Chuchu bandia humfanya mtoto kuugua, kushindwa kuzungumza


Matumizi ya cha chuchu bandia zenye jina maarufu la ‘soother’ yanaonekana yakishika kasi katika miaka ya karibuni kutoka katika fikra kwamba ni ya familia tajiri hadi kwa jamii ya kipato cha chini.

Matumizi haya yamekuwepo pasipokujua madhara ingawa wengi wanaamini vina faida nyingi za kuwafanya watoto kuwa watulivu na wasio na usumbufu kwa wale wanaowalea.

Hivi sasa imekuwa ni biashara pendwa kwa wauzaji wa vifaa vya watoto, kwani kinamama wengi wamekuwa wakiwanunulia na sasa inaonekana ni suala linaloendana na wakati.

Kwa sasa vifaa hivyo havitumiki tu kwa familia tajiri kwani vinapatikana kwa wingi na bei yake ni rahisi kiasi cha kufanya tabaka la kati na la chini kumudu kuvinunua kwa ajili ya watoto wao.

Wengi wamekuwa wakihadaika na faida chache zipatikanazo kama kumzubaisha mtoto katika michezo mbalimbali na hata hivyo kumfanya aache kulia ovyo.

Kama ni mama au mlezi ambaye anamlea, hupata muda mwingi wa kufanya shughuli zake bila usumbufu wa mtoto kulialia ovyo. Licha ya hivyo wengi wanapendelea soother kwa kuwa zinawafanya watoto wapendelee chakula sana kutokana na kukinyonya kwa muda mrefu.

Wakati mwingine wanawake wengi hufurahia kumzubaisha na chuchu hiyo ili asihangaike na ziwa lake na hivyo kumfanya anyonyeshe kwa vipindi anavyovitaka.

Madhara ya ‘soother’

Licha ya faida chache na zisizo na msingi zilizopo, soother zina madhara makubwa kwa watoto wachanga.

Madaktari na wataalamu wa afya za watoto wadogo wameshauri kinamama kuacha kuwapa watoto wao chuchu bandia, kwani kuna athari nyingi zitokanazo na vifaa hivyo maarufu kwa watoto wachanga.

Wataalamu wa afya wameshauri kwamba wanawake wanaweza kutafuta mbinu mbadala kukabiliana na ulizi wa watoto wao na si kutumia njia hiyo.

Mwanataaluma wa Tiba ya Magonjwa ya Binadamu, Samuel Shita anasema mara nyingi watoto wachanga wanaopewa chuchu bandia katika wiki za kwanza za maisha yao huwa hawapendi kuendelea kunyonya kwa kuwa humpunguzia hamu ya ziwa. Ubongo wa mtoto unapaswa kuzoea kwanza chuchu za mama.

“Mtoto anapoanza kupewa chuchu bandia mapema, humfanya kukosa hamu ya ziwa la mama na kwa kuwa muda mwingi huishi na chuchu hii bandia halafu hatimaye anajikuta akiizoea zaidi kuliko ile ya mama,” anasema Shita.

Anasema wanawake wengi hupatwa na matatizo ya kuwanyonyesha watoto wao katika wiki ya kwanza baada ya kujifungua.

Anasema sababu kubwa husababishwa na njia isiyokuwa sahihi ya kunyonyesha au kushindwa kuwapakata watoto wao wakati wa kunyonyesha kutokana na sababu mbalimbali.

“Tatizo hili husababisha kuwapa watoto wao chuchu bandia na wakati mwingine inaweza kuwa maziwa mbadala maana mtoto lazima atanyonya kwenye chuchu bandia. Kutumia chuchu bandia huathiri mafanikio ya suala zima la kunyonyesha,” anasema.

Daktari wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Dk Halifa Mkumbi anashauri kinamama kuwanyonyesha watoto wao na kuepuka kuwapa chuchu hizo bandia.

Anasema maziwa ya mwanzo yana umuhimu mkubwa katika ukuaji wa mtoto na kumwepusha na magonjwa mbalimbali katika kipindi cha utoto.

Dk Mkumbi yeye anasema wanawake wengi ambao wanafanya kazi wamekuwa wakisumbuliwa sana na tatizo la watoto wao kupata homa za mara kwa mara, lakini asilimia kubwa inatokana na chuchu bandia.

“Ukiangalia watoto wanaoongoza kwa kuumwa kila siku ni wale wa wafanyakazi. Mara nyingi mama zao wanawaacha na waangalizi, lakini chuchu bandia wanazopewa hazizingatii kanuni za usafi hivyo kumsababishia mtoto magonjwa ya tumbo,” Dk Mkumbi.

Anasema kwamba watoto wanaotumia chuchu bandia wanakosa kunyonyeshwa ipasavyo na hivyo kukosa kinga za kutosha mwilini.

Hali hiyo, anasema husababisha kupatwa na magonjwa ya milipuko ya mara kwa mara kama kuharisha na homa kali.

Madhara ya chuchu bandia

Moja kati ya madhara makubwa ambayo hayaonekani kwa wakati huohuo ni mtoto kushindwa kuzungumza kwa muda mwafaka.

Hali hii hutokana na kukosa muda wa kujifunza kuzungumza maneno kadhaa yakiwamo tata, dada, mama na minong’ono kadhaa anapokuwa mchanga. “Mtoto ana hatua zake katika ukuaji. Unapompa mtoto ‘soother’ unamnyima nafasi ya yeye kuweza kuzungumza maneno ya awali.

“Maneno haya ya awali ndiyo yanayoanza kuumba matamshi ambayo mwishowe mtoto huyatamka katika kuumba maneno. Utaratibu huo humfanya aweze kuzungumza kwa wakati,” anasema Shita.

Anasema anapoendelea kunyonya kwa muda mrefu huathirika pia kisaikolojia kwa kuiona soother kama moja ya kitu chake cha lazima. Hivyo watoto wengine hushindwa hata kulala kwa kuwa tu wamekikosa kifaa hicho.

“Kinamwathiri pia kisaikolojia. Wapo watoto leo hii hawawezi tena kulala kwa kuwa tu wamekosa kifaa hiki,” anasema Shita na kuongeza:

“Wengi wao wamepata michubuko mikubwa kwenye fizi. Unajua chuchu bandia ni ngumu na si laini kama chuchu ya mama.”

“Tatizo lingine ni watoto wanaweza kupata mzio kutokana na vifaa hivi.”

Nini kifanyike

Shita anasema kwa kuwa usafi wake ni mgumu sana hasa kwenye kitundu cha kutolea maziwa kwa wale wanatumia chuchu bandia za kunyonyea maziwa mbadala.

“Kinamama wengi hawana uelewa mzuri jinsi ya kusafisha. Kila siku utaishia hospitali mtoto akiharisha. Pale inapolazimu, mtoto apewe maziwa kwa kikombe chenye mdomo mkubwa,” anashauri.

Dk Mkumbi anasema ni vizuri kinamama wakashauriana na wataalamu wa afya kuhusu mambo ambayo yanafaa kwa watoto wao na siyo kusikiliza au kuiga mambo yanayofanywa na wengine mitaani.

Sitta, Mbowe vitani

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta akisisitiza jambo juzi, baada ya mkutano wa Kamati ya Maridhiano uliofanyika jijini 
Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiazimia kuzifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwabana wajumbe wa Bunge hilo ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), viongozi wa kundi hilo wamesema hawatishwi na uamuzi huo na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo.

