Selemani Uliza akionyesha kitanda cha kusafishia na kuchunguza miili ya marehemu.
Maiti ya Adrian Louis iliokotwa kando ya barabara kuu ya kwenda Lukuledi wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara.
Haikuwa na jeraha lolote. Ndugu zake walipopata taarifa za msiba, waliuchukua mwili na kuusitiri harakaharaka.
Hawakuwa na wasiwasi wowote wa kutaka kujua chanzo
cha kifo cha ndugu yao kwani waliamini kuwa amefariki dunia kwa sababu
ya kuzidiwa na ulevi, kwa kuwa siku zote alikuwa mlevi kupindukia.
Kumbe, walikuwa wamekosea, kwani siku hiyo Louis hakuwa amelewa, bali
kifo chake kilisababishwa na majambazi waliompora fedha kabla ya
kumnyonga hadi kufa.
Yapo matukio mengi ya namna hiyo katika sehemu
mbalimbali nchini, lakini mengi kati ya hayo hayafanyiwi uchunguzi wa
kujua chanzo.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa na
Kiongozi wa Idara ya Uchunguzi wa Vifo katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Innocent Mosha anasema ni muhimu kufanya uchunguzi wa
sababu za kifo ili kujiondolea shaka au wasiwasi wa kipi kilisababisha
kifo hicho.
Dk. Mosha anaelezea maana ya uchunguzi wa kifo na
kusema kuwa ni kitendo cha madaktari kutafuta chanzo kilichosababisha
kifo cha mtu na kujiridhisha au ndugu kuridhika pasipo shaka.
“Watanzania walio wengi bado hawafahamu umuhimu wa
kufanya uchunguzi wa vifo vya ndugu zao, jambo ambalo linasababisha
wakati mwingine kupoteza ushahidi au kukosa cheti cha kifo ambacho kina
umuhimu mkubwa katika masuala ya mirathi,” anasema Dk Mosha
Anasema uchunguzi wa kifo si kwa ajili ya polisi
wa upelelezi tu, bali ni mchakato unaotakiwa kufanywa na ndugu wa
marehemu ili kujiridhisha na sababu ya kifo cha ndugu yao.
Anaongeza kuwa tatizo kubwa hapa nchini ni kuwa
watu wengi hawaelewi maana na umuhimu wa kuchunguza miili ya ndugu zao
ili kujua chanzo au sababu za vifo vyao.
Mchakato wa Uchunguzi
Kwanza, Dk. Mosha anasema uchunguzi wa kifo kwa
matukio yanayohusisha polisi, huhitaji taarifa ya utangulizi ambapo
polisi hutakiwa kutoa maelezo ya awali kuhusu marehemu.
Anasema pia kuwa katika matukio hayo, ndugu zaidi
ya mmoja huhitajika kwa ajili ya kumtambua marehemu, sanjari na
kujaza fomu ya maelezo mafupi. “Baada ya polisi kutoa maelezo yao ambayo
kwa kawaida huwa ni mafupi, daktari huendelea na uchunguzi wake
kulingana na ujuzi wake,” anasema.
Anaeleza kuwa zipo hatua kadhaa za kufanya uchunguzi wa kifo
ambazo hazina budi kufuatwa. Anazitaja kuwa marehemu huchunguzwa
sehemu za nje za mwili akiwa na nguo zake.
“Hapo daktari huangalia mazingira ya nje, kwa
mfano nguo alizovaa; iwapo zina damu; damu imeingiaje, kama zimechanika
na zilikuwa katika mazingira gani. Utambuzi huu wa awali wakati
marehemu amevaa nguo zake, huweza kutuonyesha mazingira ya nje iwapo
kulikuwa na purukushani kabla ya kifo au la,” anasema.
Baada ya hapo, Dk. Mosha anasema daktari hutakiwa
kwenda hatua ya pili ya kuchunguza ndani ya mwili ambapo mwili wa
marehemu huchunguzwa kwa umakini mkubwa kama kuna chochote
kitakachoashiria sababu ya kifo chake.
Kwa mfano, Dk. Mosha anasema majeraha ya mwili huangaliwa, pia mazingira ya majeraha hayo.
Anaongeza kuwa hapo daktari anaweza kujua iwapo marehemu alipigwa alizama majini, alikunywa maji mengi au kuzamishwa majini.
“Kama mtu amezama majini ni rahisi kujua kwani
macho yake huwa na mshipa midogo midogo iliyovilia damu. Mwingine huwa
na kitu kinachoitwa ‘Perypheral discoloration’ ambapo kisigino cha
marehemu huwa na rangi ya bluu kwa sababu ya kukosa hewa ya oksijeni.”
Mtaalamu huyo anasema wakati mwingine uchunguzi wa vifo hivi ni muhimu
kwani husaidia kujua iwapo mtu amefia majini au aliuawa, kisha akatupwa
kwenye maji.
Uchunguzi wa mwingine wa vifo vya marehemu huweza
kuhusisha kumpasua mwili na kisha kuangalia ogani kama ini, figo,
mishipa ya damu, utumbo na kifua.
