Singh anapaswa kuomba radhi kwani kitendo chake cha kukubali kuwatetea watuhumiwa wa ubakaji na kauli yake, vinashusha hadhi yake.

Hata hivyo Singh amesema anasimamia kauli yake na anajivunia kuwa mmoja wa watetezi wa vijana hao. Ameongeza kuwa anasubiri kufutiwa leseni naye atachukua hatua nyingine kupigania haki yake kama wakili.

Shambulio la kutisha

Binti wa miaka 22 akiwa na mpenzi wake walitekwa baada ya kupanda basi walilokuwemo wabakaji hao. Walikuwa wakitokea kuangalia sinema, wakalisimamisha basi hilo.

Mwanamume ambaye alinusurika katika tukio hilo anasema baada ya kuwateka waliwapiga , kuwang’ata kwa meno na kisha kuingiza chuma katika sehemu za siri za mwanamke huyo.

Baadaye waliwatupa kandokando ya barabara na wao kutokomea. Walipoamka walijikuta hospitalini lakini hali ya mwanamke ilikuwa mbaya zaidi na alihitaji matibabu ya hali ya juu. Alipelekwa nchini Indonesia hata hivyo hakupona  na kufariki dunia wiki mbili baadaye. Nchini India kuna zaidi ya kesi 1,098 za ubakaji.

Ingawa familia za watuhumiwa zinasema Serikali imewatumia vijana hao kama njia ya kuwaridhisha raia wake, lakini vipimo vya vinasaba (DNA) katika alama za meno zinaonyesha ni za vijana hao. Hata mwanamume aliyenusurika katika tukio hilo anathibitisha kuwa washambuliaji ni vijana hao sita.

“Binti yangu amepata haki leo, tumefurahishwa sana na hukumu hii,” anasema baba wa binti aliyefariki katika tukio hilo.

Wakati hukumu hiyo ikisomwa, baba wa binti huyo alikuwa amekaa chini  amejiinamia huku akibubujikwa machozi lakini ghafla aliibuka na kuruka juu baada ya kusikia wamehukumiwa kunyongwa.

Anasema tangu binti yake aliposhambuliwa, alibatizwa jina la Nirbhaya ambayo maana yake ni Isiyo na Woga.

Nirbhaya amekuwa nembo ya wanawake ambao hushambuliwa kila baada ya dakika 21. Nchini India matukio ya ubakaji, udhalilishaji na matukio ya kumwagiwa tindikali hutokea kila baada ya dakika 21.

Hukumu hiyo itapelekwa mahakama kuu ya nchi hiyo na majaji wawili wataiangalia na kuipitisha au kuifuta adhabu hiyo.Hata hivyo utekelezaji wake unaweza kuchukua miaka mingi.

Tangu kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, mmoja wa watuhumiwa, Ram Sigh alijinyonga akiwa katika chumba chake gerezani Machi mwaka huu.

Hata hivyo hali ya mambo hapa nchini inaonekana kuwa tofauti, ni suala la kawaida kuona mawakili wakitetea hata wauza dawa za kulevya au watu wengine ambao wanaonekana wazi kufanya maovu yenye ushahidi kwa jamii.

Ni wakati wa Watanzania kuweka masilahi ya taifa mbele kwa kupigana vilivyo na watu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wanachangia kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

 Makala haya yameandikwa na Julieth Kulangwa kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari.

Bagamoyo na maeneo ya kihistoria yasiyojulikana

Sehemu ya lango la Mji wa Bagamoyo, wakati wa ukoloni.


Siku chache zilizopita nilitembelea Kitongoji cha Magomeni, mjini Bagamoyo, katika kitongoji hicho nilipiga picha vipande vya nguzo ambayo ni mabaki ya lango la mji huo.

Dereva wa bodaboda aliyenipeleka hapo nilimuuliza kama anaelewa chochote kuhusu kuta hizo mbili, lakini cha ajabu alisema hajui licha ya kuishi  Bagamoyo miaka mingi.

Baada ya hapo nilikutana na dada ambaye anasema amezaliwa na kuishi eneo la Magomeni, lakini hajui maana ya kuta hizo. Nilimwambia kijana kwamba enzi hizo, Bagamoyo ilipokuwa chini ya Wakoloni wa Kiarabu, eneo hilo palikuwa na lango likionyesha mtu anaingia mjini na kwa wenye nchi.

Misafara ya watumwa, wamisionari na wavumbuzi, wafanyabiashara, walipita katika lango hilo. Kuta  nyingine zilizokuwa upande mwingine wa barabara, zimepotea. Kuta nilizopiga picha ziko kwenye uwanja wa mtu. Zinaweza kupotea kwa kuharibiwa wakati wowote.

Pia kulikuwa na nguzo nyingine pale ‘top life bar’ lakini sasa imebaki moja, nyingine imepotea. Nilielezwa na wahifadhi kwamba eneo linalozunguka Caravan Serai, katika soko, na kule kituo cha mabasi kipya lilitumika kujenga kambi za watumwa. Lakini hakuna anayefahamu hilo.