Kikao kilichokuwa kiwe cha mashauriano kilichoitishwa juzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta kiliazimia kuzifanya marekebisho baadhi kanuni za uendeshaji kwa lengo la kusimamia nidhamu wajumbe wake, hatua inayotafsiriwa kwamba inawalenga Ukawa.

Jana Sitta akizungumza na Mwananchi Jumamosi alisema mabadiliko yanayokusudiwa kufanywa yatahusisha masuala ya nidhamu, yakiwamo fujo na utoro, mambo ambayo hivi sasa hayawezi kudhibitiwa moja kwa moja na mwenyekiti wa Bunge hilo.

Sitta alikuwa akitoa ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake jana na kusomwa mbele ya waandishi wa habari na Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad, ikieleza maazimio ya kikao ya usuluhishi alichokuwa amekiitisha kwa ajili ya kutanzua mzozo unaotishia kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Hata hivyo, Ukawa unaoundwa na wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka Vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, CUF na baadhi ya wajumbe kutoka Kundi la 201 walioteuliwa na Rais, walisusia kikao hicho na kusababisha uamuzi uliofikiwa kuwa wa upande mmoja.

Hata hivyo, wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti, viongozi wa Ukawa ambao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na yule CUF, Profesa Ibrahim Lipumba walisema hawatishwi na mabadiliko ya kanuni yanayokusudiwa kufanywa na kwamba wataendelea kususia vikao hivyo hadi hoja zao zitakapozingatiwa.

Ukawa walitoka bungeni siku chache kabla ya kuahirishwa kwa awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu mwezi Aprili mwaka huu, kwa madai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatumia wingi wa wajumbe wake kutaka kufutwa kwa baadhi ya mapendekezo ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.

Kauli ya Sitta

Sitta aliliambia gazeti hili kuwa moja ya kasoro katika uendeshaji wa Bunge ni pale makundi kama Ukawa na Tanzania Kwanza yanapotambuliwa kama makundi rasmi ya Bunge Maalumu, wakati makundi rasmi ni wabunge, wawakilishi na Kundi la Wajumbe 201 wa kuteuliwa na Rais.

“Bunge hili lina uhuru wa ajabu ambao ni mkubwa kuliko Bunge jingine lolote, Bunge ambalo hata uongozi wake hauwezi kumchukulia mtu hatua kwa utovu wa nidhamu eti mpaka umuone mtu anafanya makosa, umpeleke kwenye Kamati ya Kanuni na hivyo ndiyo inakuwa imekwisha maana kama ana watetezi wake wanamtetea,” alisema Sitta na kuongeza:

“Matokeo yake wananchi wanalalamika kwamba hakuna nidhamu bungeni na kwamba kiti kimeshindwa kuchukua hatua, sasa unachukuaje hatua wakati kanuni zetu ndivyo zilivyo?”

Aliendelea: “Yako mambo mengi yanapaswa kufanyika na tuna siku 63 tu za kukamilisha kazi tuliyopewa sasa hatuwezi kutumia fedha za umma na watu wengine wanafanya mzaha, leo huyu anachukua posho, mara anaondoka, haya mambo lazima yatafutiwe dawa.”

Kauli hiyo ya Sitta inaungwa mkono na taarifa iliyotolewa mapema jana ikisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge kutokuwa na vipengele vinavyozuia utoro, ukosefu wa nidhamu na matendo mengine yanayolenga kuvuruga mchakato wa Katiba, ni kasoro ambayo lazima itafutiwe ufumbuzi katika kikao kijacho.

Taarifa hiyo inasema kitendo cha Ukawa kuendelea kususia Bunge, kinapuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini na juhudi za usuluhishi za kutaka kuwezesha vikao vya Bunge hilo viendelee.

“Mambo hayo yote yanazua mashaka kuhusu lengo la wasusiaji kwamba pengine ajenda ya viongozi hawa ni nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba. Kwa mtindo huu wa kususa ni vigumu kuweza kupata mwafaka” inasomea sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Sitta.

Mbowe na Lipumba

Akizungumzia uamuzi huo, Mbowe alisema haamini kwamba kauli kama hizo zimetolewa na Sitta ambaye ni msomi na mwanasiasa mzoefu anayefahamu misingi ya hoja na maridhiano.

“Kanuni hazitungi Katiba, Katiba inatungwa na utashi wa wale tuliopewa dhamana ya kufanya kazi hiyo, sasa ni kwa bahati mbaya kwamba Sitta anafikiri vitisho vya kutunga kanuni za kutubana vitasaidia, haviwezi kusaidia chochote,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Ukawa hatutishwi na mabadiliko ya kanuni, waende wakabadilishe ili dunia nzima iwashuhudie wakipitisha Katiba ya upande mmoja, wasikwepe hoja wanapaswa kutafakari mantiki ya hoja zetu na siyo kutoa vitisho vya kutulazimisha kwenda bungeni, Katiba ni hiari na wala haitungwi kwa vitisho.”

Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisema Bunge Maalumu la Katiba haliwezi kubadili kanuni ili kumbana au kumfuta mjumbe wa Bunge hilo bila kwanza kubadilishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

“Kwanza, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inatakiwa kufanyiwa marekebisho na Bunge la Jamhuri ya Muungano na siyo Bunge Maalumu la Katiba. Pili, hata Rais aliyeteua wajumbe 201 wa Bunge la Katiba hawezi kuwafukuza kwa sababu haijaelezwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sasa Bunge la Katiba litaweza vipi kuwafukuza,” alihoji.

Profesa Lipumba alisema wajumbe 201 waliteuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kufafanua kuwa hata wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi nao hawawezi kufukuzwa kwa kubadilishwa kwa kanuni za Bunge la Katiba.

“Mbunge wa Jamhuri ya Muungano au Baraza la Wawakilishi ili apoteze sifa za kuwa mjumbe wa Bunge la Katiba ni lazima kwanza apoteze sifa za kuwa mbunge,” alisema.

Alisema kuwa msimamo wa Ukawa ni kutoshiriki kikao cha Bunge hilo hadi hapo wajumbe wote 629 wa Bunge hilo watakapokubaliana kuheshimu Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi yenye msingi wa muundo wa serikali tatu na siyo serikali mbili.

Mapema katika taarifa iliyosainiwa na Sitta kisha kutolewa kwa waandishi wa habari na Hamad, inaeleza kuwa vikao vya Bunge Maalumu hilo vitaendelea mpaka mwisho hata kama Ukawa wataendelea kususia vikao vyake.

“Kuanzia Agosti 5 Bunge liendelee kwa kuzingatia upya baadhi ya kanuni zake ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kuwa kazi ya kujadili na kupitisha Katiba inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, yaani 60 za nyongeza na tatu pungufu ya zile siku 70 za awali,” inasomeka taarifa hiyo.

Hamad alisema kikao cha juzi kimeamua Bunge hilo kuendelea kutokana na kuwa na masuala mengi muhimu ya kikatiba ambayo yanawaunganisha Watanzania, yakiwamo usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi, kuikarabati Tume ya Uchaguzi (Nec), kurekebisha kikatiba masuala ya muungano na ukomo wa vipindi vya uongozi.