Pia, mwili wa marehemu huangaliwa kama kuna
uvimbe usoni, mapafu kujaa maji na wakati mwingine mapafu hutolewa na
kupimwa kama yameingia maji na maji hayo ni ya aina gani.
Kuna watu wanaofariki wanaodhaniwa kuwa
wamejinyonga kuna utaalamu wa kuangalia kama kweli wamejinyonga au
walinyongwa na kutundikwa.
Anasema uchunguzi wa kifo cha marehemu si lazima
kuukatakata mwili, bali wakati mwingine wataalamu wanaweza kuchukua
maelezo au kukata sehemu ndogo tu ya mwili huo.
“Wakati mwingine iwapo mgonjwa amefariki dunia kwa
kuugua malaria au aliletwa hospitali akiwa anaumwa ugonjwa huo na kama
amekufa, basi ili kuthibitisha sababu ya kifo hicho, tunaweza kukata
tishu kuangalia dalili za malaria katika mwili, kuangalia rangi ya
manjano katika macho au wakati mwingine kipande cha ini kinachunguzwa,”
anasema.
Gharama za uchunguzi
Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Muhimbili, Dk. Praxeda Ogweyo
anasema gharama za uchunguzi kwa watu wa kawaida ni Sh200,000, lakini
kwa raia wa kigeni ni 800,000. Anasema kwa madaktari wanaotaka kufanya
uchunguzi wa vifo kwa sababu za kitaaluma hawatozwi gharama zozote na
kwa polisi gharama zao hulipwa na serikali.
Dk. Ogweyo anasema ni wakati kwa Watanzania
kujifunza na kuujua umuhimu wa uchunguzi wa vifo vya ndugu zao kwa kuwa
husaidia kusuluhisha migogoro ndani ya familia.
“Kama ndugu wanahisi kuwa kifo cha ndugu yao kina
utata basi uchunguzi unasaidia. Mara nyingi mtu anapofariki ghafla
huleta utata kwa jamii,” anasema
Dhana au mazoea
Dk. Mosha anasema kuna dhana zilizozoeleka kuwa
kama mtu ameuawa, basi sura ya muuaji huonekana kwenye macho ya
marehemu, lakini anasema hilo halina ukweli kwani kinachoonekana
machoni ni kuvilia kwa damu au kuvimba kwa macho kwa sababu kama za
kunyongwa.
Takwimu za uchunguzi
Kuhusu hilo, Dk. Mosha anasema Watanzania wengi
hawafanyi uchunguzi wa vifo vya marehemu ndugu zao kwa sababu ya dhana
potofu kuwa ndugu zao hukatwakatwa au kuibiwa baadhi ya viungo. “Wengi
wanaochunguza vifo vya marehemu ni polisi kwa sababu za kipolisi na
madaktari kwa sababu za kitaaluma. Lakini watu wa kawaida bado hawana
uelewa kuhusu uchunguzi wa vifo.” Kwa mfano, takwimu za hapa Muhimbili
zinaonyesha kuwa uchunguzi wa vifo vya marehemu unaofanywa kwa maombi
ya ndugu ni watu wawili hadi wa tatu kwa mwezi wakati uchunguzi
unaofanywa kwa maombi ya polisi ni matukio sita hadi saba kwa wiki.
Sababu za kuchunguza miili
Dk. Mosha anasema, uchunguzi wa miili ya marehemu una umuhimu mkubwa katika kufahamu sababu za kifo na kujiridhisha.
Lakini pia, uchunguzi huu huwasaidia madaktari
kujifunza kutorudia makosa ya kitabibu au kujua kifo kilisababishwa na
nini wakati wa matibabu. “Kwa mfano mtu aliyepata ajali akaumia kichwa,
madaktari huangalia jeraha la kichwani pekee. Hata hivyo, baadaye
uchunguzi wa kifo huonyesha kuwa utumbo wa marehemu ulipasuka na ndicho
chanzo cha kifo, tunajiridhisha,” anasema.
Sheria na uchunguzi wa kifo
Kisheria, uchunguzi wa kifo cha marehemu unatakiwa kufanyika ndani ya saa 24 iwapo mgonjwa alikuwa akiugua maradhi kama malaria.
“Iwapo mtu amefariki dunia halafu kuna daktari alikuwa
akimwangalia, basi uchunguzi wake unatakiwa kufanyika ndani ya siku 14
na hapa si lazima kumpasua marehemu.
Kisheria, wiki mbili zikipita hata daktari
aliyekuwa akimtibu hawezi kumfanyia ‘post- mortem’ kwani hana nguvu za
kisheria kufanya hivyo,” anasema.
Wakili wa Kujitegemea wa Kampuni ya Kakamba and
Partners, Mathew Kakamba anasema kisheria uchunguzi wa kifo husaidia
kupata uthibitisho wa kina kuhusu chanzo au sababu ya kifo.
“Kama watu wanadai marehemu alinyweshwa sumu, basi
ripoti ya post-mortem (uchunguzi baada ya kifo) huleta kithibitisho
kama ni kweli ni sumu na ni sumu ya aina gani na imesababisha vipi
kifo,” anasema
Anasema ripoti hii huondoa utata. Huweza kubadili mwelekeo wa kesi.
No comments:
Post a Comment