Katika Idara ya Mambo ya Kale, inayoshughulikia masuala ya historia, hakuna maelezo yanayoonyesha eneo hilo kulikuwa na lango hilo. Hakuna kumbukumbu yoyote.

Nimekwenda Bagamoyo mara kadhaa, kila unapotembelea moja ya kivutio cha historia utapata habari tofauti, aidha itatofautiana na ya zamani, au itapotoshwa kidogo. Inafika mahali unashindwa kuelewa ukweli ni upi.

Baada ya kusoma kitabu cha Henry Morton Stanley anaeleza walipoanza safari walipumzika kwenye shamba la mama mmoja, Gonera wa Kihindi, nje ya Bagamoyo. Lakini safari hii niliambiwa Gonera alikuwa ni askari mlinzi aliyejengewa nguzo pale eneo la Mji Mkongwe na von Wisman mwaka 1898.

Inaonekana Bagamoyo ina maeneo mengi ya kihistoria ambayo hayajawekwa katika historia kuu. Na hili ni kosa la idara husika.

WATAKIWA KUTUNZA MIUNDOMBINU

Na John Banda, Dodoma

Wakazi wa kitongoji cha Msangalalee kata ya Dodoma Makulu Manispaa ya Dodoma wametakiwa kuilinda na kuitunza miundombinu ya maji safi iliyopo kwenye maeneo yao ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mwenyekiti wa kitongoji hicho William Chacha wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kitongoji hicho.

Chacha alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu ambao huwa wanaharibu miundombinu ya maji kwa makusudi na kusababisha adha ya maji katika eneo hilo.

Alimtaka kila mtu kuwa mlinzi wa miundombinu ya hiyo ili huduma hiyo muhimu iwe endelevu kwa kupatikana kila wakati kwaa jili ya manufaa ya kila mmoja.

“Nimepata taarifa kuwa kuna watu wanang’oa mabomba ya maji na kwenda kuyauza kama vyuma chakavu, hilo ni kosa kisheria na kama tukikubaini tutakufikisha mahakamani kwa kosa la uharibifu wa miundombinu ya maji ambapo adhabu yake utaijua hukohuko mbele,” alisema Chacha.

Aliongeza, ni jukumu la kila mwananchi kulinda mabomba hayo ya maji safi kwani ndiyo chanzo pekee cha majisafi katika kitongoji hicho ambacho kimeanza kupata huduma ya majisafi mwaka huu tangu uhuru.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho Lesca Chedego aliipongeza mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini hapa (DUWASA) kwa kuwafikishia huduma hiyo muhimu ya maji wakazi wa kitongoji hicho.

Kitongoji cha Msangalalee kimeanza kupata huduma ya majisafi tangu mwezi wa sita mwaka huu ambapo gharama za mradi huo ziligharamiwa na Duwasa kwa kuweka vituo (Domestic Points (DP)) 6 katika kitongoji hicho.

Mwisho

Hakimu achomwa kisu mahakamani



Shinyanga. Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo eneo la Nguzo Nane, Kata ya Kambarage Mjini Shinyanga, Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu katika shavu lake la kushoto baada ya kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa baiskeli.

Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa na mlalamikaji katika kesi hiyo, Emmanuel Izengo (28), mkazi wa Tambukareli, Shinyanga baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa bila ya mshtakiwa, Daniel Makelezia, mkazi wa Lubaga Shinyanga na mdhamini wake, Marko Nkelezia kuwepo mahakamani.

Katika hukumu yake, Hakimu Nyangoha alisema mshtakiwa atakapopatikana atatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa baiskeli hiyo aina ya Neria yenye thamani ya Sh150,000.

Awali, ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo la wizi lililotokea Agosti Mosi, mwaka huu katika eneo la Nguzo Nane, mshtakiwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu na kufunguliwa kesi namba 460 ya 2013 kabla ya kuachiwa kwa dhamana Agosti 23, mwaka huu huku kesi yake ikiendelea na pande zote mbili zilitoa maelezo.

Hata hivyo, baada ya kutoa maelezo, si mshtakiwa wala mdhamini wake aliyehudhuria mahakamani hapo licha ya kesi hiyo kusikilizwa mara mbili bila ya taarifa yoyote kabla ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo jana.

Kushambuliwa

Baada ya hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani na kuwashika mikono wote waliokuwamo mahakamani humo na kutoka nje.

Ilidaiwa kuwa baada ya dakika 15, Izengo alirudi mahakamani hapo na kudai kuwa ameleta risiti ya kumwonyesha hakimu thamani ya baiskeli yake alipoingia ndani ndipo kelele za Mshauri wa Baraza, Mary Wamba zikaanza kusikika akisema: ‘Njooni jamani hakimu kavamiwa anapigwa’.

Baada ya watu waliokuwa karibu kuingia katika ofisi ya Mahakama hiyo walikuta hakimu ameshacwhomwa kisu katika shavu la upande wa kushoto huku akivuja damu nyingi huku mtuhumiwa huyo akiendelea kumshambulia. Baada ya tukio hilo, wasamaria wema walimpeleka hakimu huyo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako alilazwa kwa matibabu.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya tukio hilo kusubiri hatua za kisheria dhidi yake.