Taarifa hiyo ilieleza kukerwa na mikutano ya Ukawa inayofanyika katika mikoa mbalimbali nchini. “Hatua ya baadhi ya wajumbe wa Ukawa kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo mwafaka na siyo wakati wake. Bunge la Katiba liwajibike katika siku za usoni kujibu upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa Katiba kadiri ulivyojitokeza” alisema Hamad.

Wapalestina wakimbia Gaza kaskazini

Wapalestina wahama Gaza kaskazini
Mamia ya Wapalestina wamekuwa wakikimbia sehemu za kaskazini za Gaza, baada ya Israel kuonya kuwa italenga sehemu hiyo katika mashambulio yake ya sasa.

Umoja wa Mataifa umenukuliwa ukisema kuwa watu kama 4,000 tayari wameomba hifadhi katika hifadhi ya muda.

Jumamosi usiku mashambulio ya ndege za Israel yaliendelea Gaza.

Wapalestina zaidi ya 160 wameuwawa hadi sasa.

Hamas imerusha makombora zaidi dhidi ya miji ya Israel pamoja na Tel Aviv; hakuna mtu aliyekufa Israel.

Israil ilisema wanajeshi wane walijeruhiwa waliposhambulia eneo ambapo makombora yakirushwa.

Hamas inasema wanajeshi wa Israil hawakuwahi kufika ardhini.

Watu 17 wa familia moja wafariki Gaza

Makombora ya Israel yalipua majumba katika eneo la Gaza

Maafisa wa Palestina wanasema kuwa watu kumi na saba wa familia moja wameuawa baada ya makombora ya Israel kuharibu nyumba moja ya ghorofa tatu ya mkuu wa polisi wa Hamas.

Tayseer Al-Batsh anadaiwa kujeruhiwa katika shambulizi hilo.

Mashambulizi hayo yanajiri baada ya wapiganaji wa Hamas kurusha makombora ya masafa marefu katika miji ya Israel ikiwemo Tel Aviv.

Maafisa wa Israel wanasema kuwa makombora mawili ya Roketi yalirushwa kutoka lebanon lakini yakaanguka katika eneo lililo wazi kazkazini mwa Israeli.

Na katika hatua ya kulipiza kisasi ,Israel ilirusha makombora nchini Lebanon na kuzidisha hofu kwamba huenda mzozo huo ukapanuka.

Takriban raia 150 wa Palestina wameuawa katika mashambulizi hayo huku ikiwa hakuna vifo vyovyote vilivyoripotiwa nchini Israel.

Mgomo mwengine wapamba moto A Kusini

Wanachama wa NUMSA
Wachimba migodi wa Afrika Kusini wamekataa nyongeza ya mishahara iliyopendekezwa na makampuni ya migodi.

Chama cha wachimba migodi, NUMSA, chama kikubwa kabisa cha wafanyakazi Afrika Kusini, piya kimetishia kuwaomba maelfu ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali kujiunga na mgomo wao.

Wanachama wa NUMSA, katika sekta ya chuma cha pua na kutengeneza mashini walianza mgomo kama wiki mbili zilizopita - na kusababisha kiwanda kimoja cha kutengeneza zana za magari kufungwa; na kuzusha hofu kuwa uchumi wa Afrika Kusini unaweza kuzorota tena.

Mgomo huu wa sasa umeanza punde baada ya wachimba dhahabu nyeupe kurudi makazini baada ya mgomo wa miezi mitano.

Busara ya Ukawa sasa inahitajika

Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika kwa wakati tulionao. Ikiwa yatakosekana kupatikana mwakani, anaweza akatokea rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango wa kuunda katiba mpya hadi miaka 50 mingine ipite na kuiona iliopo inafaa na kukidhi haja.PICHA|MAKTABA 
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi


Sauti za viongozi wa kisiasa, kiserikali na madhehebu ya dini kuwaasa na kuwasihi Ukawa warejee bungeni zimesikika, kazi sasa ni kwa wajumbe wa kundi hilo kuitikia wito huo au kuziba masikio.

Matamshi ya viongozi hao kwa nyakati tofauti, yameeleza wazi na kuwataka wabunge hao kutengua misimamo yao na kurejea bungeni ili kuchuana, kushindana kwa hoja na kukosoana wakiwa ndani ya Bunge, si nje ya chombo hicho cha kikatiba na kisheria au kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.

Viongozi hao kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa itakuwa busara ikiwa upande wa wabunge waliobaki ndani ya Bunge na wale waliotoka nje, wakakaa pamoja kwa kuzitumia kamati ya mashauriano, iliyopo.

Miongoni mwa viongozi waliotoa wito wa kuwataka Ukawa warejee bungeni ni Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Hussein Mwinyi.

Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Askofu wa Kanisa la Katoliki Jimbo Iringa Tarcius Ngalalekumwa na Mufti Mkuu wa Bakwata Sheikh Shaaban Bin Simba.

Hata hivyo Ukawa wameeleza kuwa wamelisusa Bunge la Katiba, baada ya kujitokeza matusi, kejeli na maneno ya ubaguzi kutoka kwa wajumbe wa CCM, ambao wanadaiwa kuwa waliacha kujadili hoja za msingi na kuanza malumbano kinyume na dhamira ya kuundwa Bunge maalumu la Katiba.

Pia wanaeleza na kutoa masharti kuwa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ijadiliwe kama ilivyo, isipunguzwe kipengele wala kifungu chochote na kwamba ushauri au maoni ya Tume yabaki vilevile kama yalivyo bila ya kutiwa mikono au kuchakachuliwa.

Madai haya ya Ukawa kwa upande mmoja yanaleta mkanganyiko na kutia hofu. Kazi ya Bunge maalumu la Katiba ni kuipitia rasimu, kuijadili, kuongeza au kupunguza yaliyomo kwa masilahi ya taifa pale inapobidi, si kuwa muhuri wa kuidhinisha matakwa ya tume yatokanayo na makamishna wao kwa kulitumia Bunge, kabla ya kuitishwa kura ya maoni.

Pia Ukawa wanamtupia lawama Rais Kikwete na kumtaja kuwa ndiye chimbuko la kuvurugika kwa mchakato huo, baada ya kutoa maoni yake kama Mkuu wa Nchi.

Dai hili kwa maoni yangu naona kama limekosa nguvu ya hoja kutokana na Rais kuwa na haki ya kutoa maoni kama ambavyo makamishna wa Tume na Mwenyekiti wao walivyotoa.

Rais pia ana haki ya kutoa maoni yake kwa niaba ya chombo anachokiongoza ambacho ni serikali na kwa niaba ya taifa akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Anapotakiwa anyamaze, afumbe mdomo au aache mambo yaende kama yanavyotakiwa na wengine, hapo atakuwa anapoteza sifa ya kuitwa Rais wa Nchi na kiongozi wa Serikali.

Kama alivyosimama Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Jopseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhan na makamishna wa tume hiyo na kushiriki makongamano, semina na warsha nyingine kutetea msimamo wao, rais pia ana haki na wajibu wa kusimamia lile analoliamini kwa niaba ya Serikali.

Madai kwamba Rais amevuruga mchakato wa katiba hayana mashiko na yamekosa uzani wa kusimamia ukweli katika lengo la kumlisha maneno au kumwambia amevuruga zoezi zima la kupatikana Katiba Mpya kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa, wanataaluma na makala za waandishi wa habari.

Sote tumeshuhudia jinsi Rais Kikwete alivyoichambua Rasimu ya Katiba kitakwimu, hoja alizoziainisha, hofu yake kuhusu vipengele alivyovitaja pia wasiwasi wake kama Mkuu wa Nchi kuhusu suala la mabadiliko ya muundo wa Muungano na mabadiliko yake kama inavyotarajiwa iwe kulingana na maoni ya Tume ya Katiba.

Kadhalika wakati mjadala ukianza na wabunge kujadili sura ya kwanza hadi ya sita, pande zote mbili zilikuwa zikitupiana vijembe, mipasho na wakati mwingine kutupiana maneno mazito kinyume na uungwana wa demokrasia.

Madai ya kupatikana Katiba Mpya yamekuwa yakidaiwa na kambi ya upinzani na baadhi ya wadau tangu mwaka 1992 kwa kuelezwa kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikidhi haja, imepitwa na wakati, ina upungufu wa msingi na si ya kidemokrasia.

Malalamiko hayo yakazingatiwa na utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Yamefanyika kwa weledi na utashi, mambo yamewiva, yameonyesha njia na mwelekeo wa kutosha badala yake, Wajumbe wa Ukawa wanatoka na kususia vikao.

Katika rasimu hiyo ya Katiba ukiangalia kwa kina na undani, utajua na kubaini pande zote zinatakiwa kuacha kejeli na mipasho, zijadili hoja, wanachokikataa au kukiafiki waonyeshe kama ni kweli hawakitaki kwa sababu zipi na kuafiki kwa minajili gani badala ya kuweka mbele itikadi na sera za vyama.

Kwa mfano, kabla ya kutoka kwao nje kumekuwa na matamshi kuwa Wajumbe wa CCM madai waliokuwa wakiyatoa Zanzibar kabla ya kufika Dodoma wamefyata na kushangaa hulishwa kitu gani wanapovuka bahari kuja Dar es Salaam hadi Dodoma.

Wengine wakasoma Hansard kuhusu michango ya wajumbe ili kuwasuta na kuelezwa huo ndiyo unafiki na uzandiki.

Upande wa upinzani nao ukatupiwa maneno ya usaliti wa Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar, wakaitwa vibaraka na mawakala wa utawala ulioangushwa mwaka 1964 huku wengine wakiambiwa Zanzibar si kwao na hata rangi zao hazifanani na Afrika,

Wakati akitoka bungeni Profesa Ibrahim Lipumba aliliita Bunge hilo ni la Interahamwe. Tafsiri yake ni mbya sana, haifai kuelezwa au kutamkwa na kiongozi anayeaminika katika jamii mwenye kaliba yake kama msomi na mweledi kitaaluma.

Haya yote hayakustahili kutamkwa ndani ya Bunge la Katiba. Madhali viongozi wa juu wakiwamo wanasiasa na viongozi wa madhehebu ya dini kuwataka Ukawa warejee bungeni, nafikiri ni wakati wao mwafaka Ukawa kukaa na kutafakari ushauri uliotolewa ili warejee bungeni.

Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika kwa wakati tulionao. Ikiwa yatakosekana kupatikana mwakani, anaweza akatokea rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango wa kuunda katiba mpya hadi miaka 50 mingine ipite na kuiona iliopo inafaa na kukidhi haja.

Ikiwa hilo litatokea,kundi la Ukawa halitaachwa kubebeshwa lawama na viongozi wake wataingia katika kurasa za lawama ya kihistoria kwa kutopima wakati na kusoma kuvuma kwa pepo ili kushika turufu na piku mkononi mwao.

Watoaji wa roho za watu ni wengi lakini madereva wamezidi



Kufa kumeumbiwa kiumbe chochote kilicho hai. Kama kilizaliwa basi siku moja kitakufa. Lini kitakufa hakuna ajuaye labda yule aliyepanga mauaji ya kiumbe hicho na wakati mwingine hata yeye muuaji anafikia hatua asifanikiwe katika azma yake hiyo. Kwa sisi wenye imani za dini tunaamini kwamba Mungu alitupa ruhusa ya kutoa uhai wa mimea na wanyama ili kujifanyia chakula. Wapo wanaoondoa baadhi ya wanyama kwamba nao hawaruhusiwi kwa imani zao.

Pia wapo wale wanaoondoa wanyama wote na kubaki na ruhusa ya kutoa uhai wa mimea tu. Katika wote hao sijasikia wanaosema kwamba imani yao imewapa ruhusa ya kutoa roho za watu wengine. Hivyo kila mwenye kuamini kwa imani yake anaamini kwamba mwenye haki na roho ya binadamu ni yeye aliyemuumba yaani Mungu anayemwamini. Pamoja na ukweli huo ambao bahati nzuri wengi wetu tunauamini bado wapo watu ambao wao wanafikiria wamepata ruhusa ya kutoa roho za watu wengine.

Tuwaache wale wenye kupewa kazi ya kunyonga au wanajeshi wanaokwenda vitani ambao hao mjadala wao ni tofauti na hawa ninaowazungumzia. Mimi nazungumzia wale ambao kazi walizopewa ni kuzifikisha roho za watu salama kule ziendako hapa duniani yaani madereva wa mabasi ambayo yanasafirisha abiria. Watu hawa naona wamesahau kwamba wana jukumu hilo. Ajali zinazotokana na magari ya abiria zimekuwa nyingi mno na kwa asilimia kubwa utaambiwa chanzo ni uzembe wa dereva. Hatuwezi kuendelea kuufumbia macho uzembe huu! Ni lazima tufanye kitu kwa madereva hawa waliojiajiri kutoa roho za watu.

Dereva aliyekamilika yaani ni mtu mzima, hajalewa, hana ugonjwa wa akili, kwa jumla anajitambua sawasawa na bila shaka anajua kwamba roho ya binadamu ikitoka haina mbadala. Pia anajua kwamba alichokibeba ndani ya gari hilo kina thamani kuliko vitu vyote ambavyo Mungu ameviumba.

Haiwezekani kabisa kwa dereva kama huyo kuamini kwamba fedha anazozisaka ni muhimu kuliko hao binadamu. Kwanza hata kama anapenda fedha kuliko watu atapata wapi watu wa kumpatia hiyo fedha kama yeye kazi yake ni kuwapunguza kila siku? Kwa sababu hiyo mimi naamini kwamba hawa madereva wanaoendesha magari ya abiria ambao kila kukicha tunawasikia kwa uzembe huu na ule uliosababisha maafa ya kupoteza uhai wa watu, au kuwapatia vilema vya kudumu ni watu wenye hitilafu fulani katika ubinadamu wao kama siyo akili zao.

Maana wewe unajua umebeba roho za watu ambazo hazina mbadala lakini kichwani kwako unachofikiria ni fedha iliyoko katika kituo kinachofuata kiasi kwamba hujali namna unavyoyapita magari yaliyo mbele yako. Akili yako inakuwa imevurugukiwa kiasi kwamba hatari ya kugongana uso kwa uso na gari iliyopo upande huo unaopita huifikirii bali unachokiona ni fedha zilizopo kituo hicho unachokikimbilia.

Nasema huu ni uwazimu kwa sababu pamoja kwamba tunasema binadamu anatakiwa kuthubutu ili apate anachohitaji lakini kuthubutu huko huwa kunafanyika kwa mahesabu; yaani asilimia gani umeweka ya kufanikiwa katika mkakati wako? Ukifanikiwa utapata nini?

Ukikosa utapoteza nini? Sasa katika hali ya kawaida kabisa inaonesha kwamba uwezekano wa kufanikiwa kuyapita magari yaliyo mbele yako bila kupata ajali ni mdogo. Kwa uwezekano huo mdogo bado ni kwamba ukishindwa utapoteza maisha ya watu. Kweli unacheza kamari ya uwezekano mdogo wa kufanikiwa na kupata vinauli dhidi ya uwezekano mkubwa wa kushindwa na kupoteza maisha ya watu? Kama huko siko kukosa hekima ni nini?

Mimi nafikiri wakati umefika sasa wa kupandisha viwango vya watu wanaotaka leseni za udereva wa kubeba abiria. Kama vile ilivyo kwa kazi nyingine nyeti kama usalama wa taifa basi na udereva nao ungechukuliwa hivyo hivyo.

Watu wachunguzwe hata katika maisha yao ya kawaida, namna wanavyoyapokea mambo mbalimbali yanayohusu jamii, namna wanavyofanya uamuzi pale inapobidi wafanye uamuzi kati ya fedha au vitu na watu na mengine. Vigezo hivyo wapewe wamiliki wa vyombo ili kuhakikisha kwamba wanaajiri watu wanaojitambua katika kazi hizo.

Bila kufanya hivyo tutaendelea kuwa na madereva hawa wasiojali, wasiojitambua, wasiokuwa na ubinadamu na ambao wameamua kujiajiri kwenye kazi ya kunyonga watu.

Baada ya hapo sheria pia zirekebishwe kuhakikisha kwamba anayefanya uzembe barabarani na kupoteza maisha ya watu basi asikabidhiwe tena roho nyingine maana yake asiruhusiwe tena kuwa dereva wa magari ya abiria.

Huyo mmiliki wa gari naye asijinasue kwenye mkono wa sheria mpaka hapo atakapothibitisha kwamba yeye alitimiza sehemu yake kwa kuajiri dereva mwenye viwango. Pia anampatia dereva wake huyo mwenye viwango muda wa kupumzika kwa kuhakikisha kwamba haruhusu dereva huo mwenye viwango kuendesha gari toka saa kumi asubuhi mpaka saa sita usiku bila mapumziko.

Kama dereva hana viwango au kama mwajiri hajafanya mpango wa dereva kupumzika kwa kumuwekea dereva mwingine kwa gari linalohudumia zaidi ya muda wa kawaida wa kufanya kazi basi sheria imgeukie mwajiri, naye asiruhusiwe kuhudumia umma katika biashara ya kubeba abiria.

Vita dhidi ya kulawiti na kubaka watoto yawaka moto uzunguni


Leo tuzungumzie watoto. Tuangalie afya, mapenzi na usalama wao. Hakuna kipindi cha historia yetu wanadamu ambapo watoto wanafanyiwa unyama duniani kama sasa.

Machi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) lilisema tangu vita vianze vita Syria, watoto 10,000, wameuawa makusudi. Wengine milioni tano hawana makazi maalumu. Mauaji haya yanafanywa majumbani, mashuleni, mitaani na kambi za wakimbizi. Watoto wanapigwa risasi makusudi na magaidi wa Boko Haram, Nigeria. Miezi miwili sasa wasichana 200 waliotekwa na hawa (wanaotumia dini kama ngao ya uyahawani wao) hawajapatikana. Kila kukicha watoto vijijini na shuleni Nigeria wanauliwa bila hatia yoyote.

Wiki iliyopita mtoto wa Kipalestina, Tarik Abu Khdeir, mwenye miaka 15 alipigwa na askari wa Kiyahudi Jimbo la West Bank nusura afe. Alipokuwa akiongea na wanahabari uso mzima ulikuwa umemvimba utadhani kaota vichuguu vya mchwa. Kipigo kilifuatilia mgogoro kati ya Wapalestina na Wayahudi. Watoto watatu wa Kiyahudi walikokotwa njiani wakakutwa wamekufa kitongoji cha Wapalestina. Serikali ya Israel ilidai Hamas iliwaua. Ili kulipiza kisasi mtoto wa miaka 16 wa Kipalestina, Mohammed Abu Khdeir, naye aliburutwa barabarani, akapigwa kikatili na kutupwa msituni kama fuko.

Ingawa waliohusika wameshakamatwa na askari wa Israel, haisaidii kurudisha maisha ya watoto.

Barani Afrika, nchi zenye vita mathalan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan na Kongo, unyanyasaji wa watoto ni jambo la kawaida. Umoja wa Mataifa umekadiria asilimia 65 ya ubakaji uliofanywa Kongo kipindi cha miaka 15 iliyopita uliwaathiri watoto. Asilimia kumi ya watoto waliobakwa Kongo wana umri chini ya miaka kumi! Mbali ya kubakwa, kupigwa au kulawitiwa watoto hulazimishwa kubeba mizigo na kuwa askari.

Kwetu Tanzania mateso ya watoto- kwa njia mbalimbali- yamefikia daraja la kishetani kwa taifa hili lenye utamaduni mahususi wa amani. Juma lililopita msichana wa kazi za nyumbani, ambaye jina lake halikutajwa (aliitwa tu ‘hausigeli’ utadhani kijiti au kifuu cha nazi) aliteswa miaka miwili na tajiri wake, Boko, Kinondoni. Mateso ya watoto wanaofanya kazi majumbani hayasemeki. Kwa kuwa hawana midomo, haki au cha kuwatetea, hali zao hazifahamiki.

Baadhi ya maoni ya wasomaji kwenye mitandao yanasomeka: “Huwezi kumtesa binadamu mwenzio kiasi hiki hata kama amefanya nini, unampiga kama mwizi, lahaulaa. Ilhali yeye ndiye anayeangalia nyumba yako?”

Au “Yaani ukatili mwanamke unamfanyia mtoto wa mwenzio hivyo au hujawahi kuzaa hujui uchungu? Huyu ni sawa na muuaji hukumu yake ni kifo tu. Je, kama ni mtoto wake alifanyiwa hivyo angejisikiaje?”

Hali inadhirisha ukosefu wa utu na ubinafsi ulioenea leo.

Labda tutasema unyanyasaji huu ni wa waovu wachache tu. Lakini je, watu wazima wenye nafasi zao wanaolala na kuwalawiti watoto kisirisiri?

Hapa Uingereza mwaka mzima sasa ‘tetemeko la habari’ linaendelea kufichua visa vya watu mashuhuri waliowalawiti au kuwabaka watoto.

Mosi alikuwa Jimmy Saville. Mstahiwa alikuwa mtangazaji mashuhuri wa BBC aliyependwa na mamilioni kiasi ambacho hakuna hata mtu mmoja aliyemkisia mabaya. Jimmy Saville na sigara lake kubwa, nywele nyeupe zilizofanana na katani, miwani mekundu juu ya pua nene iliyompa sura ya majigambo na vichekesho alifariki dunia mwaka 2011 akiwa na miaka 84. Baada tu ya mazishi malalamishi na mashtaka zaidi ya 200 yalifanywa na wanawake na wanaume waliodai aliwafanyia uanaharamu wakiwa watoto lakini enzi hizo sheria iliziba masikio. Hawakusadikiwa. Wengine wanne walidai aliwachezea wakiwa na miaka kumi. Kutokana na umaarufu wake alipewa ufunguo akaruhusiwa kuingia hospitalini kutumbuiza wagonjwa ambao aliwanajisi na kuwafanyia uchafu. Aliingia vyumba vya vilema na maiti. Karibuni madai yameongeza kusema Bwana Saville alihusudu kulala pia na maiti. Alifanya vituko hivi tangu mwaka 1964.

Baada ya habari za Jimmy Saville kuzagaa, watu wengine maarufu wanaendelea kushtakiwa. Wiki jana mwanamuziki na mchoraji aliyetunukiwa taji la heshima na Malkia na kuitwa Sir Rolf Harris, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano baada ya kupatikana na hatia 12 za kulala na watoto. Madai yanasema Bwana Harris mwenye umri wa miaka 84 alianza ufuska wake miaka 40 iliyopita. Tarakilishi au kompyuta zake zilikutwa na picha zaidi ya 200 za watoto wadogo wakiwa uchi.

Wakati mashtaka yakiendelea Serikali imetangaza mabomu mawili. La kwanza lahusu viongozi serikalini. Mwaka 1983 enzi za uongozi wa marehemu Margaret Thatcher uchunguzi uliofichua ulawiti na ubakaji wa watoto ndani ya mashirika makubwa ya hospitali, BBC na serikalini ulizimwa. Aliyepewa mafaili ya uchunguzi Bwana Leon Brittan, tajiri- mbunge na Waziri enzi hizo-inadaiwa aliyaharibu mafaili ya mashtaka. Wiki jana Serikali iliamuru uchuguzi ufanywe na maofisa saba wa polisi wameteuliwa kuusimamia.

Bomu la pili ni ukeketaji. Alhamisi Julai 3, Serikali ya Uingereza iliwaamuru waganga, walimu na wafanyakazi wa taasisi za umma kutotetereka kuzuia ukeketaji eti kwa sababu za kitamaduni. Tangu sheria ilipopitishwa kutokomeza desturi hii mwaka 1985 hakuna aliyeshtakiwa hadi mwaka huu.

“Ukeketaji ni uhalifu. Siyo suala la kikabila bali utesaji. Siyo jando unyago bali unyanyasaji.” Kamati husika ya Wizara ya Uhamiaji ilitamka. Baraza la Waislamu Uingereza nalo lilitoa taarifa iliyopinga vikali ukeketaji na kusema Uislamu hauafiki kitendo hicho.

Wenzetu wameamua vita kutetea watoto.

Je, sisi Afrika?Ukeketaji, ubakaji na kulawiti watoto vinaendelea kisirisiri (na wazi) mijini na vijijini Tanzania. Sababu kuu ni umaskini na watoto wengi kutokwenda shule. Watoto kulazimika kulala nje au kuishi maisha ya dhiki. Pili, woga umeenea. Wahusika hawasemwi. Vyombo husika huficha au kutumia mabavu kuuzima moto.

AL Shabaab washambulia ikulu Somalia


wapiganaji wa AL shabaab

Vikosi vya serikali Somalia vimefanikiwa kuidhibiti upya ikulu ya rais katika mji mkuu Mogadishu baada ya hapo awali wapiganaji wa kiislamu kuishambulia.

Maafisa wanasema washambuliaji wapatao watano kutoka kundi la al-Shabab - waliuawa walipoingia katika eneo la ikulu hiyo.

Washambuliaji hao wanadaiwa kulipua bomu lililotegwa kwenye gari karibu na langu kuu la Ikulu hiyo.

waziri wa habari wa Somalia Mustaf Dhuhulow

Waziri wa habari na mawasiliano wa Somalia Mustaf Dhuhulow ameambia BBC kuwa tayari mmoja wa washambuliaji hao amekamatwa na anahojiwa na polisi.

Waziri Mustaf amesema, '' Walishambulia ikulu ya rais saa za jioni. Alikuwa watu washambuliaji watatu pamoja na dereva wao. Washambuliaji hao waliuawa lakini dereva wao alipata majeraha madogo na anazuiliwa na polisi na kuhojiwa. Walijaribu kuvamia Villa Somalia lakini wakakomeshwa. Tutawapa maelezo zaidi baadaye. Na tutaweza kutoa maelezo zaidi kwa raia wa Somalia na dunia nzima.''

Shambulio la Al shabaab Mogadishu

Hii ni mara ya pili kwa Al Shabaab kuvamia ikulu ya rais mjini Mogadishu mwaka huu japo mara ya kwanza walifanikiwa kuingia ndani.

Rais Hassan Sheikh Mohamoud hakuwepo wakati wa shambulio hilo.

Kundi la wapiganaji wa kiislamu Al shabaab limefukuzwa kutoka mjini Mogadishu tangu mwaka wa 2011 lakini limekuwa likifanya mashambulio ya kuvizia tangu wakati huo.

Wanamgambo hao wanaaminiwa kufanya mashambulio kadhaa pia katika nchi jirani ya Somalia kama vile Kenya, Uganda na Tanzania kama njia ya kulipiza kisasi kwa kuingia majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia.

January Makamba, Zitto waungana urais

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (kulia) akimweleza jambo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Picha na Maktaba 
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi


Dar es Salaam. Uamuzi wa mwanasiasa kijana, January Makamba wa kutaka kuwania urais, umezidi kukoleza mijadala ya kisiasa katika mitandao ya kijamii na kuibua hoja zinazokinzana kuhusu ujana na uzoefu wa uongozi.

Makamba (40) ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na mbunge wa Bumbuli (CCM), ametangaza kuwa ameamua kwa asilimia 90 kujitokeza kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, akisema asilimia zilizobaki zitategemea mambo kadhaa.

Katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa facebook, Makamba alisema uongozi wa kizazi kipya upo tayari kushika hatamu za uongozi na kuijenga Tanzania mpya, fikra mpya na maarifa mapya.

Alisema mabadiliko yaliyotokea Tanzania, yalidaiwa na kuongozwa na vijana na kwamba vijana nchini wanaweza kushika usukani wa kuleta mabadiliko wanayoyataka.

“Ukiona kijana anamwambia kijana mwenzake hana uzoefu, basi kazi ya kuleta mabadiliko ni kubwa zaidi. Kutokuwa na uzoefu ni sifa ya kijana.”

Alisema kuwa tusi kubwa kwa Rais wa Marekani, Barack Obama mwaka 2008 lilikuwa ni kukosa uzoefu na kukosa rekodi, lakini tusi hilo liligeuka kuwa muziki kwa wapigakura wa nchi hiyo.

“Tanzania mpya inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya. Inahitaji kuthubutu mambo makubwa siyo kulinda uzoefu wa nyuma... tunaweza,” ameandika mwandishi huyo wa zamani wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete.

Akichangia mada hiyo, mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema: “Ni kweli vijana hatuna uzoefu. Uzoefu wa kuiba. Tunataka namna mpya na bora ya kuongoza nchi. Nilipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2005 sikuwa na uzoefu. Kulikuwa na wengi wenye uzoefu, lakini uzoefu wa posho bila kazi.”

Naye William Sunday Sempoli alisema tatizo siyo umri wa mtu. Unaweza ukawa kijana mwenye mawazo ya kizee na unaweza ukawa mzee mwenye mawazo ya ujana. “Tanzania tunamhitaji mtu mwenye uwezo wa kututoa hapa tulipokwama na kutupeleka mbele.”

Kwa upande wake Cleophas Cyprian alisema kabla ya kuchagua vijana mwaka 2015, “Ninyi mliopo sasa ilitakiwa muonyeshe uwezo wenu katika kulipigania taifa kwa matendo na siyo maneno”.

Method Nyakunga akichangia mjadala huo alisema tatizo siyo tu kizazi kipya, alihoji kama mifumo nayo ni mipya? “Kama mifumo ni hii iliyopo basi labda kizazi kipya kitokane na vyama vya upinzani kwani ndani ya chama tawala, kwa namna kilivyo sasa, kimehodhiwa na watu wachafu wa kila aina wanaoangalia masilahi yao.”

Mzalendo Joseph Goliama alisema uko sawa kwa upande mmoja lakini kwa upande mwingine kauli hizo ni za ubaguzi wa rika. Nchi yetu na katiba ya nchi yetu inataka Rais atokane na Watanzania wenyewe.

Mabomu yazidi kutikisa Arusha

Majeruhi Deepak Gupta aliyepoteza mguu wake kutokana na shambulio la bomu lililotokea juzi usiku katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine, jijini Arusha. Picha na Filbert Rweyemamu. 

Arusha/Dar. Milipuko ya mabomu nchini inazidi kuongezeka baada ya bomu jingine kulipuka mjini Arusha na kujeruhi vibaya watu wanane wenye asili ya Kiasia katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine ulioko eneo la Arusha Gymkhana.

Mlipuko huo, uliotokea majira ya saa 4:30 usiku juzi karibu na eneo la Mahakama Kuu, ni wa tano kutokea jijini Arusha baada ya ule uliotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti, kwenye mkutano wa kampeni za udiwani wa Chadema, Baa ya Arusha Night Park na nyumbani kwa Imam wa Msikiti wa Answar Sunna.

Mbali na Arusha, ambayo inategemewa kuingiza fedha nyingi kutokana na sekta ya utalii, mji mwingine ambao umekuwa ukikumbwa na milipuko ya mabomu ni Unguja, ambao pia ni maarufu kwa utalii.

Mlipuko wa juzi ulitokea wakati watu hao walipokuwa wakipata chakula na burudani kwenye mgahawa huo ambao mara nyingi wateja wake ni raia wa kigeni. Mmoja wa majeruhi hao aliyetambulika kwa jina la Deepak Gupta(25), alipoteza mguu wake wa kushoto uliokatwa kutokana na kujeruhiwa vibaya.

Taarifa za mashuhuda zinasema washambuliaji hao walitumia usafiri wa pikipiki katika kutekeleza azma yao.

Mbali na Guptam, majeruhi wengine katika tukio la juzi ni Vinod Suresh, Ritwik Khandelwal, Raj Rajin, Prateek Javey, Manci Gupta, Marisa Gupta na Mahushi Gupta ambao ni ndugu na walipelekwa katika Hospitali ya Selian.

Mkurugenzi wa tiba wa Hospitali ya Selian, Dk Paul Kisanga alisema walipokea majeruhi wanane kati yao wanawake ni watatu ambao baada ya kufanyiwa uchunguzi wameonekana wana vipande vya vyuma kwenye miili yao.

“Kuanzia jana usiku (juzi) tumekua tukiwapa matibabu hadi asubuhi. Wagonjwa wengine wanaendelea vizuri isipokuwa mmoja ndiye amepoteza mguu wake wa kushoto na yuko katika chumba cha uangalizi maalumu,” alisema Dk Kisanga.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari kutokana na milipuko ya mabomu inayoendelea katika baadhi ya maeneo nchini kwa kutoshiriki katika mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu alitoa tahadhari hiyo jana alipozungumza jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kutokea mlipuko huo Arusha.

Kamishna Mngulu alisema tayari jeshi hilo linafanya operesheni maalumu kubaini chanzo cha mlipuko huo wa jana na wameshawakamata washukiwa wawili wanaodhaniwa kuhusika na mlipuko huo.

“Mlipuko huo umetokea siku chache baada ya kutokea kwa mlipuko mwingine wa aina hiyo baada ya bomu kurushwa sebuleni kwa Sheikh Sudi Ally Sudi usiku wa Alhamisi wiki iliyopita na kumjeruhi yeye pamoja na mgeni wake. Kuhusu tukio hilo tulishawakamata washukiwa sita,” alisema

 

Alieleza kwamba wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kubwa na kutilia mashaka kila nyendo za watu wanaokutana nao au wanapokuwa wamekaa katika maeneo ya mapumziko au mikusanyiko.

Alisema wamebaini kwamba wahusika wana mtandao mpana ambao upo nchi nzima na wanaendelea kuuchunguza ili kuumaliza na kuepusha madhara zaidi kwa wananchi.

“Watu wawe makini dhidi ya kila mtu aliye kando yake. Hili ni suala muhimu zaidi katika kujizatiti na kujiepusha na maafa, na wanapobaini au kuhisi mtu asiye mwema wachukue hatua za haraka kuwakwepa na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama,” alisema.

Miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa yakitikiswa na milipuko ya mabomu ni Zanzibar, hatua ambayo inatoa ishara za kuwapo kwa mkakati maalumu wa kuvuruga amani katika miji inayoongoza kwa utalii nchini.

Alieleza kwamba hadi sasa wameshakamata watu wasiopungua 25 wanaohusishwa na milipuko yote iliyotokea Zanzibar na Arusha, huku akieleza kwamba hakuna kikundi kinachoweza kuhusishwa moja kwa moja na milipuko hiyo.

Imeandikwa na Filbert Rweyemamu, Mussa Juma, Arusha na Andrew Msechu, Dar es Salaam

Sitta ateua masheikh, maaskofu kuwarejesha Ukawa bungeni

 Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameanza mkakati mpya wa kunusuru mchakato wa Katiba Mpya kwa kuitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya Mashauriano ili kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.

Katika wajumbe hao wamo maaskofu wawili na masheikh wawili ambao Sitta amewateua kutoka katika Bunge la Katiba.

Sitta ameitisha kikao hicho jijini Dar es Salaam Julai 24 wakati kukiwa na matamko tofauti kuhusu mustakabali wa katiba hiyo, mengi yakieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyeshikilia hatima ya mchakato na wapinzani wakisema mkuu huyo wa nchi ndiye aliyesababisha suala hilo kwenda mrama.

Pia, Sitta ameitisha kikao hicho wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakieleza kuwa suala la serikali mbili kwenye muundo wa Muungano, ambalo liligawanya wajumbe, ndiyo msimamo wa chama na wapinzani wakisema suala hilo halimo kwenye Rasimu ya Katiba na ndiyo sharti lao la kurejea bungeni.

Akizungumza  jana katika mahojiano na gazeti hili, Sitta alisema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja kutazama mwenendo wa majadiliano katika Bunge hilo na sura 15 za katiba ili kujua yapi muhimu yanayotakiwa kupewa kipaumbele kabla ya Bunge la Katiba kuanza tena vikao vyake Agosti 5.

“Sisi tumeshapeleka barua kwa wajumbe, tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo tutaelewana kuhusu masuala hayo na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda ya siri,” alisema Sitta.

Alisema katika mkutano huo, kutakuwa na utaratibu maalumu ambao utahusisha viongozi wa dini walio ndani ya Bunge kutoka madhehebu tofauti na baadhi ya wajumbe wengine kutoka kada tofauti ndani ya Bunge hilo.

“Kutakuwa na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti. Atakayevimba kichwa na kudharau, wananchi watajua kuwa nia yake ni tofauti na katiba,” alisema.

Sitta alisema tatizo kubwa katika Bunge hilo litakalosababishwa na kutokuwapo kwa Ukawa ni  namna ya upigaji kura, lakini iwapo theluthi mbili ya wajumbe itatimia basi watakwenda  kwa mwenendo huo.

“Yapo mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya haki za binadamu, uongozi wa asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar nafasi zaidi katika Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko muundo...ya nini kuyapiga teke yote haya na kujikita katika muundo pekee,” alihoji.

Sitta ambaye pia alipingwa kwa k

“Inashangaza kuona kuwa kila maoni yao yanaposhindwa wanasusa...iwapo watatokea watu ambao wataona Tume ya Uchaguzi haikidhi haja. Je, watatoka nje ya mkutano?” alihoji.

Kubadili sheria

Pamoja na mambo mengine, Sitta alisema upo uwezekano wa Ukawa kurudi bungeni lakini wakasusa tena kadiri mjadala utakavyoendelea. Iwapo itatokea hali hiyo, Bunge litaangalia upya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.

“Katika sheria nyingine hatutakiwi kuangalia idadi. Katika mkutano wa kibiashara au Bunge la Muungano na hata Baraza la Wawakilishi, iwapo kuna wajumbe hawajatimia, basi wasiokuwapo hawahesabiwi,” alisema.

Sitta alishawahi kufanya jitihada za kujaribu kuwarudisha bungeni Ukawa siku chache baada ya kususia, lakini harakati zake ziligonga mwamba.

Lipumba atoa masharti

Wakati Sitta akifanya mkakati huo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesisitiza msimamo wa Ukawa kutorudi bungeni akisema ili warudi upande wa CCM unatakiwa kuheshimu rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba na kuepuka matumizi ya lugha chafu.

“Msimamo wetu uko wazi tu, kwamba Rasimu ya Katiba iheshimiwe. Bunge la Katiba lina kazi ya kujadili na kupitisha Rasimu ya Katiba, kwa hiyo lazima mjadala uongozwe hivyo, siyo vinginevyo,” alisema Profesa Lipumba.

“Kiini cha rasimu ile ni uwapo wa muundo wa Serikali ya shirikisho, yaani serikali tatu. Sasa ukienda kwenye Bunge na kuacha mapendekezo hayo na kuleta serikali mbili, unaitoa wapi?” alihoji.

Maalim Seif amvaa Kikwete

Katika hatua nyingine, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amemtupia lawama Rais Jakaya Kikwete kuwa amechangia kuukoroga mchakato wa Katiba kwa kufuata msimamo wa chama chake badala ya maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba.

Akizungumza katika kipindi cha Dk 45 kinachorushwa na ITV juzi usiku, Maalim Seif alisema kauli alizotoa Rais Kikwete wakati akilihutubia Bunge la Katiba Machi 21, mwaka huu, zimeondoa imani ya wananchi kuhusu kupatikana kwa Katiba inayotokana na maoni yao.

umpanga Rais Kikwete kuhutubia Bunge hilo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba tofauti na kanuni, alisema kuwa kuususia mkutano huo wa Bunge katika kipindi chote hicho siyo hasara kwa CCM, bali kwa wananchi kwa kuwa nia ni kupata katiba bora na wala siyo kukomoana.

“Iwapo Ukawa watasusia kila kitu, basi wataonyesha kuwa siyo wakomavu wa kisiasa,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Urambo Mashariki.

 “Mchakato huu unamtegemea yeye. Hakuna ambaye amekamilika, Rais ajiangalie kama alivyofanya ni sawa,  kama siyo sawa arekebishe mambo ili kujenga tena imani kwa wadau wote,” alisema Maalim Seif.

Alisema mwanzoni, Rais Kikwete alilichukulia suala hilo kwa busara na hekima na alipokuwa akiona mambo yanakwama alikutana na vyama na kusikiliza wanataka nini, lakini baadaye alijisahau na kusikiliza matakwa ya chama chake.

“Mfano ni hotuba yake alipokutana na Baraza la Vyama vya Siasa ilikuwa nzuri, lakini alipofungua Bunge la Katiba akajisahau kama yeye ni Rais wa Watanzania wote akachukua msimamo wa chama chake na kuihujumu Tume ya Katiba na mwenyekiti wake (Jaji Warioba).”

Katibu huyo mkuu wa CUF ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema iwapo Katiba Mpya haitapatikana wa kulaumiwa ni CCM iliyoacha ajenda kuu na kuonyesha ubaguzi wa wazi.

Alisisitiza kuwa Ukawa wanataka kijadiliwe kilichomo katika Rasimu ya Katiba na siyo rasimu ya CCM. Pia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kanuni za Bunge hilo zifuatwe.

Ushirikiano wa Ukawa

Maalim Seif alisema ushirikiano wa Ukawa utaendelea hata baada ya mchakato wa Katiba kumalizika.

“Hii ni pamoja na kuangalia kama tunaweza kuachiana majimbo ya uchaguzi iwapo chama kimoja kitaonekana kina nguvu zaidi kuliko kingine katika eneo fulani,” alisema Maalim Seif.

Alisema kama CCM ikiendelea na mchakato wa kuandika Katiba Mpya ni wazi kuwa Katiba hiyo itakataliwa na wananchi.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Maalim Seif aligusia jinsi viongozi wa juu wanavyoshirikiana katika uongozi, lakini akakiri kuwapo  tatizo katika ngazi za chini, hasa kwa viongozi kutokana kutokuwa na elimu kuhusu uendeshaji wa Serikali hiyo.

Alifafanua kuwa kuna jambo ambalo hawakufanya vizuri wakati wakibadili katiba kuunda SUK kwa kutoweka kamati ambayo itakuwa inazipitia ilani za vyama vinavyounda Serikali ili kutoa ilani moja itayayotekelezwa kwa pamoja.

 “Katiba yetu inasema ilani itakayofuatwa ni ile ya chama kilichopo madarakani. Hapo kidogo hatukufanya vizuri,” alisema.

Uandikishaji wapiga kura

Pia aligusia uboreshaji wa Daftari la Wapigakura na kutolea mfano Zanzibar kwamba zimekuwa zikifanyika njama ili wanachama wa CUF wasiorodheshwe katika daftari hilo.

“Ili ujiandikishe Zanzibar katika daftari, lazima uwe na kitambulisho cha ukaazi na ili upate kitambulisho hicho lazima upate idhini kutoka kwa masheha ambao hupewa maelezo na viongozi wa CCM kuwanyima vitambulisho wanachama wa CUF,” alisema.

Imeandikwa na Florence Majani, Elias Msuya na Fidelis Butahe